Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ITURI: Silaha zawekwa chini, nyavu za samaki zachukua nafasi

Boti kadhaa za uvuvi ziko kwenye ufuo wa mchanga huko Djugu, mkoa wa Ituri, DRC, huku wavuvi na nyavu za uvuvi zikiwa karibu.
MONUSCO MONUSCO Yazindua Mradi wa uvuvi ili Kupunguza mivutano huko Djugu DRC.

ITURI: Silaha zawekwa chini, nyavu za samaki zachukua nafasi

Amani na Usalama

Miezi sita iliyopita, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, (MONUSCO) ulizindua mradi wa ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba vinavyoelea huko mji wa Tchomia, kitovu cha biashara kilicho umbali wa kilomita 62 kusini mwa Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri, mashariki mwa nchi.

Lengo la mpango huu lilikuwa kupunguza vurugu katika jamii na kupambana na ukosefu wa ajira kwa kuunda ajira za muda kwa watu 100, wakiwemo wanawake 50 walio katika mazingira magumu na wanaume 50 waliokuwa wapiganaji msituni, vijana walioko hatarini au watu wasio na ajira, huku ikikuza ujumuishaji wa kijamii na kiuchumi ndani ya jamii.

Vifaranga vya samaki kutoka MONUSCO

Tchomia iko kwenye mwambao wa Ziwa Albert, ambapo uvuvi ndio chanzo kikuu cha maisha kwa wakazi wake. Vijana hukua katika mazingira yaliyo karibu sana na shughuli za uvuvi.

Hata hivyo, uvuvi wa kupindukia umesababisha kutoweka kwa aina nyingi za samaki. Kulingana na Idara ya uvuvi jimboni Ituri, ni aina 15 pekee za samaki kati ya 60 zilizowahi kurekodiwa ndizo bado zipo. Kwa kujibu hali hiyo, mradi wa MONUSCO unatoa mbadala endelevu kupitia mbinu mpya ya ufugaji wa samaki kwa vizimba vinavyoelea.

Tangu uzinduzi wake, vifaranga 53,000 vya tilapia vimepandikizwa, na wanufaika 100 wamefunzwa jinsi ya kutengeneza vizimba vinavyoelea vya mita za mraba 5 (urefu wa mita 3) kwa kutumia vifaa rafiki kwa mazingira kama mapipa ya plastiki na mabomba ya PVC.

Nyavu zimefungwa, vizimba vimelishwa mbolea, na samaki wanapewa chakula. Mavuno yanatarajiwa hivi karibuni.

Faida ni nyingi

“Mradi huu ni wa ubunifu kwa jamii ya wavuvi ambao mara kwa mara hukumbana na changamoto kutoka kwa mamlaka, ikiwemo kunyang’anywa kwa vifaa vya uvuvi vilivyopigwa marufuku. Uvuvi wa jadi una hatari nyingi, kama vile kulala usiku ziwani, kuvamiwa au kuzama. Mradi huu husaidia kupunguza hatari hizo,” ameeleza Florent Gbombo Nzama, Mratibu wa Mtandao wa Mashirika kwa Maendeleo Endelevu (RAD), mshirika mtekelezaji anayesaidia P-DDRCS amba oni Mpango wa serikali ya DRC wa upokonyaji silaha, usitishaji vita, urejeshaji wa jamii, na uimarishaji wa utulivu. MONUSCO inasaidia kwa kutoa msaada wa kiufundi, vifaa, na usalama.

Mbadala wa kujiunga na makundi ya kivita

Wanufaika wa moja kwa moja wamepangwa katika vikundi vinne vya ufugaji wa samaki vyenye wanachama 25 kila kimoja, kwa lengo la kuwa vyama vya ushirika endelevu na vinavyoweza kujitegemea katika Ziwa Albert. Lengo ni kuhakikisha shughuli hii inadumu na kusaidia kupunguza ukosefu wa ajira, ambao ni chanzo kikubwa cha vijana kujiunga na makundi ya kivita.

Kutoka msituni kupigana upande wa waasi hadi kuingia ziwani na kuwa mtaalamu wa ufugaji wa samaki, ndio simulizi tunayopata kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, simulizi ya matumaini kwa mustakabali wa jamii iliyogubikwa na vita kila uchao. Mwenyeji wako ni Sharon Jebichii.

Emmanuel Tibasima Kiza mkazi wa ambaye anasema “leo mimi nimekuwa mtaalamu wa ufugaji wa samaki. Mimi najenga vizimba.”

Kwa miaka miwili Emmanuel alikuwa mpiganaji wa msituni. Alirejea uraiani akawa muda mrefu bila ajira, ndipo akapata taarifa za mafunzo ya ufugaji kisasa wa wa samaki.

Mafunzo yalikuwa ya miezi mitatu kutoka ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO, huku wakipatiwa ujira wa dola 5 kwa siku. Sasa amekuwa mtaalamu akisema, “na ninajua kufuga samaki, na wamenifundisha kutengeneza chakula cha kulisha samaki.”

Familia zimeimarika

Emmanuel amefundishwa pia kujenga vizimba vya kufugia samaki ziwani Albert, na kwa kazi hiyo, kwa siku hakosi dola 20. Na matokeo ni dhahiri. “Kwa sasa watoto wangu wanaendelea kusoma vizuri,  wanasoma vizuri, na wanavaa vizuri. Na sasa nimeshaanza kazi ya ujenzi wa nyumba yangu. Kazi ya kwenda porini , wala kwenda kwenye makundi yaliyojihami vinapoteza muda bure.”

Kikundi chao kina matumaini ya kuvua tani 60 za samaki kila mwaka, sasa anahoji, “Kwa nini niingie porini?

Hivyo anaomba vijana wasio na ajira na walio bado porini, “watoke, waje na sisi tuko tayari kuwakaribisha tujenge nchi.”