Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madaraka ni kwa ajili ya kuinua watu si kuwakandamiza - Guterres

Nelson Mandela, Rais wa Afrika Kusini, akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Septemba 1998.
UN Photo/Greg Kinch
Nelson Mandela, Rais wa Afrika Kusini, akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Septemba 1998.

Madaraka ni kwa ajili ya kuinua watu si kuwakandamiza - Guterres

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa leo umeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kwa heshima ya maisha na urithi wa shujaa wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, nchini Afrika Kusini, Nelson Rolihlahla Mandela, maarufu kama Madiba.

Katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa hotuba maalum akisisitiza umuhimu wa kuendeleza maadili na maono ya Mandela ya amani, haki na utu wa binadamu.

“Maisha ya Madiba yalikuwa ushindi wa hali ya juu wa roho ya kibinadamu,” amesema Katibu Mkuu. “Alivumilia dhuluma na ukandamizaji wa hali ya juu, lakini hakujibu kwa kisasi bali kwa maridhiano, amani, na mshikamano.”

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa urithi wa Mandela sasa ni jukumu la kila mkazi wa dunia. Amesema kuwa moja ya mafundisho makuu kutoka kwa maisha ya Mandela ni kwamba mamlaka si mali ya mtu binafsi bali ni chombo cha kuwainua wengine.

“Madaraka ni kuhusu watu — na kile tunachoweza kufanikisha pamoja, kwa ajili ya kila mmoja wetu,” ameongeza.

Washindi wa tuzo ya Mandela 2025 watambuliwa

Katika hafla hiyo, pia walitambuliwa washindi wa Tuzo ya Nelson Rolihlahla Mandela ya mwaka 2025: Brenda Reynolds kutoka Canada na Kennedy Odede kutoka Kenya.

Brenda Reynolds, mshindi wa Tuzo ya Nelson Mandela, akizungumza katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kila mwaka.
UN Photo/Eskinder Debebe
Brenda Reynolds, mshindi wa Tuzo ya Nelson Mandela, akizungumza katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kila mwaka.

Bi. Reynolds ni kutoka jamii ya asili ya Saulteaux nchini Canada. Amejulikana kwa kazi yake kama mfanyakazi wa kijamii aliyeongoza jitihada za kusaidia manusura na familia zilizoathiriwa na mfumo wa shule za mabweni kwa watoto wa jamii ya asili nchini humo.

Kwa upande mwingine, Bw. Odede, ambaye alikulia katika mitaa ya mabanda ya Kibera, jijini Nairobi, Kenya, amekuwa mwanaharakati wa jamii kwa muda mrefu.

Shirika alilolianzisha SHOFCO, limeunganisha makundi mbalimbali ya kijamii nchini Kenya na kufanikisha utoaji wa huduma muhimu kama elimu na maji safi kwa watu zaidi ya milioni 2.4 kila mwaka.

Katibu Mkuu amewapongeza washindi hao kwa kutekeleza kwa vitendo maneno maarufu ya Mandela yaliyoko kwenye tuzo yao:

“Kile kinachojali maishani si kwamba tumeishi, bali ni tofauti gani tumeleta katika maisha ya wengine.”

Miaka 80 ya UN, maono ya Mandela bado yanaongoza taasisi

Akiangazia miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu amesema kuwa maono ya Mandela bado yanaendelea kuongoza taasisi hiyo katika kukabiliana na changamoto za sasa ikiwemo mizozo ya kimataifa, ukosefu wa usawa, mabadiliko ya tabianchi, na kurudi nyuma kwa haki za binadamu.

“Huu ni wakati wa kufufua ahadi yetu kwa misingi inayotutambulisha kama Umoja wa Mataifa, na maisha ya kipekee ya Nelson Mandela: Uhuru, haki, usawa, mshikamano, maridhiano, na amani.”

Katibu Mkuu amehitimisha kwa kutoa wito kwa dunia nzima kuendelea kuiga mfano wa Mandela kila siku, katika kujenga jamii zenye haki, usawa na mshikamano.

Brenda Reynolds, mpokeaji wa Tuzo ya Nelson Rolihlahla Mandela ya Umoja wa Mataifa 2025, akiwa katika picha ya pamoja na sanamu ya hayati Rais wa Afrika Kusini katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.
UN News/Paulina Greer
Brenda Reynolds, mpokeaji wa Tuzo ya Nelson Rolihlahla Mandela ya Umoja wa Mataifa 2025, akiwa katika picha ya pamoja na sanamu ya hayati Rais wa Afrika Kusini katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Kauli ya Bi. Reynolds baada ya kupokea tuzo

Akizungumza baada ya kupokea tuzo ya Mandela, Bi. Reynolds amesema “kupokea tuzo iliyopewa jina la mtu aliyeendesha harakati za upinzani kwa amani na maridhiano ni heshima kubwa na wajibu mzito.”

Reynolds aliangazia safari yake ya maisha kama mshauri wa kisaiokolojia katika shule za mabweni za watu wa jamii ya asili Canada, akisimulia jinsi alivyosaidia waathiriwa wa unyanyasaji wa kingono kufunguka, hatua iliyochangia kesi ya pamoja kubwa zaidi katika historia ya Canada.

Ameelezea jinsi alivyoanzisha mpango wa usaidizi wa kisaikolojia kwa manusura na familia zao, akizingatia mafunzo ya kina kwa wafanyakazi wa jamii, wakijifunza kuhusu athari za muda mrefu za mshtuko wa kihisia hususan ule wa kitamaduni.

Kwa Reynolds, tuzo hii si tu kutambuliwa binafsi, bali ni mwelekeo wa kuendeleza kazi ya uponyaji wa kihistoria na ujenzi wa amani.

“Tumejifunza kutoka kwa Mandela kwamba kuachilia chuki ni mwanzo wa kujenga maisha mapya. Tuliona mabadiliko hayo ndani ya wahanga na familia zao. Tulikuwa tunajenga amani ndani ya mtu mmoja mmoja na familia,” amesema kwa msisitizo.

“Ninawashukuru Umoja wa Mataifa kwa kutambua njia hii ya haki, maridhiano, na uponyaji. Ni safari ya pamoja inayohitaji mshikamano wa kimataifa kwa heshima ya utu, amani, na uponyaji wa pamoja.”

Katibu Mkuu António Guterres (kushoto) akiwa na mshindi wa Tuzo ya Nelson Mandela Kennedy Odede wa Kenya katika mkutano usio rasmi wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kila mwaka.
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu António Guterres (kushoto) akiwa na mshindi wa Tuzo ya Nelson Mandela Kennedy Odede wa Kenya katika mkutano usio rasmi wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kila mwaka.

Kauli ya Kennedy kutoka Kenya

Kwa Kennedy Odede, Mwanzilishi wa Shirika la Shining Hope for Communities (SHOFCO), Kennedy Odede, yeye amesema kupokea tuzo ya Mandela ni heshima kubwa kwa watu wa makazi ya mabanda ya Kibera na jamii zilizopuuzwa kote ulimwenguni.

“Mandela alinifundisha kuwa nguvu siyo ukosefu wa changamoto, bali ni kile tunachojenga ndani ya changamoto hizo,” amesema Odede katika hotuba yake ya kupokea tuzo.

Miaka 20 iliyopita, Odede alianza harakati zake kwa kununua mpira wa miguu kwa akiba ya senti ishirini kutoka mshahara wa chini ya dola moja kwa siku. Mpira huo haukuwa kwa ajili ya burudani tu, bali ulikuwa chombo cha kuunganisha vijana wa Kibera na kupalilia ndoto ya mabadiliko.

Leo hii, SHOFCO imesambaa katika maeneo 90 nchini Kenya, ikiwafikia watu zaidi ya milioni 4 kwa huduma kama elimu, maji safi, matibabu dhidi ya utapiamlo, na mikopo kwa familia masikini zaidi.

“Uongozi haupaswi kuwa maslahi  ya wachache waliozaliwa na madaraka. Ni haki ya yeyote aliye tayari kutumikia na kujiangalia ndani,” ameongeza Odede.

Kennedy Odede akiwa na watoto wa shule huko Kibera Kenya.
© SHOFCO/Kennedy Odede
Kennedy Odede akiwa na watoto wa shule huko Kibera Kenya.

Amesema tuzo hii haimaanishi mwisho wa safari bali ni msukumo mpya wa kuendeleza ujenzi wa jamii zenye heshima, usawa, na matumaini. Amesisitiza kuwa mabadiliko halisi huanzia kwa wale waliokumbana na changamoto, na wao ndio wanaopaswa kuongoza njia ya mbele.

“Hatungojei ruhusa kuwa sehemu ya mustakabali. Tunaunda huo mustakabali kwa vitendo,” amesema kwa msisitizo.

“SHOFCO ilianza kwenye njia ya vumbi Kibera, mpira mmoja, vijana wachache, na msimamo wa pamoja wa kutokubali kudhalilishwa,” amesema.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha siku ya kimataifa ya mandela 2009
UN
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha siku ya kimataifa ya mandela 2009

Katika hotuba yake, Odede amewahimiza viongozi na mashirika duniani kuamini uongozi wa mashinani, unaochipuka kutoka kwa wale walioguswa moja kwa moja na matatizo ya jamii.

“Tunaendelea kutembea barabara ndefu ya uhuru — si kwa hofu, bali kwa matumaini. Na kama Mandela alivyosema, sisi ni mabaharia wa nafsi zetu,” amehitimisha kwa sauti ya matumaini.