Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Alimpigania msichana ambaye dunia ilimsahau: Mchango wa Dk. Natalia Kanem kwa UN

Dkt. Natalia Kanem (kushoto), Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi na Idadi ya Watu, (UNFPA), akizungumza na Mita Hosali katika mahojiano na UN News.
UN News
Dkt. Natalia Kanem (kushoto), Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi na Idadi ya Watu, (UNFPA), akizungumza na Mita Hosali katika mahojiano na UN News.

Alimpigania msichana ambaye dunia ilimsahau: Mchango wa Dk. Natalia Kanem kwa UN

Afya

Dkt. Natalia Kanem anapoangazia uongozi wake wa miaka minane katika shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi na Idadi ya Watu, (UNFPA), haanzi na takwimu za kimataifa, mafanikio ya mikutano, au hata kumbukumbu za ziara zake kwenye kambi za wakimbizi.

Anarudi tena na tena kwenye taswira moja: ya msichana  mwenye umri wa miaka 10 – aliye kwenye ukingo wa ujana, mustakabali wake ukiwa haujulikani, na haki zake bado zikiwa zinajadiliwa.

“Je, ataweza kuendelea na shule, kuhitimu, na kujitengenezea njia yake maishani?” Dk. Kanem anajiuliza. “Au ataathirika na mambo kama ndoa za utotoni, ukeketaji, au umaskini uliokithiri?”

Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Natalia Kanem (katikati), akutana na vijana katika hafla huko Cotonou, Benin.
© UNFPA/Abdoulatif Keita
Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Natalia Kanem (katikati), akutana na vijana katika hafla huko Cotonou, Benin.

Swali hilo zito na msichana huyo, kwa hakika si mtoto mmoja, bali mfano wa mamilioni kote duniani ambao mustakabali wao uko hatarini – vimekuwa alama ya utumishi wa Dk. Kanem kama Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA.

Kutoka siku zake za mwanzo akiongoza harakati huko Afrika Mashariki hadi kusimamia shirika lenye bajeti ya dola bilioni 1.7 likihudumu  katika nchi zaidi ya 150, Dk. Kanem ameisimamia UNFPA kupitia mabadiliko ya kimataifa, misukosuko ya kisiasa, na upinzani wa kiitikadi. Zaidi ya yote, ameongoza mapinduzi makubwa katika maisha ya mamilioni ya wanawake na wasichana.

Mwezi huu, anang’atuka. “Ni wakati wa kukabidhi kijiti,” Dkt. Kanem, mwenye umri wa miaka 70 amewaambia wafanyakazi wake – jeshi la watu 5,000 – katika hotuba ya video mapema mwaka huu. “Nimeahidi kufanya kila niwezalo kuendelea kuweka UNFPA katika nafasi ya kuendelea kufanya mambo makubwa.”

Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Natalia Kanem (katikati) akitembelea Soko la Mamas lililopo Port Vila, Vanuatu.
© UNFPA Vanuatu
Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Natalia Kanem (katikati) akitembelea Soko la Mamas lililopo Port Vila, Vanuatu.

Dk. Kanem ni nani? Safari yake hadi kufika UNFPA

Mzaliwa wa Panama na aliyesomea udaktari, Dk. Kanem alijiunga na UNFPA mwaka 2014 baada ya kazi katika masuala ya hisani. Uamuzi wake wa kutumikia “kusudi tukufu la Umoja wa Mataifa” kwanza ulimleta Tanzania, ambako alishangazwa na ushujaa wa kimya wa wafanyakazi wa mashinani. “Ni kweli kwenye ngazi ya nchi ndipo tunathibitisha thamani yetu,” ameiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Lakini kazi haikuwa rahisi. Mwaka 2017, alipoichukua hatamu ya shirika hilo, Dk. Kanem alirithi shirika lililokuwa likikabiliana na changamoto ya kupungua kujulikana kwake, ufadhili usiotegemewa, na upinzani endelevu kutoka kwa watendaji wenye msimamo mkali. Hata hivyo, UNFPA ilikua – si tu kwa bajeti, bali kwa hadhi.

“Nilipokuja, simulizi ilikuwa, ‘Sisi ni shirika dogo, lililokandamizwa, hakuna anayeelewa tunachofanya,’” amesema. “Sasa, nadhani ni wazi zaidi.”

Ufafanuzi huo ulitokana, kwa sehemu, na kile Dk. Kanem anachokiita “uongozi wa mawazo.” Iwe akipinga dhana potofu kuhusu uzazi au kukabiliana na ukatili wa kijinsia unaowezeshwa na teknolojia, alihimiza UNFPA kuongoza katika mijadala ya kimataifa. “Tupo katika soko la mawazo,” ameeleza. “Na tunapaswa kusema ukweli kwa njia ya kusisimua vya kutosha ili tuweze kupata washirika ambao harakati hii inahitaji.”

Wasichana wadogo wakiwa katika nafasi salama kwa Wanawake katika makazi ya wakimbizi ya Rohingya huko Cox's Bazar, Bangladesh.
UNFPA Bangladesh/Allison Joyce
Wasichana wadogo wakiwa katika nafasi salama kwa Wanawake katika makazi ya wakimbizi ya Rohingya huko Cox's Bazar, Bangladesh.

Mchango wake na uongozi madhubuti akiwa UNFPA:

Chini ya uongozi wake, shirika hilo limefundisha mamia ya maelfu ya wakunga, kusambaza mabilioni ya njia za uzazi wa mpango, na kupanua shughuli za kibinadamu ili kuwafikia wanawake na wasichana katika mazingira magumu zaidi – kutoka kambi za Rohingya huko Cox’s Bazar hadi Ukraine iliyoharibiwa na vita, na Haiti iliyokumbwa na kipindupindu.

Uwepo wa UNFPA katika maeneo ya migogoro haukuwa tu wa kimantiki, bali pia wa ishara. Nchini Sudan, Syria, na huko Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli, mahema yaliyokuwa na pedi za hedhi, blanketi, na sabuni viligeuka kimbilio. “Inawakilisha pumziko ambalo mwanamke analihitaji wakati wa shida,” amesema. “Unajua, tunaviita vifurushi vyetu ‘vifurushi vya utu kwa sababu hiyo.”

Zaidi ya kutoa huduma, Dk. Kanem alipandisha jukumu la UNFPA kama kiongozi wa mawazo katika ulimwengu uliogawanyika. Aliongoza shirika hilo katika mazungumzo magumu ya umma – kuhusu mimba za utotoni, wasiwasi wa mabadiliko ya hali ya hewa, viwango vya uzazi, na unyanyasaji mtandaoni – kwa msisitizo usiotetereka juu ya haki.

Zaidi ya robo tatu ya wasichana nchini Niger wameolewa wakiwa bado watoto.
© UNFPA Niger
Zaidi ya robo tatu ya wasichana nchini Niger wameolewa wakiwa bado watoto.

“Msichana wa umri wa miaka 10 yupo,” amesema. “Yale ambayo wazazi wake na viongozi wake wa dini na jamii yake wanadhani ni muhimu kwake kujiandaa vizuri, kwake kujua nini cha kufanya anapokabiliwa na mazoea ya kulazimishwa.”

Uongozi huo ulienea hadi kwenye data. Chini ya Dk. Kanem, UNFPA iliwekeza sana katika kusaidia sensa za kitaifa na kujenga dashibodi ili kusaidia wabunge kuunda sera za afya ya uzazi kwa kutumia taarifa za wakati halisi.

Ripoti ya Mwaka huu ya Idadi ya Watu Duniani, ambayo ni uchunguzi wa kila mwaka wa shirika hilo kuhusu mwenendo wa idadi ya watu, ilibadilisha simulizi za kawaida kuhusu kinachoitwa “kuporomoka kwa idadi ya watu” – ikibainisha kuwa wanawake na wanaume wengi huchelewesha kupata watoto si kwa sababu ya itikadi, bali kwa sababu hawawezi kumudu kuwalea.

Dk. Kanem amesifu ukarimu wa vijana ambao wanasema wanachagua kutokuwa na watoto kwa hofu ya kuzidisha mgogoro wa tabianchi.  Lakini hiyo sio inayooneshwa na data. “Kiwango cha uzazi duniani cha kubadilisha vizazi hakitishii sayari,” ameeleza. “Ukweli unasema: unaweza kuwa na watoto wengi kadri unavyoweza kumudu.”

Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt. Natalia Kanem akizungumza katika Kituo cha Afya cha Saupia huko North Efate, Vanuatu.
© UNFPA/Anirban Mahapatra
Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt. Natalia Kanem akizungumza katika Kituo cha Afya cha Saupia huko North Efate, Vanuatu.

Dira na msimamo wa Dk.Kanem dhidi ya changamoto na vikwazo katika uongozi wake

Uongozi wa Dk. Kanem uliambatana na mashambulizi yanayoongezeka dhidi ya haki za uzazi, kuongezeka kwa utaifa, na kukua kwa mashaka dhidi ya taasisi za kimataifa. Alikabiliana na miaka ya kupunguzwa kwa ufadhili wa Marekani – ikiwemo chini ya utawala wa sasa – hata kama mahitaji ya huduma za UNFPA yaliongezeka.

“UNFPA ina pesa nyingi kuliko tulivyowahi kuwa nazo,” amebainisha. “Lakini haitatosha kamwe kukomesha mtiririko wa mahitaji.”

Rasilimali pekee hazitahakikisha mustakabali wa shirika – uaminifu na uvumilivu ni muhimu vilevile. “Mfumo wa kimataifa wenyewe umehojiwa wakati ambapo unahitajika sasa zaidi kuliko hapo awali,” ameonya. “Lazima tujithibitishe kila siku. Na tunapofanya makosa, lazima tuamke na kuyasahihisha na kupata washirika ambao kweli watakuwa washirika.”

Mmoja wa washirika hao amekuwa sekta binafsi. Mnamo 2023, UNFPA iliungana na kampuni za teknolojia kuzindua hati fungani ya athari za maendeleo nchini Kenya, ikitoa huduma za afya ya uzazi kwa njia ya simu ili kuzuia mimba za utotoni na maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa wasichana wadogo.

UNFPA imefanya kazi kwa muda mrefu kumaliza mila potofu kama ukeketaji na ndoa za utotoni. Chini ya Dk. Kanem, kazi hiyo ilikuwa zaidi ya kubadili sheria, bali pia kubadili mawazo.

“Ndio, kabisa,” amesema, alipoulizwa kama maendeleo yalikuwa halisi. “Imekuwa muhimu sana kuona viongozi wa dini na viongozi wa kimila wakipinga mila fulani… na kufanya kazi na mifumo ya shule ili wasichana wenyewe waelewe hatari na waweze kufanya maamuzi bora kuhusu chaguo zao.”

coronavirus">COVID-19, amekiri, ilikuwa kikwazo. Shule zilipofungwa, baadhi ya jamii ziliharakisha sherehe. Lakini katika nchi nyingi – ikiwemo Indonesia yenye idadi kubwa ya watu – UNFPA imeona zoezi hilo likipungua, kwa sehemu kutokana na wanaharakati vijana kujitokeza kutoka ndani ya jamii zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt .Natalia Kanem alipotembea hospitali ya Panzi huko Bukavu jimboni Kivu Kusini nchini DR Congo. (Maktaba)
UNFPA/Luis Tato
Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt .Natalia Kanem alipotembea hospitali ya Panzi huko Bukavu jimboni Kivu Kusini nchini DR Congo. (Maktaba)

Ni upi mustakabali juu ya msimamo wake katika kutetea haki za wanawake na wasichana?

Akitazama mbele, Dk. Kanem hakukaa sana kwenye kutokuwa na uhakika. Badala yake amezungumzia juu ya uwezekano. “Tumejibadilisha, tumejiimarisha,” amesema. “Kuna uwezekano usio na kikomo kwa UNFPA.”

Mustakabali wake mwenyewe unajumuisha kile anachokiita “likizo fupi” – muda zaidi wa kusikiliza muziki, familia yake, na, hatimaye, yeye mwenyewe. Lakini hatakaa kimya kwa muda mrefu. “Najua kwamba shauku yangu kwa masuala ya wanawake na wasichana haitapungua,” amesema. “Imekuwa kazi ya upendo.”

Wazo lake la kuagana? Kurudi mara ya mwisho kwa msichana aliye katikati ya yote.

“Msichana huyo mwenye umri wa wa miaka 10 anapofanikiwa, kila mtu anafanikiwa,” amesema. “Utakuwa ni ulimwengu bora.”