UNESCO na Kamusi ya AI ya Kingereza - Kiswahili
UNESCO na Kamusi ya AI ya Kingereza - Kiswahili
Hii leo katika Ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, nchini Kenya kumefanyika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya lugha ya Kiswahili ambapo washiriki kwa njia moja au nyingine walionesha umahiri wao wa kuzungumza lugha hiyo inayotambuliwa hivi sasa kimataifa.
Mkuu wa Ofisi hiyo Bi. Hawa Bangura akifungua maadhimisho hayo amesema haya sio tu maadhimisho ya lugha, bali pia ni maadhimisho ya alama, urithi na kutambuliwa kwa lugha hiyo inayozungumza na watu zaidi ya milioni 200.
Amesema lugha hiyo ya kwanza ya kiafrika kutambuliwa kimataifa si jambo dogo kwani lugha hiyo imeunganisha watu wengi.
Ametamatisha hotuba yake kwa lugha ya kiswahili akisema, “asante sana na karibuni.”
Mkataa kwao Mtumwa
Balozi wa Tanzania nchini Kenya Dkt.Bernard Kibesse alianza hotuba yake kwa methali, Mkataa kwao Mtumwa akiwaeleza washiriki kuwa amechagua kuanza hotuba yake na methali hiyo kusisitiza Kiswahili sio tu lugha, bali pia “kinatukumbusha sisi ni akina nani, tumetoka wapi, pia utajiri wa utamaduni wetu wa kiafrika ulivyojikita kwenye asili yetu ya kibantu.”
Dkt. Kibesse ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la Mazingira, (UNEP) na la Makazi, (UN-HABITAT) nchini Kenya ameelezea pia umuhimu wa lugha ya Kiswahili katika kusongesha biashara hasa katika eneo huru la biashara Afrika, AfCTA.
Kamusi ya AI ya Kiingereza - Kiswahili
Mwakilishi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO Jay Ralitera akizungumza kwenye hafla hiyo amesema baada ya mashauriano na wataalamu wa Akili Mnemba, (AI) pamoja na wanaisimu, UNESCO imezindua Kamusi ya AI ya Kiingereza-Kiswahili.
Amesema kamusi hiyo iliyoko mtandaoni imebuniwa ili kuongeza uelewa wa pamoja wa istilahi zinazohusiana na AI miongoni mwa wazungumza wa lugha ya Kiswahili. “Juhudi hii ni hatua kuelekea kukuza matumizi ya lugha nyingi katika mtandao na ujumuishaji wa kidijitali,” amesema Bi. Ralitera.
Wanafunzi wa shule ya sekondari ya juu ya Mangu walitumia fursa ya kuweko kwenye maadhimisho hayo kwa kuonesha umahiri wao kwenye lugha ya kiswahili kwa kugani ngonjera iliyopatiwa jina Daraja, kwa maana kuwa Kiswahili sasa ni daraja.
Tazama video ya maadhimisho hapa.