Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya: UNICEF yasikitishwa na vifo wakati wa maandamano ya Saba Saba

Maandamano dhidi ya muswada ya kiuchumi yanayoendelea nchini Kenya.
UN News/Kevin Keitany
Maandamano dhidi ya muswada ya kiuchumi yanayoendelea nchini Kenya.

Kenya: UNICEF yasikitishwa na vifo wakati wa maandamano ya Saba Saba

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetoa tamko likieleza masikitiko yake kufuatia vifo na taarifa za kukamatwa kwa watoto wakati wa maandamano ya Saba Saba yaliyoikumba Kenya mapema wiki hii. Taarifa hiyo, iliyotolewa kutoka ofisi ya UNICEF jijini Nairobi tarehe 9 Julai, imeangazia kifo cha msichana mdogo aliyepigwa risasi akiwa nyumbani kwao, tukio la kusikitisha ambalo limezua hasira kutoka kwa makundi ya kutetea haki na umma kwa ujumla.

“Tunatoa pole za dhati kwa familia ya msichana huyo mdogo aliyeuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya nyumba yao,” taarifa ya UNICEF imesesema. “UNICEF pia inatiwa hofu kubwa na taarifa za watoto kukamatwa wakati wa maandamano. Watoto lazima walindwe dhidi ya madhara wakati wote na katika mazingira yoyote. Hilo ni haki yao ya msingi.”

Maandamano ya Saba Saba yanayofanyika kila mwaka tarehe 7 Julai yalianza mwaka 1990 kama harakati ya kudai demokrasia ya vyama vingi lakini sasa yamekuwa siku ya kitaifa ya kupaza sauti dhidi ya ufisadi wa serikali, utawala mbovu, na hali ngumu ya kiuchumi.

Maandamano ya mwaka huu yalishuhudia ushiriki mkubwa wa makundi ya vijana na mashirika ya kiraia, wakilalamikia gharama kubwa ya maisha na kile walichokiita matumizi ya nguvu kupita kiasi kutoka kwa polisi.

Makabiliano kati ya waandamanaji na polisi yalizuka katika miji kadhaa mikuu kama Nairobi, Kisumu, na Mombasa. Ingawa idadi kamili ya waliojeruhiwa na waliokamatwa haijathibitishwa rasmi, waangalizi wa haki za binadamu wameripoti majeruhi wengi na vifo vya angalau watu watano, wakiwemo watoto.

Mashirika yanayotetea haki za watoto yameitaka serikali kuwajibika kwa tukio hilo la kusikitisha, yakisisitiza kufanyika kwa uchunguzi wa wazi juu ya kifo cha msichana huyo na kuachiliwa mara moja kwa watoto wote waliokamatwa wakati wa maandamano.