Rwanda/DRC: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lakaribisha makubaliano ya amani
Rwanda/DRC: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lakaribisha makubaliano ya amani
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekaribisha kutiwa saini kwa makubaliano ya kihistoria ya amani kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda, ambayo ni hatua muhimu kuelekea kumaliza miongo kadhaa ya mizozo na ukosefu wa utulivu mashariki mwa DRC.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Jumatano Julai 7, wanachama wa Baraza hilo wametoa pongezi kwa pande zote mbili kwa kutiwa saini kwa makubaliano hayo mnamo 27 Juni 2025 jijini Washington DC, Marekani, na wakatoa shukrani zao za dhati kwa Marekani, Qatar, na Muungano wa Afrika kwa juhudi zao za upatanishi.
"Wanachama wa Baraza la Usalama wamehimiza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda kutekeleza kwa nia njema wajibu na ahadi zao kwa ajili ya amani ya kudumu katika mashariki mwa DRC," taarifa hiyo inaeleza.
Baraza hilo pia limesisitiza kuwa litaendelea kuunga mkono kwa karibu utekelezaji wa makubaliano hayo, likijumuisha kupitia ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO) na kwa mujibu wa Azimio 2773, ambalo linatoa wito kwa ushirikiano wa kikanda na ulinzi wa raia walioko katika maeneo ya migogoro.
Historia
Uhusiano kati ya DRC na Rwanda kwa muda mrefu umekuwa na hali ya kutoaminiana, huku kila upande ukilaumu mwingine kwa kuingilia masuala ya ndani, hasa kuhusiana na ghasia zinazoendelea katika mikoa ya mashariki ya DRC. Eneo hili limekumbwa na makundi yenye silaha, likiwemo kundi la waasi la M23, ambalo serikali ya DRC imekuwa ikidai linaungwa mkono na Rwanda, madai ambayo Rwanda imekanusha mara kwa mara.
Hali tete imeongezeka sana katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, na kusababisha maelfu ya watu kuhama makazi yao na kuzorota kwa hali ya kibinadamu. Shinikizo la kimataifa liliongezeka mwaka jana 2024 kufuatia mapigano makubwa na kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Makubaliano hayo mapya, ambayo baadhi ya vipengele vyake bado havijawekwa wazi kikamilifu, yanaripotiwa kujumuisha usimamizi wa mipaka kwa pamoja, kusalimisha silaha, na ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda.