Trakoma au Vikope si tatizo tena la kiafya la umma Burundi - WHO
Trakoma au Vikope si tatizo tena la kiafya la umma Burundi - WHO
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) leo Julai 11 limetangaza kwamba limeidhinisha Burundi kuwa imefanikiwa kuoandoa ugonjwa wa macho unaofahamika kama trakoma au vikope kama tatizo la kiafya la umma, na kuifanya kuwa nchi ya nane katika Kanda ya Afrika ya WHO kufikia mafanikio haya muhimu.
“Kuondoa ugonjwa kama trakoma au vikope ni mafanikio makubwa ya afya ya umma yanayohitaji jitihada za muda mrefu na kujitolea,” anasema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO. Anaongeza kusema anaipongeza serikali na watu wa Burundi kwa kazi yao ngumu na kujitolea. Na kwamba, “ni jambo la kufurahisha kuona Burundi ikijiunga na kundi la nchi zinazoongezeka ambazo zimeondoa angalau ugonjwa mmoja wa Magonjwa ya Tropiki Yaliyopuunzwa, NTD.”
Ugonjwa wa Trakoma au Vikope husababishwa na bakteria Chlamydia trachomatis na huenea kupitia mgusano wa moja kwa moja na watu, nyuso chafu au inzi waliogusa majimaji ya macho au pua. Maambukizi ya mara kwa mara husababisha makovu, kope kuingia ndani ya jicho, na hatimaye upofu. Duniani kote, ugonjwa huu bado uko katika jamii zilizo pembezoni zaidi ambazo zina upungufu wa maji safi na huduma za usafi wa mazingira.
Akizungumzia hatua hii, Dkt. Lydwine Baradahana, Waziri wa Afya ya Umma na Mapambano dhidi ya UKIMWI nchini Burundi amesema, uthibitisho huu ni hatua kubwa katika dhamira yao ya usawa katika afya na kwamba, “ni ushindi wa pamoja uliowezekana kupitia zaidi ya miaka 20 ya kuhamasisha taifa na mshikamano wa kimataifa. Nawashukuru washirika wote, watoa huduma za kijamii na taasisi zote nchini Burundi na nje ya nchi ambao walifanya mafanikio haya ya kihistoria kuwa halisi.”
Maendeleo ya Burundi
Kabla ya mwaka 2007, bila visa vilivyoripotiwa wala tafiti za kitabibu, kiwango cha ueneaji wa ugonjwa wa trakoma au vikope nchini Burundi hakikujulikana wazi. Mwaka huo, nchi ilianzisha mpango wa kukabiliana na Magonjwa wa Kitropiki yaliyopuuzwa, NTDs, ikiwemo minyoo ya tumbo, kichocho, matende, na trakoma yenyewe. Tafiti za msingi zilizofanyika kati ya 2009–2010 zilithibitisha kuwa trakoma ilikuwa katika baadhi ya maeneo nchini Burundi. Hii ilisababisha kuanzishwa kwa mikakati kulingana na mpango wa SAFE wa WHO kwa watu milioni 2.5 waliokuwa na uhitaji katika wilaya 12 za afya.
Mpango wa Burundi wa kuondoa trakoma uliungwa mkono kitaalamu na kifedha na mashirika ya CBM Christoffel Blindenmission, END Fund, Geneva Global, na WHO. Shirika la International Trachoma Initiative chini ya Task Force for Global Health lilitoa dawa ya azithromycin (Zithromax, Pfizer, New York, Marekani). WHO inaendelea kusaidia mamlaka za afya nchini kuangalia jamii ambazo zilikuwa na trakoma ili kuhakikisha ugonjwa huo haurudi tena.
“Mafanikio haya yanaonesha dhamira ya serikali kulinda watu wake walio katika mazingira hatarishi,” anasema Dkt. Xavier Crespin, Mwakilishi wa WHO nchini Burundi. “Kupitia uongozi wa Wizara ya Afya ya Umma na Mapambano dhidi ya UKIMWI, kujitolea kwa wahudumu wa afya ya jamii, msaada wa washirika muhimu, na mwongozo wa kiufundi kutoka WHO, mafanikio haya yamewezekana. Ushindi huu unatupa motisha ya kuendelea na juhudi hizo hadi tuondoe kabisa magonjwa yote ya tropiki yaliyopuuzwa.”
Ueneaji wa ugonjwa
Trakoma bado ni tatizo la kiafya katika nchi 32, ambapo watu milioni 103 wanaishi katika maeneo yanayohitaji hatua za kiafya dhidi ya ugonjwa huo. Trakoma hupatikana zaidi katika maeneo maskini na ya vijijini barani Afrika, Amerika ya Kati na Kusini, Asia, Pasifiki ya Magharibi, na Mashariki ya Kati.
Kanda ya Afrika imeathirika zaidi na trakoma, ambapo watu milioni 93 waliishi katika maeneo ya hatari kufikia Aprili 2024, wakichangia asilimia 90 ya mzigo wa trakoma duniani. Kupitia jitihada za miaka ya hivi karibuni, idadi ya watu wanaohitaji matibabu ya antibiotiki au dawa za viua vijiumbemaradhi dhidi ya trakoma katika Kanda ya Afrika imeshuka kwa watu milioni 96, kutoka milioni 189 mwaka 2014 hadi milioni 93 kufikia Aprili 2024 ikiwa ni upungufu wa asilimia 51.
Kwa sasa, kuna nchi 20 katika Kanda ya Afrika ya WHO zinazojulikana kuwa zinahitaji hatua za kuondoa trakoma. Nchi hizo ni: Algeria, Angola, Burkina Faso, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Côte d’Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Eritrea, Ethiopia, Guinea, Kenya, Msumbiji, Niger, Nigeria, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe. Nchi saba zilizothibitishwa na WHO kuwa zimeondoa trakoma ni Benin, Gambia, Ghana, Malawi, Mali, Mauritania na Togo. Nchi nyingine nne (Botswana, Guinea-Bissau, Namibia na Senegal) zimeripoti kufikia viwango vya kutokomeza ugonjwa huo.
Maendeleo duniani
Kwa kutangazwa kwa Burundi leo, jumla ya nchi 57 sasa zimeondoa angalau ugonjwa mmoja wa NTD kama tatizo la afya ya umma. Kati ya hizi, 24 (ikiwemo Burundi) zimefanikiwa kuondoa trakoma kama tatizo la afya ya umma. Nchi nyingine zilizofikia mafanikio haya ni Benin, Cambodia, China, Gambia, Iran, Laos, Ghana, India, Iraq, Malawi, Mali, Mauritania, Mexico, Morocco, Myanmar, Nepal, Oman, Pakistan, Papua New Guinea, Saudi Arabia, Togo, Vanuatu, na Vietnam.