Kifo cha Buhari, Katibu Mkuu atuma salamu za rambirambi
Kifo cha Buhari, Katibu Mkuu atuma salamu za rambirambi
Masuala ya UM
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametuma salamu za rambirambi kufuatia taarifa za kifo cha Rais wa zamani wa Nigeria Muhammadu Buhari kilichotokea Julai 13 huko London, Uingereza. Alikuwa na umri wa miaka 82.
Kupitia msemaji wake Stéphane Dujarric, Katibu Mkuu amesema amesikitishwa sana na taarifa za kifo cha Buhari, akimtaja kuwa kiongozi aliyejitoa kwa dhati kuendeleza uhuru, uthabiti, na maendeleo ya taifa lake wakati wa uongozi wake.
“Rais Buhari alionesha dhamira kubwa katika kulinda mamlaka ya taifa lake na kuhimiza amani na usalama katika eneo la Afrika Magharibi na Bonde la Ziwa Chad,” imesema taarifa hiyo iliyotolewa jijni New York, Marekani siku ya Jumatatu. “Pia alikuwa mtetezi shupavu wa ushirikiano wa kimataifa na wa kikanda.”
Katibu Mkuu ametuma salamu za pole kwa familia ya marehemu, serikali ya Nigeria, na wananchi wote wa Jamhuri ya Shirikisho ya Nigeria wakati huu wa maombolezo ya kitaifa.
Muhammadu Buhari alihudumu kama Rais wa Nigeria kuanzia mwaka 2015 hadi 2023.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, atakumbukwa kwa juhudi zake katika kupambana na rushwa, kuimarisha usalama wa ndani, na kukuza uhusiano wa kimataifa.’