Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HLPF 2025: Wadau wakutana Umoja wa Mataifa kujadili utekekezaji SDGs

Picha ya Jumba la Malengo ya Maendeleo Endelevu wakati wa Mkutano wa Malengo ya Maendeleo Endelevu mnamo Septemba 2023. (New York; Oktoba 2023) © Ofisi ya Ushirikiano/Patrick MacLeod.
© Partnerships Office/Patrick M Muonekano wa banda la Malengo ya Maendeleo Endelevu.

HLPF 2025: Wadau wakutana Umoja wa Mataifa kujadili utekekezaji SDGs

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu la Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Endelevu, HLPF la mwaka huu wa 2025 limeanza leo hapa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ambapo wadau kutoka katika nyanja mbalimbali duniani wanakutana kujadili namna ya kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs. 

Jukwaa hili la HLPF linalosimamiwa na Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa (ECOSOC), linafanyika kuanzia leo tarehe 14 hadi wiki ijayo tarehe 23 ya mwezi huu wa Julai Julai na safari hii likilenga kuangazia malengo Matano katika ya 17 ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu nayo ni afya bora na ustawi, usawa wa kijinsia, kazi zenye staha na ukuaji wa Uchumi, Maisha chini ya maji kama vile uhifadhi bora wa bahari na vilevile lengo namba 17 ambalo ni Ushirikiano kwa ajili ya Malengo, lengo la jumla ambalo hutathiminiwa  kila mwaka, likisisitiza umuhimu wa kufufua ushirikiano wa kimataifa na kuboresha njia za utekelezaji ikiwemo ufadhili.

Kupitia jukwaa hili la HLPF nchi hubadilishana uzoefu kwa kutoa tathmini zao wenyewe namna wanavyoyasongesha malengo ya maendeleo endelevu katika maeneo yao huku wakitoa maarifa kuhusu maendeleo na pia changamoto.

Ingawa HLPF ni jukwaa la kiserikali la Umoja wa Mataifa, pia hukutanisha sauti mbalimbali, zikiwemo vikundi vya vijana, mamlaka za mitaa, watu wa jamii za asili, asasi za kiraia, wasomi, sekta binafsi na mashirika ya mfumo wa Umoja wa Mataifa.

Kupitia jukwaa hili, leo hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres anategemewa kuzindua ripoti ya mwaka huu wa 2025 ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs.