Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 875 wamethibitishwa kufariki wakijaribu kusaka mlo Ukanda wa Gaza

Noha Hassouna, mama Mpalestina, ameketi kwenye kiti cha hospitali katika Jiji la Gaza, akiwabeba wanawe wawili wadogo waliojeruhiwa katika shambulio kwenye makazi ya Shule ya Dar Al-Arqam.
© UNICEF/Mohammed Nateel Viwango vya utapiamlo vinaongezeka huko Gaza.

Watu 875 wamethibitishwa kufariki wakijaribu kusaka mlo Ukanda wa Gaza

Amani na Usalama

Takribani Wapalestina 900 waliokuwa na njaa na kukata tamaa wameuawa katika wiki za hivi karibuni wakijaribu kutafuta chakula, huku vifo vingi vikiripotiwa katika maeneo binafsi ya misaada yanayoendeshwa na taasisi inayojiita Gaza Humanitarian Foundation (GHF), ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) imeeleza leo Julai 15. 

Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, Thameen Al-Kheetan amewaeleza leo waandishi wa habari Geneva, Uswisi kuwa watu 674 kati yao waliuawa wakiwa kwenye maeneo ya Mfuko wa Kiutu wa Gaza, (GHF) unaoendeshwa na Israeli na Marekani.

“Tarehe 13 Julai, tumerekodi vifo vya watu 875 waliouawa Gaza wakijaribu kupata chakula, kati yao 674 waliuawa karibu na maeneo ya GHF,” amesema Thameen Al-Kheetan.

Watu wengine 201 waliuawa wakijaribu kupata chakula “karibu na misafara ya misaada” inayoendeshwa na Umoja wa Mataifa au mashirika yanayoshirikiana na Umoja wa Mataifa ambayo bado yanafanya kazi katika ukanda huo ulioporomoka kwa vita, Bwana Al-Kheetan amewaambia waandishi wa habari.

Wapalestina waliokimbia makazi yao wakisafirisha mali zao kwenye mkokoteni katika Kambi ya Halawa, Gaza, wakijiandaa kwa ajili ya kuhamishwa.
© UNICEF/Mohammed Nateel Familia zinahamisha mali zao kaskazini mwa Gaza kufuatia amri mpya za kuwalazimisha kuhama.

Mauaji yanayohusishwa na vituo vya misaada vya Marekani na Israel vinavyoungwa mkono na Marekani yalianza muda mfupi baada ya kuanza kufanya kazi kusini mwa Gaza tarehe 27 Mei, na kupita Umoja wa Mataifa na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali.

Tukio la hivi karibuni lililotokea Jumatatu tarehe 14 Julai, majira ya saa tatu asubuhi, lilihusisha jeshi la Israeli kulipua na kufyatua risasi kwa wapalestina waliokuwa wakitafuta chakula katika kituo cha GHF kilicho eneo la As Shakoush, kaskazini-magharibi mwa Rafah.

Kwa mujibu wa OHCHR, wapalestina 2 waliuawa na wengine wasiopungua 9 walijeruhiwa. Baadhi ya waathirika walikimbizwa katika hospitali ya Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) huko Rafah. Jumamosi, madaktari walipokea wagonjwa zaidi ya 130, “idadi kubwa” wakiwa na majeraha ya risasi na “wote waliokuwa hai” waliripoti kuwa walikuwa wakijaribu kufika vituo vya usambazaji wa chakula.

Njaa inayoua

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limeonesha wasiwasi mkubwa juu ya kuendelea kuuawa kwa raia wanaojaribu kupata chakula, huku utapiamlo wa kutisha ukiendelea kuwaathiri watoto.

“Timu zetu – kutoka UNRWA na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa zimezungumza na manusura wa mashambulizi haya, wakiwemo watoto wenye njaa, waliopigwa risasi wakiwa njiani kwenda kuchukua chakula kidogo sana,” amesema Juliette Touma, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa UNRWA.

Akizungumza kwa njia ya video kutoka Amman, Bi. Touma amesisitiza kuwa mzingiro mkali uliowekwa na Israeli dhidi ya Gaza umesababisha vifo vya watoto wachanga kutokana na utapiamlo mkali wa kupindukia.

“Hatujaruhusiwa kuingiza msaada wowote wa kibinadamu Gaza kwa zaidi ya miezi minne sasa,” amesema, kabla ya kuashiria “ongezeko kubwa” la utapiamlo miongoni mwa watoto tangu kuanza kwa mzingiro huo wa Israeli tarehe 2 Machi.

“Tuna malori 6,000 yaliyokwama maeneo kama Misri na Jordan; kutoka Jordan hadi Ukanda wa Gaza ni safari ya saa tatu tu, sivyo?” Bi. Touma ameongeza  

Mbali na chakula, malori hayo ya UN pia yamebeba bidhaa muhimu kama sabuni. “Dawa na chakula vitakaribia kuharibika iwapo hatutafanikiwa kuvipeleka kwa watu wa Gaza wanaovihitaji zaidi – miongoni mwao watoto milioni moja ambao ni nusu ya idadi ya watu wa Gaza,” Bi. Touma ameongeza.

Wakimbizi wanatembea kwenye barabara ya udongo katika Kambi ya Wakimbizi ya Jenin, wakiwa na askari wenye silaha na gari la kivita nyuma.
© UNICEF/Alaa Badarneh Familia zinakimbia makazi yao katika Ukingo wa Magharibi, kutokana na kuongezeka kwa ghasia. (Maktaba)

Ukingo wa Magharibi: ‘Vita ya kimya inazidi kushika kasi’

Wakati huo huo, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu, ikiwemo Yerusalemu Mashariki, wapalestina wanaendelea kuuawa kwenye vurugu zinazodaiwa kusababishwa na walowezi wa kiyahudi na vikosi vya usalama vya Israeli, kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Kulingana na OHCHR, mtoto wa umri miaka miwili Laila Khatib alipigwa risasi kichwani na vikosi vya usalama vya Israeli tarehe 25 Januari akiwa ndani ya nyumba yao katika kijiji cha Ash-Shuhada, mkoa wa Jenin.

Mnamo tarehe 3 Julai, mwanaume mwenye umri wa miaka 61, Walid Badir, alipigwa risasi na kuuawa na vikosi vya Israeli, akiripotiwa kuwa alikuwa akirudi nyumbani kutoka maombi kwa baiskeli, akipitia pembezoni mwa kambi ya wakimbizi ya Nur Shams, OHCHR imeeleza.

Bwana Al-Kheetan ameongeza kuwa mashambulizi, uharibifu wa nyumba na kufurushwa kwa wapalestina vimeongezeka katika wiki za karibuni, huku watu wapatao 30,000 wakilazimika kuhama tangu kuanza kwa operesheni ya kijeshi ya Israeli iitwayo “Iron Wall” kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi mapema mwaka huu.

“Tukumbuke kwamba sheria za kimataifa ziko wazi kuhusu wajibu wa taifa, kubadili muundo wa idadi ya watu katika eneo lililokaliwa kimabavu kunaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita na ni sawa na usafishaji wa kikabila. Vita ya kimya inaendelea kushika kasi, ambapo kuna vikwazo vikali vya harakati, umasikini unaongezeka huku watu wakikosa njia za kujipatia riziki na ukosefu wa ajira ukiongezeka,” amesema Bi. Touma wa UNRWA.

Kwa sasa, operesheni ya kijeshi ya Israeli imejikita katika Ukingo wa Magharibi na kuathiri kambi za wakimbizi za Jenin, Tulkarem, na Nur Shams.

“Inasababisha kuhama kwa idadi kubwa zaidi ya watu wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi tangu mwaka 1967,” Bi. Touma amehitimisha.