Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HLPF 2025: Jukwaa la UN kuangazia afya, usawa wa kijinsia na bahari katika juhudi za kufanikisha SDGs

Mabango katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa yakionesha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs (Pichaya maktaba)
UN News/Abdelmonem Makki Mabango katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa yakionesha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs (Pichaya maktaba)

HLPF 2025: Jukwaa la UN kuangazia afya, usawa wa kijinsia na bahari katika juhudi za kufanikisha SDGs

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Wakati muda  wa mwisho mwaka 2030 kukamilisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs ukikaribia, mawaziri, wataalamu na wawakilishi wa jumuiya za kiraia kutoka kote duniani wanakutana jijini New York kuanzia Jumatatu hii ya Julai 14 kwa ajili ya jukwaa la ngazi ya juu la Umoja wa Mataifa la kuharakisha utekelezaji wa SDGs.

Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu la Maendeleo Endelevu la 2025 (HLPF) linafanyika mara tu baada ya Mkutano wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo uliofanyika mjini Sevilla, Hispania.

Mkutano huo ulimalizika kwa wito mpya wa kuchukua hatua za haraka kufidia pengo kubwa la kila mwaka la dola trilioni 4 linalohitajika kufanikisha SDGs – jambo linalosisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji na kufanyia mageuzi mfumo wa kifedha wa dunia.

Jukwaa hilo, litakalosimamiwa na Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa (ECOSOC), litafanyika kuanzia tarehe 14 hadi 23 Julai katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.

Hivi ndivyo mambo matano muhimu ya kujua kuhusu jukwaa la mwaka huu:

1. Lengo kuu ni kuharakisha utekelezaji

HLPF ya 2025 itafanyika kwa kaulimbiu:

“Kusongesha mbele suluhisho endelevu, jumuishi, la kisayansi na la msingi wa ushahidi kwa Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu na Malengo yake ya Maendeleo Endelevu kwa kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.”

Hii inaonesha hali ya dharura inayoongezeka. Kadri mwaka 2030 unavyokaribia, jukwaa litaangazia mikakati ya vitendo inayotegemea takwimu ili kufidia mapengo ya utekelezaji  hasa kwa kuzingatia migogoro ya kimataifa kama mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa usawa na kuyumba kwa uchumi.

2. Malengo matano ya SDGs kupewa kipaumbele

Kila mwaka, HLPF hufanya tathmini ya kina ya baadhi ya malengo. Mwaka 2025, mwelekeo utakuwa kwenye:

  • SDG 3: Afya bora na ustawi
  • SDG 5: Usawa wa kijinsia
  • SDG 8: Kazi zenye staha na ukuaji wa uchumi
  • SDG 14: Maisha chini ya maji
  • SDG 17: Ushirikiano kwa ajili ya malengo

Malengo haya yanagusa masuala mbalimbali – kutoka afya ya umma na usawa wa kijinsia hadi ustahimilivu wa kiuchumi na uhifadhi wa mazingira ya baharini. SDG 17, linalokaguliwa kila mwaka, linasisitiza umuhimu wa kufufua ushirikiano wa kimataifa na kuboresha njia za utekelezaji – ikiwemo ufadhili, ambao nchi zilikubaliana mwezi uliopita huko Sevilla.

3. Nchi zitaonesha maendeleo yao kwa hiari

Sifa kuu ya HLPF ni Tathmini za Hiari za Kitaifa (VNRs) – ambazo ni tathmini binafsi zinazotolewa na nchi wanachama kuhusu hatua wanazopiga kuelekea SDGs. Mwaka 2025, nchi kadhaa zinatarajiwa kuwasilisha VNRs zao, zikitoa maarifa kuhusu mafanikio na changamoto zinazoendelea.

Tathmini hizi huimarisha uwazi, kujifunza kwa pamoja na uwajibikaji. Pia huwapa nafasi mashirika ya kiraia na wadau wengine kushiriki moja kwa moja na serikali kuhusu vipaumbele vya maendeleo.

MUHIMU: VNR Labs – vipindi vya mwingiliano vinavyolenga tathmini za kitaifa – huunda nafasi ya mazungumzo, uvumbuzi na ushirikiano.

4. Si serikali tu zitakazohusika

Ingawa HLPF ni jukwaa la kiserikali la Umoja wa Mataifa, pia hukutanisha sauti mbalimbali, zikiwemo vikundi vya vijana, mamlaka za mitaa, watu wa jamii za asili, asasi za kiraia, wasomi, sekta binafsi na mashirika ya mfumo wa UN.

Kutakuwa na programu tajiri ya matukio ya pembeni, maonesho na mijadala ya kahawa. Mtazamo huu jumuishi unaakisi roho ya Ajenda ya 2030, inayotambua kuwa maendeleo endelevu ni jukumu la pamoja la dunia nzima.

5. 5 - 4 - 3 - 2 - 1: Huu ndio muda wa uamuzi

Kwa kuwa zimebaki miaka mitano tu kufikia Ajenda ya 2030, HLPF ya 2025 ni wakati muhimu wa mwelekeo.

Ni zaidi ya ukaguzi wa kila mwaka. Kikao cha mwaka huu kinakuja wakati ambapo sayansi, mshikamano na hatua za haraka lazima viungane. Kitasaidia kuweka mwelekeo kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa SDGs wa mwaka 2027, ambapo viongozi wa dunia watapima maendeleo ya pamoja na kuamua msukumo wa mwisho kuelekea 2030.

Kinachofanyika sasa – katika kipindi hiki cha "sehemu mbili ya tatu ya muda uliopangwa" – kitabaini kama SDGs zitakuwa ahadi ya dunia iliyotekelezwa au fursa iliyoachwa ipite.