Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania yawa mwenyeji wa mafunzo ya wakufunzi wa ulinzi wa amani

Picha ya pamoja baada ya uzinduzi wa mafunzo ya ukufunzi kwa wanadhimu wa Umoja wa Mataifa yaliyofanywa na Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN).
© DPO Picha ya pamoja baada ya uzinduzi wa mafunzo ya ukufunzi kwa wanadhimu wa Umoja wa Mataifa yaliyofanywa na Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN).

Tanzania yawa mwenyeji wa mafunzo ya wakufunzi wa ulinzi wa amani

Amani na Usalama

Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) kimezindua rasmi mafunzo ya ukufunzi kwa wanadhimu wa Umoja wa Mataifa. Mafunzo hayo yameanza tarehe 7 hadi 18 mwezi huu wa Julai  katika chuo hicho kilichoko Dar es Salaam, nchini Tanzania.

Washiriki ni 22 wakitoka Ghana, Nigeria, Ghana, Botswana, Zambia na mwenyeji Tanzania ambapo ufunguzi ulifanywa na Mkuu wa Chuo Brigedia Jenerali George Itang’are.

Akifafanua kuhusu lengo la mafunzo hayo ,Brigedia-Jenerali Itang’are amesema, “Kozi hii kwa namna ya kipekee kabisa imepata bahati ya kuwa na wakufunzi wabobezi wa kimataifa saba na wawili kutoka Tanzania.

Madhumuni ya kozi hii ni kuwawezesha maafisa wenye uzoefu katika ulinzi wa amani, kuwa na uwezo wa kuendesha mafunzo maalum ya walinzi wa amani katika mtaala kwa kuzingatia mtaala mpya ambao umetolewa na Umoja wa Mataifa .

Mafunzo yanatumia mtaala mpya wa Umoja wa Mataifa

Amesema unadhimu ndio nguzo kubwa kabisa katika operesheni yeyote ile, “hasa ukizingatia katika kipindi hiki ambapo dunia inakabiliwa na changamoto kadhaa za kiusalama. Ni kwa sababu hiyo, Umoja wa Mataifa uliona ni vyema kuupitia upya mitaala ya mafunzo, mafunzo ya wanadhimu wa ulinzi wa amani ili waweze kuendana na hali ya sasa. Kwa hiyo, tunatarajia kwamba maafisa wanadhimu wanaopitia katika kozi watabeba na watakuwa na uwezo wa kufanya kazi hii kwa weledi katika misheni za ulinzi wa amani. “

Akazungumzia pia mfumo wa ulinzi wa amani katika zama za sasa akisema kwamba katika kuendesha kozi hii walizingatia mambo muhimu yafuatayo ili kuendana na changamoto kadhaa zilizopo.

“Mosi, utaona ushiriki wa kozi hii umewekwa katika uwiano ili kuwezesha ushirikiano kikanda na ushirikiano kimataifa ili kutoa fursa kwa nchi wanachama kuweza kutekeleza majukumu yake. Kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika ya kimataifa, lakini vile vile tumezingatia kuboresha ujuzi wa watendaji wa maafisa Wanadhimu wa Umoja wa Mataifa,” amesema Brigedia-Jenerali Itang’are.

Mafunzo yanaendana na changamoto za sasa

Tweet URL

Ameongeza kuwa wanajikita pia katika matumizi ya teknolojia mpya katika utendaji, hasa ikizingatiwa katika kipindi hiki ambapo Umoja wa Mataifa kwa ujumla uko katika mikakati ya kuboresha vituo vya ya ulinzi wa amani kuendana na na ukuaji wa teknolojia ili kurahisisha utendaji, upatikanaji wa taarifa katika ngazi zote kuanzia makao makuu ya Umoja wa Mataifa, makao makuu ya misheni, makao makuu ya sekta pamoja na vikundi mbalimbali na kushiriki katika ulinzi wa amani.

Sababu ya kuichagua Tanzania

Kwa upande wake, Mkuu wa Huduma za Mafunzo Umoja wa  Mataifa ameelezea furaha yake ya kuona mafunzo hayo ya wakufunzi kwa mara ya kwanza yanafanyika barani Afrika, hususan nchini Tanzania.

“Mafunzo haya yatawawezesha wakufunzi hawa kurudi nchi zao na kufundisha maafisa wengine ambao wataweza kutumwa kwenye misheni za UN mashinani kama wafanyakazi, hivyo wanaweza kuendesha kozi hizi kitaifa. Pia wanaweza kushiriki kuendesha kozi kama hizi kimataifa, hivyo kujenga uwezo mkubwa kwa ajili ya kutumwa kwenye misheni za mashinan,” amesema Bwana Sood.

Alipoulizwa kwa nini wameamua kuendeshea mafunzo hayo nchini Tanzania, Sood amesema, “Nafikiri Tanzania imekuwa na historia ndefu ya kushiriki kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kuzuia migogoro na kudumisha amani. Ni nchi nzuri na yenye utulivu. Nafikiri inatoa fursa si kwa nchi jirani tu na Tanzania bali pia. Kama umeona kumekuwa na wataalamu wa mafunzo hapa ambao ni sehemu ya kozi hii ambao wametoka mbali kama Vietnam.”

Na hatimaye akasema, “tunatarajia Tanzania itaendelea kusaidia shughuli za kudumisha amani za Umoja wa Mataifa pia na sisi kama Umoja wa Mataifa. Kila mara tunataka dunia iungane ili tuwe na amani na usalama endelevu mbele. Licha ya migogoro inayojitokeza hivi sasa.”

 
 
Imeandaliwa na Kapteni Mwijage Inyoma kutoka TPTC