Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Chaguo lisilokubalika- Njaa au upigwe risasi

Msichana mdogo akitembelea hema lake ambalo liliharibiwa kufuatia mashambulizi ya anga huko Deir al-Balah, Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba
Msichana mdogo akitembelea hema lake ambalo liliharibiwa kufuatia mashambulizi ya anga huko Deir al-Balah, Gaza.

Gaza: Chaguo lisilokubalika- Njaa au upigwe risasi

Amani na Usalama

Baada ya vifo vya watoto kadhaa siku ya Alhamisi katika shambulio la anga lililofanywa na Israel dhidi ya wapalestina waliokuwa wamesimama kwenye foleni wakisubiri msaada wa vyakule vyenye virutubisho katikati mwa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwan na Israeli, maafisa wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu wamelaani tena mauaji ya watu katika maeneo ya ugawaji misaada ndani ya ukanda huo.

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu ya (OHCHR), Ravina Shamdasani, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo kuwa, "tumeelezea wasiwasi wetu kuhusu uhalifu mkubwa wa kikatili ambao tayari umetokea na hatari ya kutokea tena kwa uhalifu kama huo, ambapo watu wanasimama kwenye foleni wakisubiri bidhaa muhimu kama chakula na dawa, halafu wanashambuliwa — ambapo tena... wanakabiliwa na chaguo kati ya kupigwa risasi au kupata chakula.”

Bahati mbayá ya kifo

“Hali hii haikubaliki, na inaendelea,” amesema kwa masikitiko.

Bi. Shamdasani amesema kuwa ofisi yake bado inachunguza tukio hilo ambapo takribani wapalestina 15, wakiwemo wanawake na watoto, wanaripotiwa kuuawa na shambulio mbele ya kliniki mjini Deir al-Balah inayosimamiwa na shirika la misaada la Marekani la Project Hope, ambalo ni mshirika wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).

Katika taarifa siku ya Alhamisi, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell, alisema kuwa kuua familia zinazojaribu kupata msaada wa kuokoa maisha ni jambo “lisilokubalika kabisa”.

Jeshi la Israel linaripotiwa kusema kuwa lilikuwa likimlenga mwanachama wa Hamas aliyeshiriki katika mashambulizi ya kigaidi nchini Israel tarehe 7 Oktoba 2023.

Alipoulizwa kuhusu busara ya kuwaweka raia, wakiwemo watoto, katika hatari ya kifo ili kumlenga mtu mmoja, Bi. Shamdasani amesema kuwa katika kipindi chote cha mzozo wa Gaza, OHCHR imekuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu kuheshimiwa kwa misingi ya msingi ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, ikiwemo utambuzi wa raia na matumizi ya nguvu kwa uwiano.

“Tumeona kuwa kati ya idadi yote ya vifo huko Gaza; sehemu kubwa ni wanawake na watoto. Hali hii tena inazua maswali makubwa kuhusu kama kanuni hizi za msingi zinaheshimiwa,” ameongeza.

Watu wenye njaa huko Gaza wanahatarisha maisha yao kwa kupigwa risasi wanapokwenda kuchukua misaada ya chakula.

Mamia wauawa wakisubiri msaada wa chakula

Mauaji ya wapalestina katika au karibu na maeneo ya ugawaji wa misaada na karibu na misafara ya kibinadamu yamekuwa jambo la kawaida katika mazingira ya vizuizi vya kuingiza chakula, mafuta na bidhaa nyingine za misaada katika Ukanda wa Gaza, hasa tangu kuanzishwa kwa maeneo ya ugawaji wa chakula yanayoendeshwa na Gaza Humanitarian Foundation (GHF) ambayo hayahusiani na UN.

Tangu mwishoni mwa Mei, mfumo huu wa kijeshi wa usambazaji wa misaada, unaoungwa mkono na Israel na Marekani, umelenga kuipuuza UN na washirika wake wenye uzoefu wa kibinadamu.

Bi. Shamdasani wa OHCHR amesema kuwa kuanzia tarehe 27 Mei, wakati GHF ilipoanza kazi Gaza, hadi 7 Julai, OHCHR ilirekodi vifo 798, "ikiwa ni pamoja na 615 karibu na maeneo ya GHF na 183 waliodhaniwa kuuawa njiani kwenye misafara ya misaada."

Majeruhi wa risasi

Vifo vya karibu watu 800 waliokuwa wakijaribu kupata misaada vilitokana “kwa kiasi kikubwa na majeraha ya risasi,” amesema Bi. Shamdasani.

Akiungana naye kulaani mauaji hayo, msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Christian Lindmeier, amesema kuwa “polepole anakosa maneno ya kuelezea hali hii.”

“Watu kupigwa risasi kwenye maeneo ya misaada… wanawake, watoto, wanaume, wavulana na wasichana kuuawa wakichukua chakula au wakiwa kwenye maeneo yanayodhaniwa kuwa salama kama makazi au wakielekea kwenye kliniki — hili limepitiliza kikomo cha kutokubalika.”

Uhaba wa mafuta

Alipoulizwa kuhusu mafuta lita 75,000 yaliyoingizwa Gaza Jumatano, ikiwa ni mara ya kwanza kwa zaidi ya siku 130, Bwana Lindmeier amesema, "ni vizuri kwamba mafuta haya yameingia hatimaye… lakini hatupaswi kutegemea habari za ‘misaada ya dharura’ kama hii,” iwe ni mafuta, chakula au misaada mingine.

“Unapaswa kuwa na ugawaji wa mara kwa mara wa misaada Gaza ili kudumisha maisha — kwa ajili ya ambulensi, hospitali, mitambo ya kuchuja maji ya chumvi, na mikate… vyote vinavyohitajika kuweka uhai,” amesema.

Msemaji wa WHO pia ameeleza kuwa asilimia 94 ya hospitali Gaza sasa zimeharibiwa au kuharibiwa kabisa, huku watu wakizidi kulazimishwa kukimbia makazi yao na kukusanyika kwenye maeneo madogo zaidi.

Bwana Lindmeier ameelezea pia matumaini yake kuwa mazungumzo ya kusitisha mapigano yatakuwa na matokeo chanya.

“Amani ndiyo dawa bora, na kufungua mipaka ndilo suluhisho pekee la kweli,” ametamatisha.