Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 11 wanakosa misaada baada ya wahisani kupunguza ufadhili – UNHCR

Mwanamke aliyevaa kitambaa cha rangi ya chungwa amembeba mtoto mdogo mgongoni katika mkusanyiko wa watu waliokimbia makazi yao huko Renk, Sudan Kusini.
© UNHCR/Reason Moses Runyanga Familia zawasili katika kituo cha usafiri huko Renk, Sudan Kusini, baada ya kukimbia ghasia zinazozidi kuongezeka nchini Sudan.

Watu milioni 11 wanakosa misaada baada ya wahisani kupunguza ufadhili – UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limeonya leo kuwa takribani watu milioni 11.6, wakiwemo wakimbizi na waliolazimika kuhama makazi yao, mwaka huu wako katika hatari ya kukosa misaada ya kuokoa maisha poteza msaada wa kuokoa maisha kutokana na upungufu mkubwa wa ufadhili.

Idadi hiyo ni sawa na theluthi moja ya watu waliopokea msaada kutoka UNHCR mwaka 2024.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Nje wa UNHCR, Dominique Hyde, ameelezea hali hiyo kuwa ni “muunganiko hatari wa ongezeko la watu waliotawanywa, upungufu wa ufadhili, na kutojali kwa viongozi wa kisiasa.”

“Wanawake na watoto, kama kawaida, ndio wanaoathirika zaidi,” amesema Hyde.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya UNHCR, dola bilioni 1.4 za Marekani za programu muhimu zimekatwa au kusitishwa mwaka huu.

Athari zake ni mbaya: kuzorota kwa hali za maisha, kuongezeka kwa hatari ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia, na tishio kubwa la kutawanywa kwa mara nyingine kwa mamilioni ya watu.

Huduma muhimu zakumbwa na pigo dunia nzima

Katika nchi kama Chad na Sudan Kusini, uhaba wa fedha umeilazimu UNHCR kusitisha uhamishaji wa wakimbizi kutoka maeneo ya mipakani kwenda maeneo salama, na kuwaacha maelfu wakiwa wamekwama katika maeneo ya mbali na hatarishi. Nchini Uganda, utapiamlo unazidi kuongezeka katika vituo vya mapokezi kutokana na uhaba wa chakula na maji safi.

Nchini Bangladesh, elimu ya watoto warohingya wapatao 230,000 iko hatarini, huku mpango mzima wa afya wa UNHCR nchini Lebanon ukikabiliwa na uwezekano wa kufungwa ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Kwa ujumla, msaada wa kifedha na bidhaa za dharura umepunguzwa kwa asilimia 60, na mipango ya makazi imepungua kwa kiwango kikubwa.

Nchini Niger, familia zimebanwa kuishi katika maeneo yaliyojaa watu au ziko katika hatari ya kukosa makazi kabisa. Familia za Waukraine waliokimbia vita sasa zinashindwa kumudu mahitaji ya msingi kama chakula, kodi ya nyumba, au matibabu.

“Nyuma ya takwimu hizi kuna maisha halisi yanayoning’inia katika hali ya kutoweka,” amesema Hyde. “Familia zinalazimika kuchagua kati ya kuwalisha watoto wao, kununua dawa au kulipa kodi.”

Huduma za ulinzi na msaada wa kisheria zazorota

Huduma muhimu kama vile ulinzi wa watoto, ushauri wa kisheria, na kinga dhidi ya ukatili wa kijinsia zimeathirika vibaya kwa kiasi kikubwa.

Nchini Sudan Kusini, asilimia 75 ya maeneo salama kwa wanawake na wasichana yanayosaidiwa na UNHCR yamefungwa, na kuwaacha hadi wasichana na wanawake 80,000, wakiwemo waathirika wa ukatili wa kingono, bila msaada wa kimatibabu, kisaikolojia, kisheria, au njia za kujipatia kipato.

Mipango ya kuhamishia wakimbizi makazi mapya na kurejea nyumbani kwa hiari kwa usalama pia imekwama.

Licha ya karibu waafghani milioni 1.9 kurejea au kulazimika kurejea nyumbani tangu Januari, msaada wa kifedha kwao ni mdogo mno — mara nyingi hauwezi hata kufanikisha ununuzi wa chakula.

UNHCR yaomba ufadhili wa dharura

Mahitaji ya kifedha ya UNHCR kwa mwaka 2025 yamefikia dola bilioni 10.6, lakini hadi kufikia katikati ya mwaka huu, ni asilimia 23 pekee ya kiasi hicho kilichopatikana.

Licha ya changamoto hizi, Hyde amesisitiza kuwa UNHCR inaelekeza rasilimali zake chache katika shughuli za kuokoa maisha, na iko tayari kuongeza msaada haraka endapo ufadhili zaidi utapatikana.

“UNHCR ina mifumo, ushirikiano na utaalamu wa kuchukua hatua — lakini tunahitaji msaada,” amesema.

Shirika hilo limeonesha shukrani za dhati kwa wafadhili waliodumu kusaidia wakati huu mgumu, na linatoa wito wa dharura kwa serikali, taasisi, na watu binafsi kuongeza juhudi za kuziba pengo la ufadhili na kuzuia mateso zaidi.