Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNDP na serikali Kenya wajengea uwezo wananchi ili wakabiliane na tabianchi

Teknolojia na ushirikiano vinavyotatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima wa maeneo kame ya Kenya.
© UNDP Teknolojia na ushirikiano vinavyotatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima wa maeneo kame ya Kenya.

UNDP na serikali Kenya wajengea uwezo wananchi ili wakabiliane na tabianchi

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katika maeneo kame ya Kenya, mvua moja ikikosa kunyesha, inaweza kuleta njaa, umaskini na kukosa matumaini. Lakini badala ya kukata tamaa, jamii za wakulima katika kaunti za Tana River sasa zinatoa simulizi kwa ujasiri na mabadiliko. Kupitia msaada kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Ukame (NDMA) na Serikali za Kaunti, wakulima wanatumia teknolojia rafiki kama umwagiliaji wa maji kwa nishati ya jua, kilimo cha kisasa na ushirika wa kijamii kuinua maisha yao.

Katika eneo la Ngao katika Kaunti ya Tana River, nchini Kenya ushirikiano wa mashirika na serikali umebadilisha hali ya kilimo kwa jamii. Awali kukosekana kwa msimu mmoja wa mvua kulimaanisha janga sio tu kwa mifugo bali pia kwa binadamu. Lakini mbegu ya mabadiliko ikatokea kupitia mradi. Je ni mradi gani?  

Adam Ndamungu, Mkulima kutoka shirika la NDMA, Tana River Kenya.
© UNDP Adam Ndamungu, Mkulima kutoka shirika la NDMA, Tana River Kenya.

Adam Ndamungu, kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Ukame, NDMA katika kaunti ya Tana River, anafafanua jinsi mradi ulivyoanzishwa. Anaema " Mashirika pamoja na serikali kwa kushirikiana na UNDP, tukaleta pamoja serikali ya kaunti na Wizara ya Kilimo. Tukazindua miradi ya umwagiliaji wa maji – mmoja ukiwa hapa Ngao na mwingine kule Maroni. Hadi kufikia hapa, ni wazi kuwa tuko kwenye mwelekeo mzuri. Wakulima wameukubali mradi huu na pia wamejitolea kuendeleza kilimo kwa bidii. Hii ni ishara njema kwamba jitihada zetu zina matokeo chanya kwa jamii na maendeleo ya sekta ya kilimo."

Katika shamba lake lenye kijani kibichi, Moris Kadenge, Katibu wa kikundi cha Umwagiliaji hapa Ngao, anakumbuka changamoto kabla ya mradi na mafanikio ambayo yamegusa maisha yao kama jamii, anasema "Ninalima mazao mbalimbali kama mahindi, pojo, mchicha, nyanya na mengineyo. Hapo awali, tulitegemea mvua sana, lakini siku hizi mvua imekuwa haba na haitoshelezi mahitaji ya kilimo. Mwanzoni, tulikuwa tunapata mavuno ya takriban kilo 200 hadi 300.”

Kisha wakapata msaada kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP na mambo yakaanza kubadilika, Moris Kadenge anasema “Mazao yameongezeka kwa kiwango kikubwa na sasa tunavuna hadi tani nne na nusu au zaidi. Mavuno haya yamekuwa na manufaa makubwa kwa jamii – tunapata chakula cha kutosha kwa familia zetu, na kilichobaki tunakiuza ili kutimiza mahitaji mengine kama vile kugharamia elimu ya watoto. UNDP walitupatia mafunzo muhimu yaliyotuwezesha kuboresha mbinu zetu za kilimo. Mafunzo haya yamenisaidia binafsi kufikia hatua kubwa.”

Hakuona haya kukumbuka makazi yake ya awali. Moris Kadenge anaongeza kuwa “Hapo awali, nilikuwa nikiishi katika nyumba ya matope, lakini sasa nimeweza kujipanga na kujenga nyumba bora kutokana na mapato ya kilimo. Haya yote yamewezekana kwa sababu ya ushirikiano kati ya UNDP na wizara husika za kilimo. Kwa kweli, tumeona maendeleo na maisha yamebadilika. Tuna matumaini makubwa kwa siku zijazo."

Lucy Maina, mwanachama wa mpango wa umwagiliaji wa Ngao na kikundi cha Ndaramio kutoka Tana River, Kenya.
© UNDP Lucy Maina, mwanachama wa mpango wa umwagiliaji wa Ngao na kikundi cha Ndaramio kutoka Tana River, Kenya.

Kwa upande mwingine wa mradi, wanawake nao wamechukua nafasi yao. Lucy Maina, mwanachama wa Kikundi cha Umwagiliaji cha Ngao na kikundi cha Ndaramio, anasimulia safari ilivyokuwa akisema walianza kama vikundi vya kina mama, nami nilikuwa katika kikundi kimoja kinachoitwa Ndaramio. Kule tulikuwa tunatengeneza mikate kwa mikono, tukipika kwa kutumia makaa au kuni na kutumia sufuria za kawaida. Hali haikuwa rahisi, lakini tulijikakamua na tukaanza kikundi cha akina mama cha kukusanya pesa na kugawana kwa mzunguko, tukijisaidia kidogo kidogo. 

Lucy anaongeza kuwa baadaye, wakakutana na watu wa UNDP ambao wamewasaidia kwa kutupatia mashine za kisasa za kutengeneza mikate, mashine za kukata mikate vipande, na hata mashine za kusagisha nafaka. Hapo ndipo wakapata msukumo wa kuanza kilimo cha mahindi kwa kiwango kikubwa ili waweze kuwa na unga wa kutosha kwa shughuli zao. 

Anasema awali walikuwa wanalima kidogo tu, lakini sasa wamepanua mashamba yetu. na sasa wanaona faida tupu. akikiri kuwa hiki ndicho kinachoitwa kuwezeshwa, kwani UNDP wamewawezesha kwa vitendo. Kwa sababu mtu anapokupatia elimu na vifaa vya kazi, basi amekuwezesha kwa kiwango kikubwa sana."