Ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa yaangazia usongeshaji SDGs Gambia
Ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa yaangazia usongeshaji SDGs Gambia
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed akiwa ziarani barani Afrika ambapo juzi tarehe 7 aliingia nchini Gambia, kwa njia ya mtandao wa X ameonesha namna ziara yake ilivyokuwa ya mafanikio kwa kukutana na viongozi na wadau mbalimbali nchini humo katika harakati za kufanikisha Malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu.
Japo kwa muda mfupi nchini Gambia, ziara imekuwa ya mafanikio kwani ndani ya muda huo mfupi, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed mara tu baada ya kupokelewa na Waziri wa mambo ya nje wa Gambia na baadaye wakawa na mazungumzo kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (#SDGs) na vipaumbele vya pamoja vya dunia, kwa kuzingatia kaulimbiu ya Kutomwacha Mtu Yeyote Nyuma Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alienda moja kwa moja kukutana na Rais wa nchi hiyo Adama Barrow na mazungumzo yao yakajikita katika vipaumbele vya maendeleo endelevu, kuimarisha amani, na maono ya pamoja ya maendeleo endelevu.
Pia alipata wasaa wa kukutana na Waziri wa Fedha wa Gambia na wawili hao walijadili kufungua njia mpya za kufadhili #SDG, ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa rasilimali za ndani na kutumia msaada wa kimataifa kwa ajili ya ukuaji jumuishi.
Vilevile alifanya mazungumzo na washirika wa maendeleo kuhusu kuimarisha ushirikiano, kutumia rasilimali kwa ufanisi, na kutoa matokeo ya mabadiliko chanya kwa watu na sayari akisisitiza kwamba, “hakuna anayeweza kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs akiwa peke yake.”
Aidha Naibu Katibu Mkuu AminaJ Mohammed, alitembelea Kituo cha Uzalishaji na Ubunifu cha Bakoteh, ambacho kinawawezesha vijana kujikwamua kiuchumi kwa kufanya kazi za kibunifu kama ufumaji na kushona nguo.
Kwa maneno yake Bi. Mohammed anaandika kwamba, “kwa kuwawezesha wanawake na vijana kupitia ujuzi, Gambia inaharakisha maendeleo katika kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu (#SDGs).”
Baada ya ziara hiyo nchini Gambia, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alielekea Cameroon ambako mapema leo amefungua mkutano wa kimataifa kuhusu Uchumi wa buluu kwenye ghuba ya Guinea.