Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Türk ataka hatua za haraka kuhakikisha ulinzi wa watu Sweida na kote Syria

Wanaume wawili wanaendesha pikipiki kwenye barabara ya Saraqab, Idleb, Syria, ambapo kuna jengo limeharibiwa sana na rundo kubwa la magofu nyuma.
© UNOCHA/Ali Haj Suleiman Syria inapata ahueni baada ya miaka mingi ya migogoro na utawala wa kidikteta.

Türk ataka hatua za haraka kuhakikisha ulinzi wa watu Sweida na kote Syria

Haki za binadamu

Mamlaka za mpito za Syria lazima zihakikishe uwajibikaji na haki kwa mauaji na ukiukwaji mwingine mkubwa wa haki za binadamu uliofanyika katika mji wa kusini wa Sweida, amesema Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, leo jijini Geneva, Uswisi, akirudia wito wake wa kuijenga Syria mpya inayowahudumia watu wote kwa usawa, heshima, na bila ubaguzi.

Ripoti za kuaminika zilizopokelewa na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, zinaonesha kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa haki, ikiwa ni pamoja na mauaji ya haraka bila mchakato wa kisheria, utekaji nyara, uharibifu wa mali binafsi, na uporaji wa nyumba. Miongoni mwa waliotajwa kuwa wahusika ni wanachama wa vikosi vya usalama na watu wanaohusishwa na mamlaka za mpito, pamoja na makundi mengine yenye silaha kutoka eneo hilo, ikiwa ni pamoja na Druze na Wabedui. Hali hii imesababisha maelfu ya watu kukimbia katika jimbo hilo linalokaliwa na watu wa jamii ya Druze.

“Umwagaji damu huu na vurugu lazima vikome, na ulinzi wa watu wote uwe kipaumbele cha juu, kwa mujibu wa sheria za kimataifa za haki za binadamu,” amesema Türk. “Lazima pawepo na uchunguzi huru, wa haraka na wazi kuhusu ukiukwaji wote, na waliohusika wawajibishwe, kwa mujibu wa viwango vya kimataifa. Kuchochea vurugu na hotuba za chuki, iwe mtandaoni au nje ya mtandao, lazima vikomeshwe.”

“Ni muhimu kuchukua hatua za haraka kuzuia kurejea kwa vurugu hizi. Kulipiza kisasi siyo suluhisho.” Amesisitiza.

Katika tukio moja mnamo 15 Julai, OHCHR ilithibitisha kuuawa kiharamu kwa watu wasiopungua 13, baada ya watu wenye silaha wanaohusiana na mamlaka za mpito kufyatua risasi kwa makusudi kwenye mkusanyiko wa kifamilia. Katika siku hiyo hiyo, waliwaua kwa haraka wanaume sita karibu na makazi yao katika matukio mawili tofauti. Aidha, ofisi hiyo ilibaini tukio la kumdhalilisha hadharani mwanaume wa jamii ya Druze, ikiwemo kunyolewa lazima masharubu yake, ishara muhimu ya kitamaduni kwa jamii ya Druze.

Kwa ujumla, mamia ya watu wanaripotiwa kuuawa tangu 12 Julai.

“Ofisi yangu imepokea simulizi kutoka kwa Wasyria walioko katika hofu kubwa kwa ajili ya maisha yao na ya wapendwa wao,” amesema Kamishna Mkuu na kuongeza kuwa, “uwepo wa vikosi vya usalama vya serikali unapaswa kuleta usalama na ulinzi, si kuongeza hofu na vurugu.”

Pia ameelezea wasiwasi juu ya vifo vya raia vinavyotokana na mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Sweida, Daraa, na katikati mwa Damascus. “Mashambulizi kama lile la Damascus Jumatano yanahatarisha maisha ya raia na mali zao. Mashambulizi haya lazima yakome.” Amesema.

Wito

Türk ametoa wito wa kufanyika kwa mchakato huru, wa haraka na wa kina wa kuchunguza watu wote waliotekeleza ukiukwaji wa haki, kuhakikisha hawapewi nafasi katika vyombo vya usalama au kijeshi vya serikali ya Syria. “Hii ni hatua muhimu katika kujenga upya imani ya umma na kusukuma mbele mchakato mpana wa mpito nchini Syria,” ameeleza Kamishna Turk.

Pia amezitaka mamlaka za mpito kuchapisha matokeo ya uchunguzi uliofanywa na kamati ya kitaifa kuhusu vurugu zilizotokea katika maeneo ya pwani mapema mwaka huu.

“Uchunguzi usioegemea upande wowote kuhusu vurugu za karibuni pia utasaidia kuimarisha mchakato wa haki ya mpito ili kuhakikisha uwajibikaji kwa ukiukwaji uliopita,” aliongeza Kamishna Mkuu. “Wasyria wanastahili ukweli, uwajibikaji, na uhakikisho kuwa ukiukwaji wa namna hiyo hautarudiwa.”

Kamishna Mkuu Turk amesema pamoja na kuanguka kwa serikali ya zamani, “Wasyria wameona tumaini la wakati wa mabadiliko kuelekea maisha bora yanayozingatia haki za binadamu. Ni jukumu la mamlaka za mpito kuhakikisha kuwa sura hii mpya inaongozwa na haki, usawa, na ulinzi wa wote.”