Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Aona matunda ya kumsindikiza mkewe mjamzito kliniki

Mwanamume mwenye tabasamu aliyevaa shati jeupe amemshika mtoto mchanga aliyefunikwa kwa blanketi lenye rangi nyingi, amesimama mlangoni.
UN News Mkazi wa wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, aliyevunja desturi ya wanaume na kuambatana na mkewe kuhudhuria kliniki ya mtoto.

Aona matunda ya kumsindikiza mkewe mjamzito kliniki

Afya

Vifo vya wajawazito vimekuwa wimbo usiokoma kusikika kwenye masikio ya binadamu hususan nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara. Moja ya sababu ni wajawazito kutohudhuria kliniki, na zaidi ni pale wenza wao wanapokuwa hawaambatani nao.

Umoja wa Mataifa unasema kuambatana na mwenza kunaweza kupunguza idadi ya vifo vinavyoweza kujitokeza.Japhet Mbogo, mkazi wa wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, alivunja desturi ya wanaume kwa kuambatana na mkewe Lucy Stephano.

Sasa wamefanikiwa kupata mtoto na Japhet anasema, “ni ile dhana potofu tu kwamba mwanaume hawezi kwenda kliniki. Anayekwenda kliniki ni mwanamke. Lakini kumbe unapokwenda na mke wako kliniki unafundishwa mambo mengi ambayo wewe mwenyewe yana yanakusaidia katika maisha yako pale nyumbani wewe na yeye.”

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya, uzazi, (UNFPA) za mwezi Aprili 2025, wanawake 712  hufariki dunia kila siku wakati wa ujauzito ama kujifungua ikiwa ni sawa na kusema kila baada ya dakika mbili mjamzito mmoja hupoteza maisha.

Faida za baba na mama kwenda kliniki

Ili kupunguza hali hiyo wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza wajawazito kwenda kliniki na wenza wao. Gregory Dismas, Muuguzi Msaidizi anasema, “ni muhimu kwa wote wawili kuhudhuria kliniki hasa mama na baba. Kwanza huwa tunatoa elimu ya afya hasa kwa upande wa mama ambayo elimu hiyo inahusisha hasa dalili za hatari kwa mama mjamzito. Pia kwa upande wa baba humsaidia baba kupata uelewa zaidi juu ya majukumu yaliyo mbele yake.”

Je Lucy mwenyewe anasemaje? “nilimshauri mume wangu kwamba twende kituo cha afya kwa sababu ni utaratibu ambao kwamba tunakuwa  na wenzi wetu. Nilifurahi, naye pia alifurahi na hakushtuka kwa sababu sio mara yake ya kwanza. Kila nikiwa na ujauzito tunaambatana naye. Najisikia mtu wa amani kabisa, yani nilijawa na bubujiko la furaha kabisa kwa sababu ni wachache ambao hutembea na wenza wao wakiwa wanaelekea hospitali.”

Utamaduni wa wanaume kuwapeleka wake zao kliniki bado ni changamoto kutokana na imani potofu zilizopo katika jamii, lakini elimu waliyoipata kupitia Shirika lisilo la kiserikali la Amani Girls lililopo mjini Mwanza, kaskazini magharibi mwa Tanzania, ilitosha kuzifuta fikra hizo.

Mwanamume Mtanzania ameketi kwenye kiti cha bluu karibu na mwanamke anayemnyonyesha mtoto wake katika kliniki ya nje huko Sengerema, Tanzania.
UN News Mkazi wa wilaya ya Sengerema akiwa na Mkewe mkoani Mwanza Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, Mwanaume aliyevunja desturi ya wanaume na kuambatana na mkewe kuhudhuria kliniki ya mtoto.

Waliniona ‘mke wangu ananitawala’

Alipoulizwa kauli za kejeli alizokuwa anapata akimsindikiza mkewe kliniki, Japhet anasema,“walikuwa wananicheka sana na kuniona mjinga kwamba mke wangu kanitawala. Ile ni dhana ya ujinga kwamba mwanamke siku zote huwa yuko chini ya mwanaume wakati ni jambo la kawaida katika maisha tuliyonayo sasa hivi.”

Bwana Dismas ambaye ni Muuguzi Msaidizi katika Zahanati ya Nyamatongo anatamatisha kuwa kuambatana pamoja kutawezesha pia kufahamu hali za afya yao, iwapo wana maambukizi ya magonjwa au la.”Pia  tunatoa elimu. Baba lazima aelewe dalili za hatari pia kwa mama ambazo kama atapata dalili za afya anaanza kuona hizo dalili hatari mzazi atakuwa na uelewa na kuchukua hatua mapema.”