Siku ya idadi ya watu duniani yaadhimishwa kwa kuangazia uwezeshaji wa vijana
Siku ya idadi ya watu duniani yaadhimishwa kwa kuangazia uwezeshaji wa vijana
- Vijana wanaleta mabadiliko makubwa chanya kwenye jamii
- Lakini wanakumbwa na changamoto lukuki wanapojaribu kuanzisha familia
- Wanahitaji mazingira wezeshi ikiwemo huduma za malezi ya watoto
- Serikali zitunge sera sahihi za afya na uzazi na malezi
Katika siku ya Idadi ya Watu duniani hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amepongeza kizazi cha sasa cha vijana kwa uwezo wao mkubwa wa kuleta mabadiliko chanya duniani.
“Leo tunasherehekea uwezo na ahadi ya kizazi cha vijana kilicho na idadi kubwa zaidi kuwahi kuishi. Wao si tu wanaunda mustakabali wetu, bali pia wanadai dunia yenye haki, ujumuishaji na ustawi endelevu,” amesema Guterres.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kuwawezesha vijana kuanzisha fawazitakazo katika dunia ya haki na matumaini na inasisitiza tena ahadi ya Mkutano wa Kimataifa wa Idadi ya Watu na Maendeleo uliofanyika mwaka 1994, kuwa kila mtu ana haki ya kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha na mustakabali wake,” amesema Guterres.
Changamoto lukuki
Hata hivyo, Guterres ametambua changamoto nyingi zinazowakumba vijana duniani kote, ikiwemo hali ngumu ya kiuchumi, ukosefu wa usawa wa kijinsia, matatizo ya kiafya, athari za mabadiliko ya tabianchi, na migogoro.
“Pamoja na hayo yote, vijana wanaonesha uongozi wa kweli – kwa ujasiri, dhamira na uwazi. Wanatoa wito kwa mifumo inayotambua haki zao na kusaidia maamuzi yao,” ameongeza.
Wajibu wa serikali
Katibu Mkuu amezihimiza serikali kuwekeza katika sera zinazohakikisha elimu bora, huduma za afya, ajira yenye staha, na ulinzi kamili wa haki za uzazi kwa vijana.
“Tusimame pamoja na vijana na tujenge dunia ambamo kila mtu anaweza kuamua hatima yake katika mazingira ya haki, amani na matumaini,” amesema Guterres.
Mazingira wezeshi kwa vijana ni muhimu kwa jamii
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, (UNFPA), Dkt. Natalia Kanem, katika ujumbe wake ametoa wito kwa jamii na serikali kuweka mazingira yanayowawezesha vijana kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha na familia zao.
Amenukuu ripoti ya hivi karibuni ya UNFPA iliyoonesha kuwa mtu 1 kati ya 5 walio na umri wa chini ya miaka 50 wanatarajia kuwa na familia ndogo kuliko walivyotarajia, huku karibu theluthi moja ya walio na umri zaidi ya miaka 50 wakisema walikuwa na watoto wachache kuliko walivyotaka.
Katika ujumbe wake wa siku hii, Dkt. Kanem amesema changamoto ya kweli si kupungua kwa viwango vya uzazi kama inavyodhaniwa, bali ni ukosefu wa uwezo wa vijana kufanya maamuzi ya uzazi kwa hiari.
Huduma za malezi ya watoto ni moja ya majawabu
"Vijana wengi hawawezi kuunda familia wanazotamani, huku wakilaumiwa kwa kushindwa kuongeza idadi ya watoto na kuwekwa katika presha ya kulitatua tatizo hilo,” amesema Dkt. Kanem.
Dkt. Kanem amesisitiza umuhimu wa sera rafiki kwa familia, kama vile huduma nafuu za kulea watoto, likizo za uzazi zinazolipwa na kubadilika, pamoja na kushirikishwa kwa wanaume katika malezi.
Pia amesisitiza uwekezaji katika elimu ya afya ya uzazi na jinsia kwa vijana, ili kuwasaidia kufanya maamuzi ya busara.
Akatamatisha kwa kusema "jamii jumuishi na endelevu huanza na kuhakikisha kila kijana ana haki na uwezo wa kufikia ndoto ya kuwa mzazi kwa njia inayomfaa – katika dunia yenye usawa, matumaini, na fursa."
Siku ya idadi ya watu duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 11 Julai, ikiwa ni fursa ya kuangazia changamoto na mafanikio katika masuala ya idadi ya watu, maendeleo, na haki za binadamu.