Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen: Hali ya Kibinadamu yazidi kuwa mbaya

Watu katika wilaya ya Aslam magharibi mwa Yemen wanakusanya chakula katika kituo cha WFP cha usambazaji wa chakula.
© WFP/Riad Al-Qadmi
Watu katika wilaya ya Aslam magharibi mwa Yemen wanakusanya chakula katika kituo cha WFP cha usambazaji wa chakula.

Yemen: Hali ya Kibinadamu yazidi kuwa mbaya

Msaada wa Kibinadamu

Yemen inaendelea kuwa hatarini kuvutwa zaidi katika mizozo ya kikanda huku mamilioni ya watu wakiendelea kukumbwa na njaa, wametahadharisha Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Hans Grundberg, na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA, Tom Fletcher, katika kikao cha Baraza la Usalama leo Jumatano, Julai 9.

Grundberg amesema hali katika eneo hilo bado ni tete sana. Ameelezea wasiwasi kuhusu mashambulizi ya roketi ya Houthi dhidi ya Israel na mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya meli mbili za kibiashara katika Bahari Shamu, yaliyosababisha vifo vya raia na madhara yanayowezekana kwa mazingira. Mashambulizi hayo, ambayo ni ya kwanza kwa muda wa miezi saba, yalipelekea mashambulizi ya kisasi kutoka Israel.

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Hans Grundberg (kwenye skrini) akitoa taarifa kwa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Yemen.
UN Photo/Loey Felipe
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Hans Grundberg (kwenye skrini) akitoa taarifa kwa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Yemen.

Hali ya kutoaminika

"Uhuru wa kusafiri katika Bahari ya Shamu lazima ulindwe, na miundombinu ya raia haipaswi kulengwa na pande zinazohusika katika mzozo," Grundberg amesisitiza. Ameongeza: "Yemen haipaswi kuvutwa zaidi katika migogoro ya kikanda inayotishia kuharibu zaidi hali ya nchi ambayo tayari ni dhaifu kupita kiasi; kuna mengi yaliyomo hatarini, na mustakabali wa Yemen unategemea dhamira yetu ya pamoja kuiepusha na mateso zaidi na kuirudishia matumaini na heshima watu wake."

Mjumbe huyo maalum ameeleza kuwa hali ndani ya nchi bado ni ya kutotulia. Aliripoti kuwepo kwa shughuli za kijeshi zinazoendelea katika maeneo kadhaa. Kwa mujibu wake, ni mchakato wa kidiplomasia na mazungumzo pekee, licha ya changamoto, vinavyoweza kuleta matumaini ya suluhisho endelevu.

Ameeleza pia kuhusu kuzorota kwa hali ya kiuchumi nchini Yemen, pamoja na tishio la baa kamili ya njaa. Kwa kumalizia, Grundberg ameeleza vipaumbele vitatu: kupunguza mvutano wa mzozo, kuanzisha mazungumzo kati ya pande husika, na kutoa dhamana muhimu za kiusalama. Pia almesisitiza umuhimu wa kulinda na kupanua nafasi ya asasi za kiraia, na kurudia wito wake wa kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa wafanyakazi wote wa Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wanadiplomasia waliokamatwa kiholela.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu, Tom Fletcher akitoa taarifa kwa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Yemen.
UN Photo/Loey Felipe
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu, Tom Fletcher akitoa taarifa kwa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Yemen.

Ukosefu wa ufadhili

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu, Tom Fletcher, ameonya juu ya kuzorota kwa hali ya chakula nchini humo. Kwa mujibu wake, zaidi ya watu milioni 17 nchini Yemen wanakumbwa na njaa, na kufikia Septemba idadi hiyo inaweza kuzidi milioni 18. Zaidi ya watoto milioni moja walio na umri wa chini ya miaka mitano wanakabiliwa na utapiamlo mkali na hatari kwa maisha. "Hatujawahi kushuhudia kiwango hiki cha mahitaji tangu usitishaji mapigano uliowekwa na Umoja wa Mataifa mapema mwaka 2022," amesema Fletcher.

Ameongeza kuwa ufadhili wa misaada ya kibinadamu unapungua kwa kasi, hasa katika maeneo ya afya na ulinzi, ikiwemo kwa wanawake na wasichana milioni 6.2 walio katika hatari ya ukatili wa kijinsia.

Hata hivyo, licha ya rasilimali chache, wafanyakazi wa misaada wanaendelea kuwafikia watu walio hatarini zaidi nchini Yemen, Fletcher amesema. Mbinu mpya kupitia kile kinachoitwa "marekebisho ya misaada ya kibinadamu" imeleta mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa visa vya kipindupindu kwa zaidi ya asilimia 70 ikilinganishwa na mwaka jana. Mikakati mipya imehakikisha zaidi ya watoto 650,000 walio katika hatari kubwa ya utapiamlo wanapata matibabu madhubuti, na vituo vya afya 3,200 vinaendelea kuhudumia watu milioni 7.2.

Mratibu huyo wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa Baraza la Usalama kuongeza ufadhili kwa misaada ya chakula na kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha sheria za kimataifa za kibinadamu zinazingatiwa. Pia amesisitiza umuhimu wa juhudi za kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wawakilishi wa asasi za kiraia waliokamatwa.