Fletcher: Msaada lazima uende mahali ambapo mahitaji ni makubwa zaidi huko Gaza
Fletcher: Msaada lazima uende mahali ambapo mahitaji ni makubwa zaidi huko Gaza
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limekutana hii leo jijini New York Marekani katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kujadili kuongezeka kwa mzozo wa kibinadamu huko Gaza, ambako amri mpya za kuwataka watu kuhama katika makazi yao zinazotolewa na jeshi la Israel zimewaondoa makumi kwa maelfu ya watu walati huo huo mashambulizi ya mabomu yakendelea kukatisha uhai wa watu wakiwemo watoto.
Akizungumza na wajumbe wa baraza hilo Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA, Tom Fletcher, amesema “Chakula kinaisha na wale wanaoenda kusaka msaada wa chakula wapo hatarini kupigwa risasi. Watu wanakufa wakijaribu kuwapatia mlo familia zao.”
Fletcher amesema hospitali zilizoko Gaza zimekuwa kizipokea maiti na watoa huduma za afya wamekuwa wakisimuliwa na waliojeruhiwa kila siku.
Akielezea kinaga ubaga madhila yanayowakumba wakazi wa Gaza ambalo ni eneo la wapalestina linalokaliwa kimabavu na Israel Mkuu huyo wa UN amesema viwango vya utapiamlo miongoni mwa watoto vimepanda mara dufu mwezi wa Juni 2025 na kwamba ni hospitali 17 kati ya 36 na Zahanati 63 kati ya 170 ndio zinazofanya kazi na tena kwa kiasi Fulani ilihali iadadi kubwa ya majeruhi wanawasili kila siku.
“Katika baadhi ya hospitali, watoto watano wanatumia mashine moja ya kuwasaidia kupata joto. Asilimia 70 ya dawa muhimu zinazohitajika zimeisha.”
Dunia imewaangusha watoto walio katika mzozo wa Gaza- Israel
Wastani wa watoto 28 wanauawa kila siku- sawa na darasa zima ... kwa karibu miaka miwili
Akigongelea msumari madhila yanayowakumba watoto, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF Catherine Russelle amesema “Katika kipindi cha miezi 21 iliyopita ya vita, zaidi ya watoto 17,000 wameripotiwa kuuawa na 33,000 wamejeruhiwa. Wastani wa watoto 28 wameuawa kila siku - sawa na darasa zima. Fikiria hilo kwa muda. Darasa zima la watoto huuawa kila siku kwa karibu miaka miwili.”
Mkuu huyo wa UNICEF ameeleza jinsi watoto wanavyouawa na kupewa ulemavu wakati wakiwa wamepanga foleni kwa ajili ya kusaka chakula na dawa za kuokoa maisha. Akitolea mfano watoto tisa na wanawake wanne waliokutwa na madhila hayo wiki iliyopita huko Deir al Balah.
Amesema kati ya tarehe 27 mwezi Mei na Julai 7Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilirekodi mauaji ya raia 798 wa Palestina ikiwa ni pamoja na watoto waliokuwa na wanahangaika kupata chakula, wakiwa karibu au wakiwa kwenye maeneo ya usambazaji wa chakula na kwenye misafara ya kutoa misaada ya kibinadamu.
“Tunahitaji haraka kurejea kwenye utoaji wa misaada unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa huku kukiwa na usalama na misaada ya kibinadamu ikiruhusiwa kuingia kupitia katika mipaka yote iliyopo.”