Mgawanyiko wa Cyprus: Katibu Mkuu UN ahimiza majadiliano kuendelea kwa ajili ya amani
Mgawanyiko wa Cyprus: Katibu Mkuu UN ahimiza majadiliano kuendelea kwa ajili ya amani
Amani na Usalama
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amepongeza mazungumzo “yenye kujenga” kati ya viongozi wa Wacyprus Wagiriki na Wacyprus Waturuki baada ya mkutano wa ngazi ya juu uliofanyika leo Julai 17 katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kwa lengo la kuendeleza juhudi za kuleta amani na kuaminiana katika kisiwa kilichogawanyika cha Cyprus.
Mkutano huo, uliopendekezwa na Katibu Mkuu mwezi Machi mwaka huu, umewaleta pamoja Kiongozi wa Wasyprus Wagiriki, Nicos Christodoulides, na Kiongozi wa Wacyprus Waturuki, Ersin Tatar, pamoja na wawakilishi kutoka kwa nchi tatu wadhamini: Ugiriki, Türkiye na Uingereza.
“Ninashukuru kwa ushiriki wa viongozi na Mawaziri wa Mambo ya Nje wanaowakilisha nchi wadhamini wa Cyprus,” amesema Guterres kwa waandishi wa habari. “Tangu mwanzo wa kipindi changu cha uongozi, nimejitoa kwa usalama na ustawi wa Wacypriot wote Wagiriki Wacypriot na Waturuki Wacypriot.”
Katibu Mkuu alieleza mafanikio ya wazi yaliyopatikana kupitia mipango sita ya kujenga imani iliyokubaliwa mwezi Machi. Kati ya hiyo, minne imekamilika:
- Kuanzishwa kwa kamati ya kiufundi kuhusu vijana;
- Ushirikiano wa kimazingira na mabadiliko ya tabianchi, hasa athari za maeneo ya migodi;
- Ukarabati wa makaburi; na
- Makubaliano kuhusu kuondoa mabomu ya ardhini ambayo yapo katika hatua ya mwisho ya maelezo ya kiufundi.
Majadiliano yanaendelea kuhusu mipango miwili iliyosalia:
- Ufunguzi wa vituo vinne vipya vya kuvukia mipaka; na
- Mradi wa nishati ya jua katika eneo la mpakani.
Zaidi ya hayo, viongozi hao wamefikia makubaliano ya pamoja juu ya maeneo mapya ya ushirikiano, yakiwemo:
- Kuanzishwa kwa chombo cha ushauri cha kushirikisha jamii ya kiraia;
- Kubadilishana mali za kitamaduni;
- Mpango wa kufuatilia hali ya hewa na ubora wa hewa; na
- Kukabiliana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na plastiki ndogondogo.
“Mipango hii siyo ishara tu za kisiasa bali ni hatua halisi zinazoweza kuwa na athari kubwa na chanya kwa maisha ya watu kote visiwani,” amesema Guterres.
Tutakutana tena
Pia ametangaza kuwa atakutana tena na viongozi hao wawili wakati wa wiki ya ngazi ya juu ya Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba, na pia kutakuwa na mkutano mwingine wa kawaida wa aina hii baadaye mwaka huu.
“Kuna safari ndefu mbele yetu,” Guterres ameongeza. “Lakini hatua hizi zinaonesha dhamira ya kuendeleza mazungumzo kuhusu njia ya kusonga mbele na kufanya kazi kwa mipango itakayowanufaisha Wacypriot wote.”
Umoja wa Mataifa umekuwa ukiunga mkono juhudi za kuunganisha tena Cyprus, ambayo imegawanyika tangu mwaka 1974. Ingawa juhudi za awali za amani zilikwama, mpango mpya wa Katibu Mkuu unaashiria mwamko mpya wa maendeleo unaotegemea ushirikiano wa vitendo na vipaumbele vya pamoja.