Siku ya kimataifa ya vijana na stadi
Siku ya kimataifa ya vijana na stadi
Siku ya Kimataifa ya stadi za Vijana huadhimishwa tarehe 15 mwezi Julai kila mwaka. Mwaka huu 2025, siku hii inaadhimishwa huku ikiwa na kauli mbiu inayosema “Uwezeshaji wa Vijana kupitia akili mnemba na stadi za kidijitali, ikisisitiza jinsi vijana wanavyoweza kutumia teknolojia kuleta mabadiliko chanya na Maendeleo endelevu katika jamii.
Rashid Malekela, kijana mwenye umri wa miaka 26 anayesoma Shahada ya kwanza ya Mawasiliano kwa Umma chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino, Mwanza Kaskazini Magharibi mwa Tanzania,hutumia majukwaa ya kidijitali na akili mnemba katika kutoa elimu ya uelimishaji rika na afya ya uzazi kwa vijana wa Kitanzania.
Nini kilimsukuma Rashid hadi kuwa muelimishaji rika wa kupitia majukwaa ya kidijitali?
“Baada ya kujiunga na chuo kikuu kusoma shahada yangu ya kwanza, ndipo nilipoweza kukutana na kikundi cha Vijana hapa chuoni, ambao ni waelimishaji rika kuhusiana na masuala mbali mbali yanayotuhusu sisi vijana, kwa hivyo hapo ndiyo nikapata msukumo zaidi. Mimi na vijana wenzangu tulijiunga na kuanza kusambaza elimu tuliyoipata kwa njia ya mitandao ya kijamii.”
Vijana walengwa wa elimu hii ni akina nani? Na hupokea maudhui yapi hasa?
Rashid ameeleza kuwa vijana walengwa wa hayo maudhui ni wanafunzi wa vyuo, na elimu wanayoitoa inahusu uelimishaji rika na afya ya uzazi ikihusisha ukatili wa kijinsia, afya ya uzazi na haki, magonjwa ya zinaa na UKIMWI na namna sahihi za kujilinda na namna bora ya usimamizi wa fedha kwa Vijana
Ni aina gani ya mifumo ya maudhui hutumika kuwasilisha elimu hiyo kwa Vijana?
“Maudhui ambayo ninatengeneza yapo katika mifumo mbalimbali hususani ni picha,ambazo zinakuwa picha zinazotoa ujumbe Fulani na mtu anakuwa anaelewa kwamba linatoa ujumbe gani kulingana na jambo mahususi ambalo nimeamua kuchapicha katika chapisho hilo inaweza kuwa masuala ya mimba za mapema kwa vijana, njia za kujikinga na UKIMWI. Pia natumia infografiksi,na njia ambayo mimi naiweza zaidi kuitumia ni njia ya video pamoja na masimulizi,na kuna wakati mimi mwenyewe naigiza nikionesha ushirikishi na uhalisia wa maisha ya Vijana,huu husaidia maana kuna muda mwingine akiona picha pekee asielewe.”
Majukwaa yapi ya kidijitali Rashid huwa anatumia na kwa nini hayo majukwaa?
Rashid ameeleza kuwa hupendelea zaidi kutumia majukwaa ya Tik Tok, Instagram pamoja na Facebook katika kutoa elimu. Ameongeza kwa kueleza kwamba wao kama waelimishaji rika waliwahi kupatiwa mafunzo na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kuoneshwa kwamba baadhi ya mitandao(majukwaa) ndiyo inayoongoza zaidi kuwa na watazamaji wengi Vijana, ambapo iliongozwa na Facebook, Instagram kisha Tik Tok,na hili ndiyo lilipelekea kutumia majukwaa hayo zaidi.
Rashid avuma, kwa Sababu ya utoaji elimu kupitia majukwaa ya kidijitali
Rashid ameeleza kuwa kazi anayoifanya imezaa matunda, kwanza kupitia mrejesho wa maoni ya baadhi ya vijana kwenye mitandao ya kijamii, pili, kupitia fursa mbalimbali ambazo amezipata yeye pamoja na vijana wengine 14 wa vyuo vikuu Tanzania kwa kuchaguliwa kuwa mabalozi wa miradi mbalimbali ya elimu ya afya kwa umma ambayo ni ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na miradi mwingine kama O3Plus, ambao wao ndiyo wapo kwa ajili ya kutoa Elimu kwa vijana. Na pia Rashid na wenzake kutoka Iringa, na mwingine wa chuo cha Makerere, Uganda walipata nafasi ya kushiriki mashindano yanayojulikana kama Safer Campuses na kupata nafasi ya kwenda Harare, Zimbabwe kushiriki mikutano ya UNESCO, yote hii ni matunda ya kutoa Elimu ya uelimishaji rika kupitia majukwaa ya kidijitali.
UNESCO, UNICEF NA UNDP yawa mstari wa mbele kwa Rashid katika kutoa miongozo ya utoaji huo wa Elimu
Kama balozi kijana wa mashirika ya Umoja wa Mataifa ya UNESCO, Shirika la watoto (UNICEF) na lile la Maendeleo (UNDP) Rashid hupata usaidizi na miongozo ya taarifa anazotumia kufikisha Elimu kwa vijana. Ameeleza kuwa UNICEF kuna ‘UNICEF Advocacy Guide’ ambao ni muongozo wa uchechemuzi kwa vijana, humsaidia kwa namna mbalimbali za kuweza kufanya uchechemuzi kwa vijana, pia humsaidia kupata maarifa na ujuzi zaidi. Sio hivyo tu,Rashid ameongeza kuwa UNESCO pia huwapa miongozo mbalimbali ikiwemo kupitia kozi ya mtandaoni ya afya ya uzazi kwa kina(CSE Online Course) ikitolewa kwa baadhi ya vyuo ambapo mradi wa O3Plus upo, hutolewa bila malipo, inayoitwa.
Rashid akiri kutumia akili mnemba katika kutengeneza maudhui ya kutoa elimu Kwa Vijana
"Mimi mwenyewe natumia akili mnemba kwa ajili ya kupata usaidizi katika kutengeneza maudhui, ninaweza nikawa nina wazo,lakini akili mnemba inanisaidia kwamba nitumie nyimbo gani,nitumie maneno gani, nipangilie katika mpangilio gani, nitumie dakika ngapi na mengine mengi."
Siku ya Kimataifa ya stadi za Vijana iliyoanzishwa mwaka 2014 ina Umuhimu na uzito kiasi gani?
Rashid amesema kwamba uwepo wa siku hiyo ni muhimu kwa Vijana,hasa mwaka huu ikichagizwa na kauli mbiu juu ya Uwezeshaji wa Vijana kwa kutumia akili mnemba. Akiongeza kuwa Vijana wanahitaji ujuzi wanapoenda kujiajiri katika biashara zao ama kuajiriwa,na ujuzi lazima urahisishwe ndiyo maana kuna akili mnemba.