Mapenzi ya Mwalimu Nyerere kwa lugha Kiswahili na kilimo kutumika kusongesha SDGs Afrika Mashariki
Mapenzi ya Mwalimu Nyerere kwa lugha Kiswahili na kilimo kutumika kusongesha SDGs Afrika Mashariki
Amani, Ukuaji wa Uchumi, Kutokomeza njaa na umaskini ni baadhi ya Malengo 17 ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu, SDGs ambapo nchi kote duniani kwa kushirikiana na wadau kutoka kila nyanja wanapambana kuyafikia ifikikapo mwaka 2025.
Taasisi ya Afrika Mashariki Fest ya nchini Uganda kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania na Uganda inatumia kampeni yake ya Twende Zetu Butiama ili kuyatumimiza malengo hayo. Kwao wao, maono ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndio njia nzuri kwani wanalenga kutumia lugha ya Kiswahili kuunganisha watu, na pia kilimo kupambana na njaa na umaskini.
“Vijana shikeni bango la lugha ya Kiswahili na muwe na moyo wa kuipenda Afrika. Hamna atakayetoka nje kuja kuipenda Afrika,” anasema Balozi wa Tanzania nchini Uganda Paul Simuli Kisesa alipokuwa akizungumza na John Kibego wa Kazi Njema FM baada ya uzinduzi wa mandalizi ya safari ya hija ya ‘Twende Zetu Butiama’ inayolenga kutumia maono ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Julius Kambarage Nyerere ili kuleta amani na umoja, kukuza lugha ya Kiswahili na kukuza uchumi kupitia kilimo.
Balozi Simuli anaongeza kuwa vijana ni wadau muhimu katika kutimiza ndoto alizokuwa nazo hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“Vijana wote na hasa wale wanahabari wanapaswa kuwa na vipindi virefu hewani kama njia ya kukuza lugha ya Kiswhaili,” anahimiza.
Safari ya pili ya hija ya ‘Twende Zetu Butiama’ imepangwa tarehe 26 hadi 30 Septemba mwaka huu wa 2025.
Ni safari inayolenga zaidi kutembelea sehemu alikozaliwa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye ananziwa kwa kuchagiza Jumuiya ya Afrika Mashariki na hasa matumizi ya lugha ya Kiswahili ambayo sasa inatambuliwa kimataifa kupitia shirika la Umoja wa Mataifa la Eimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO.
Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia
Profesa Bernard Mellau Lesakit Sipira, Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Tekinolojia cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere cha Butiama nchini Tanzania anasema, chuo kikuu hicho ni muhimu katika kumbukumbu za Mwalimu Nyerere.
“Chuo Kikuu hiki kilianzishwa na serikali ya Tanzania kama njia ya kuendeleza ndoto za Mwalimu Nyerere. Kimejengwa kwenye ardhi ambapo Mwalimu Nyerere alikuwa na shamba lake,” asema.
Mwalimu Nyerere alitambua kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa Watanzania walio wengi na hivyo lazima likumbatiwe, anongeza Profesa Mellau.
Profesa Mellau anaendelea kueleza akisema, “tunaamini kitasaida pia kukabiliana na changamoto ya uhaba wa ajira ambapo walimu watakuwa wakitoka na ujuzi wa kujiajiri na kwajiri wengine.”
Balozi wa Kenya nchini Uganda, Joash Maangi amesema ‘Twende zetu Butiama’ ni safari ya aina yake na “ni mbali zaidi na safari za kawaida. Ni ziara ya kujitolea kwa pamoja kupitia tamaduni zetu zinazofanana. Mafanikio ya safari ya kwanza ni thibithisho la nguvu za mila zetu na historia inayofanana na kuwaleta pamoja watu wa vizazi tofauti kutoka nchi tofauti.”
Safari ya kwanza mwaka jana ilivutia watu kutoka nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Msumbiji Siera leone, Ghana na Zimbabwe.
Mwaka huu wengi zaidi wanatarajiwa.
Daktari Ronex Kisembo Tendo ni Mkurugenzi wa Afrika Maskariki Fest, shirika la linaloongoza mandalizi ya safari ya hija ya ‘Twende Zetu Butiama’, anasema safari hii itajumuisha matembezi kwenye sehemu mbalimbali.
“Tutakuwa na mahojiano na wanakijiji alikozaliwa hayati Mwalimu Nyerere, tutaembelea mbuga ya wanyama ya Serengeti, chuo kikuu cha kilimo na tekinolojia cha Mwalimu Julius Nyerere cha Butiama na mengine mengi,” asema Dkt. Kisembo.
Jenerali Henry Isoke, Mkuu wa kitengo cha kupambana na ufisadi katika Ikulu ya Uganda, amesema serikali inakaribisha juhudi za kukuza utaangamano na lugha ya Kiswhaili.
“Lugha ya Kiswhaili nimuhimu sana kwentu,” anasema Jenerali Isoke.
Safari hii ya hija inafanyika ikiwa ni miaka 26 baada ya kuanza upya kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na vilevile kifo cha Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.