Sudan: Mashambulizi Kordofan Kaskazini, watoto 35 miongoni mwa waliouawa
Sudan: Mashambulizi Kordofan Kaskazini, watoto 35 miongoni mwa waliouawa
Takribani watoto 35 wameripotiwa kuwa miongoni mwa raia zaidi ya 450 waliouawa katika msururu wa mashambulizi ya kikatili kwenye jamii zilizo karibu na jiji la Bara katika Jimbo la Kordofan Kaskazini, Sudan, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell jana Julai 15.
Mashambulizi hayo yaliyotokea mwishoni mwa wiki katika vijiji vya Shag Alnom na Hilat Hamid pia yamesababisha majeruhi kadhaa huku wengine wengi wakiendelea kupotea. UNICEF ina hofu kuwa idadi ya watoto waliouawa huenda ikaongezeka kadri taarifa zaidi zinavyokusanywa.
“Mashambulizi haya ni ya kusikitisha na ya kuchukiza,” anasema Russell na kuongeza kuwa “ni ongezeko la kutisha la vurugu na dhihirisho la kutojali kabisa maisha ya binadamu, sheria ya kimataifa ya kibinadamu, na misingi ya utu wa kibinadamu.”
Miongoni mwa waliouawa ni wavulana 24, wasichana 11, pamoja na wanawake wawili wajawazito. Mashambulizi haya yanajiri wakati hali ya kibinadamu nchini Sudan inazidi kuzorota huku raia wakiendelea kuwa waathirika wakuu wa mzozo unaoendelea.
UNICEF imelaani vikali mashambulizi hayo na kutoa wito kwa pande zote zinazohusika kusitisha mapigano mara moja na kuheshimu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa, hasa kuhusu ulinzi wa raia.
Wito
“Uvunjaji wowote wa sheria unapaswa kuchunguzwa kwa kina na kwa uhuru, na wahusika wawajibishwe ipasavyo,” ameongeza Russell. “Kutokuchukuliwa hatua kwa ukiukaji wa sheria za kimataifa hakuwezi kuvumiliwa hasa pale maisha ya watoto yanapohusika.”
Katika hitimisho, kiongozi huyo wa UNICEF amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka kuwalinda watoto na kuhakikisha haki inapatikana: “Hakuna mtoto anayepaswa kupitia madhila kama haya. Vurugu dhidi ya watoto hazikubaliki na lazima zikome sasa.”