Wanawake wapatanishi warejesha maelewano baina ya jamii Ituri
Wanawake wapatanishi warejesha maelewano baina ya jamii Ituri
Huko Djugu, jimboni Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, wanawake wapatanishi waliopatiwa mafunzo na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO, wamewezesha kurejea kwa mazungumzo baina ya jamii za Ezekere na Mandro ambazo kwa miaka kadhaa zilikuwa zinazozana.
Video ya MONUSCO inaanza na sauti hiyo ya Jacques Lokana Safari, Chifu wa eneo la Ezekere akieleza kuwa kuna baadhi ya wanajamii wa Mandro ambao walikuwa wanakataa kabisa kufika eneo la Ezekere kwa sababu tu walipatiwa taarifa za uongo kutoka mitandao ya kijamii.
Anaendelea kusema kuwa hali hii ilikwamisha wanajamii hawa kuishi pamoja. Lakini tunapongeza MONUSCO kwa kupatia mafunzo wanawake walioweza kuandaa kikao hiki na kuleta mtangamano wa kijamii.
Bwana Safari alikuwa anazungumza kando ya ukumbi ambako video imeonesha wanawake wakipatanisha wanaume wawili.
Kisha Georgina Love Kitambo, mmoja wa wanawake waliopatiwa mafunzo ya upatanishi wa kijamii anaonekana akizungumza, huku wanaume, wanawake na vijana wakisikiliza. Kisha anasema, “Kwa miaka mitano, Chifu wa Ezekere hakuwahi kufika Mandro. Tumebaini pamoja mambo yanayotusababishia kukosa maelewano. Ni hofu na leo tumeivuka. , na huo uoga leo tumeutokomeza. Tunatoa wito kwa wanawake wote na wakazi wote wa Ituri kuondokana na hofu kama tulivyofanya leo.”
Kwa mujibu wa MONUSCO juhudi hii ya upatanisho inachangia kuimarisha kuishi pamoja kwa amani katika eneo hilo.