Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Amri mpya za kuhama zahatarisha afya ya wanaohitaji huduma za kusafisha damu

Mvulana mdogo wa Kipalestina ameketi bila viatu kwenye kifusi katika eneo lililoharibiwa la Gaza.
© UNICEF/Mohammed Nateel Kijana mmoja ameketi kwenye vifusi vya nyumba huko Gaza. Huduma za kimsingi ikiwa ni pamoja na huduma za afya na maji safi zinazidi kuwa ngumu kutoa, amesema msaada wa UN

Gaza: Amri mpya za kuhama zahatarisha afya ya wanaohitaji huduma za kusafisha damu

Wahamiaji na Wakimbizi

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yameonya kuwa amri mpya za kuhama huko Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli,   zilizotolewa na jeshi la Israel zimewalazimisha makumi ya maelfu ya wapalestina kuhama, huku mashambulizi yakiendelea.

Wale walioathiriwa na amri hizo wameambiwa wahamie katika ukanda wa pwani wa Al Mawasi ambao tayari umejaa watu kupita kiasi, imesema Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA).

Al Mawasi, mji ulio karibu na Khan Younis, hauna “mahitaji ya msingi ya kuishi,” imesisitiza OCHA.

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, eneo hilo pia ni karibu na kulikofanyika mashambulizi 24 dhidi ya wapalestina waliopoteza makazi na waliojihifadhi kwenye mahema hapo kati ya Machi 18 na Aprili 11,

Kadri vita vinavyoendelea kuingia mwezi wa 21, watu walio hatarini zaidi Gaza wanaendelea kupambana kuendelea kuishi.

Dharura kwa wanaosafisha damu

Tweet URL

Miongoni mwao ni Musbah Zaqqout, mwenye umri wa miaka 70, mmoja wa wagonjwa 230 wanaopokea matibabu ya kuokoa maisha ya kusafisha damu katika Hospitali ya Al-Shifa, jijini Gaza. 

Matibabu yake yamevurugwa na uhaba mkubwa wa vifaa, hali iliyosababisha kupunguzwa kwa idadi ya vipindi vya huduma hiyo kutoka vitatu hadi viwili kwa wiki, mwishoni mwa mwezi uliopita, limeonya shirika la Umoja wa Matiafa la Afya duniani, WHO.

"Aliteseka sana huduma hiyo ilipopungua," amesema Saadia, mke wa Bwana Zaqqout. "Alikuwa anashindwa kupumua, mara nyingi alikuwa analazwa hospitalini, hadi akapoteza fahamuna hakumtambua mtu yeyote."

Vifaa vya matibabu kutoka Kituo cha Misaada ya Kiutu cha Mfalme Salman na usaidizi kutoka WHO vimerejesha huduma hiyo katika hospitali ya Al-Shifa.

"Shukrani kwa Mungu, baada ya kuanza tena dialysis, hali yake iliboreka," amesema Bi. Zaqqout, huku WHO ikisisitiza wito wake wa kuingiza chakula, mafuta na misaada ya afya kwa kiwango kikubwa kupitia njia zote zinazowezekana.

"Upungufu mkubwa wa mafuta na vifaa vya tiba unaendelea kote Gaza," WHO imeonya. "Bila kujazwa kwa haraka na kwa kudumu, huduma za afya ziko hatarini kusimama kabisa."

Mtoto Mpalestina mwenye utapiamlo amefunikwa blanketi katika kliniki ya afya ya UNRWA huko Gaza.
© UNRWA/Hussein Owda Salam, mtoto mwenye umri wa miezi sita, anachunguzwa utapiamlo katika kituo cha matibabu cha UNRWA katika Jiji la Gaza.

Janga la utapiamlo kwa watoto

Kwa kuunga mkono hoja hizo, shirika la UN la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA limeonya leo Jumatano kwamba inazidi kuwa vigumu kuwasaidia wapalestina wa Gaza.

Tayari mtoto 1kati ya kila watoto 10 wanaopelekwa katika kliniki za UNRWA anasumbuliwa na utapiamlo. Hali hiyo haikuwahi kushuhudiwa kabla ya vita, lakini imeongezeka maradufu kwa watoto walio chini ya miaka mitano kati ya Machi na Juni, kufuatia mzingiro mkali wa Israel.

"Inazidi kuwa vigumu kwetu kuendelea kutoa huduma," amesema Louise Wateridge Afisa wa UNRWA. "Angalau vituo 188 vya UNRWA – zaidi ya nusu ya vituo vyote katika Ukanda wa Gaza – viko ndani ya maeneo ya kijeshi ya Israel, chini ya amri za uhamishaji, au katika maeneo ambapo hayo yanakutana."

Katika taarifa ya hivi karibuni, Bi. Wateridge alisema kwamba ni vituo sita tu vya afya vya UNRWA na vituo 22 vya tiba vya shirika hilo bado vinafanya kazi leo, pamoja na vituo 22 vya tiba vinavyotembea ndani na nje ya makazi ya wakimbizi.

Kwa sasa, karibu asilimia 60 ya vifaa vya msingi vya tiba vimeisha, kwa mujibu wa UNRWA. "Watoto wanakufa mbele ya macho yetu, kwa sababu hatuna dawa wala chakula cha kutosha cha kuwatibu,"

Dawa muhimu zimekwisha

Kama matokeo ya moja kwa moja ya mzingiro wa Israel huko Gaza ulioanza Machi 2, UNRWA imesema kwamba sasa imeishiwa dawa za shinikizo la damu, dawa za minyoo na fangasi, dawa za macho na za kuvimba, dawa zote za ngozi na antibiotiki za kumeza kwa watu wazima.

Kupatia maji safi kwa wakazi wa Gaza waliokatiwa huduma hiyo kutokana na vita bado ni changamoto kubwa, ambapo ni visima viwili tu vikuu vya UNRWA vinavyofanya kazi kwa sasa. Kabla ya vita, kulikuwa na visima vikuu 10. Visima vingine vidogo 41 vinaendelea kutumika katika makazi ya wakimbizi ya UNRWA.

Kwa miezi miwili iliyopita katika kaskazini mwa Gaza, UNRWA imelazimika kusitisha huduma za maji na usafi kwa watu wapatao 25,000 waliopoteza makazi katika vituo vya hifadhi, kutokana na amri za uhamishaji zilizotolewa na jeshi la Israel.

"Kizuizi cha kuingiza mafuta kinaendelea kuhatarisha sana huduma za kuokoa maisha," shirika hilo limesema. "Huduma muhimu za maji ziko hatarini kusitishwa kabisa ikiwa mafuta hayataruhusiwa kuingia."