Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maafa ya mafuriko ya ghafla Texas yafichua hatari na changamoto za tahadhari

Mafuriko makubwa yamesababisha uharibifu mkubwa katikati mwa Texas nchini Marekani.
© World Central Kitchen (WCK)
Mafuriko makubwa yamesababisha uharibifu mkubwa katikati mwa Texas nchini Marekani.

Maafa ya mafuriko ya ghafla Texas yafichua hatari na changamoto za tahadhari

Tabianchi na mazingira

Mafuriko makubwa ya ghafla yaliyokumba  eneo la Kati mwa  jimbo la Texas, nchini Marekani, baada ya mvua kubwa kunyesha ndani ya saa chache tu, yameonesha hatari kubwa ya janga la mafuriko na changamoto zilizopo katika kuhakikisha maonyo ya mapema yanawafikia walengwa kwa wakati.

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa, WMO limesema kupitia taarifa  yake iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi kwamba mafuriko hayo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 100, huku wengine kadhaa wakiwa bado hawajulikani walipo.

“Inasikitisha kwamba wengi wa waliopoteza maisha  ni watoto wadogo waliokuwa katika kambi ya mapumziko ya majira ya joto,” imesema WMO huku ikituma salamu za rambirambi kwa wote waliodhurika na janga hilo.

Janga hili limetokea katika eneo la milima la Kati mwa jimbo la Texas,  hasa katika Kaunti ya Kerr. WMO inasema mvua kubwa ilianza usiku wa Julai 3 kuamkia Julai 4, 2025, na kusababisha kiwango cha maji cha mto Guadalupe kuongezeka kwa kasi ya kutisha, kiasi cha mita 8 ndani ya dakika 45 tu, majira ya saa 4 asubuhi.  Mafuriko yaliendelea hadi Julai 7, 2025.

Maonyo yalitolewa lakini watu walikuwa wamelala

Ofisi ya Marekani ya Masuala ya Hali  ya Hewa, ilitoa saa 12 kabla ya mafuriko ilitoa onyo la mapema juu mafuriko ya ghafla , na baadaye saa tatu kabla ya mafuriko makubwa, tangazo la watu kuchukua tahadhari lilitolewa kupitia Radio ya Hali ya Hewa, mifumo ya usimamizi wa dharura, na vyombo vya habari zikiwemo Redio na Televisheni.

WMO inasema hata hivyo, changamoto kubwa ilikuwa kwamba maonyo ya mwisho yalitolewa wakati watu wengi wakiwa wamelala usingizi mzito, na maeneo ya kambi za mapumziko ya majira ya joto hayakuwa na ving'ora vya tahadhari. “Hii ilipunguza ufanisi wa maonyo hayo katika kuwafikia watu kwa wakati muafaka wa kujiokoa,” imesema WMO.

Shirika hilo linasema mafuriko ya ghafla ni miongoni mwa majanga hatari zaidi duniani, yakisababisha vifo zaidi ya 5,000 kila mwaka na kuathiri vibaya miundombinu na jamii, hasa katika maeneo ya mijini na milima. Huchangia takribani asilimia 85 ya vifo vyote vinavyohusiana na mafuriko.

WMO inafanya nini?

WMO husaidia nchi kutabiri mafuriko ya ghafla kupitia Mfumo wa Mwongozo wa Mafuriko ya Ghafla (FFGS), ambalo ni jukwaa la utabiri wa wakati halisi na maonyo ya mapema linalotumika katika zaidi ya nchi 70.

Mfumo huu huunganisha data za mvua kutoka satelaiti na rada, pamoja na mifumo ya utabiri wa hali ya hewa ya hali ya juu, ili kusaidia watabiri kutambua vitisho vya mafuriko ya ghafla. Pia WMO inajenga uwezo wa kitaifa na kuratibu juhudi kati ya taasisi za utabiri na wasimamizi wa majanga.