Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Angalau kila mtu awe na anwani ya barua pepe: Mshiriki WSIS

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Viongozi kuhusu Upashanaji wa Taarifa duniani, (WSIS) unaendelea huko Geneva.
© ITU/Pierre Albouy Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Viongozi kuhusu Upashanaji wa Taarifa duniani, (WSIS) unaendelea huko Geneva.

Angalau kila mtu awe na anwani ya barua pepe: Mshiriki WSIS

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Viongozi kuhusu Upashanaji wa Taarifa duniani, (WSIS) ukiingia siku ya 3 hii leo huko Geneva, Uswisi, washiriki wanapazia sauti umuhimu wa kila mtu kokote pale aliko afikiwe na teknolojia inayomwezesha kupokea taarifa kwa urahisi, usahihi na kwa haraka.

Tweet URL

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano, ITU, mwenyeji mwenza wa mkutano huu, licha ya miongo ya maendeleo, bado watu bilioni 2.6 hawana huduma za mtandaoni, ikimaanisha ukosefu wa usawa kwenye stadi za kidijitali na hawana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika jamii za kidijitali.

Akizungumzia hoja hiyo, George Thembo, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mawasiliano nchini Uganda ambaye ni miongoni mwa washiriki wa mkutano huu na anasema “Kwa upande wa kutoa ujuzi wa kidijitali, tunajitahidi kuhakikisha tunawafikia watu walioko katika maeneo yasiyohudumiwa ipasavyo ili kuwapatia ujuzi wa msingi wa kidijitali — angalau kuhakikisha kwamba kila mmoja wao ana anwani ya barua pepe. Hili ni jambo la msingi kabisa, kwa sababu bila barua pepe huwezi kulinda muamala wowote wa kidijitali.”

Kwa Hiqmat Sungdeema Saani, mwanarakati wa haki za wanawake nchini Ghana, ushiriki wake kwenye mkutano huu ni fursa tosha kwani, “Hii ni fursa kwangu kuleta sauti za wanawake na vijana kutoka maeneo yaliyo pembezoni ili kuhakikisha kuwa sauti zao zinaakisiwa katika majadiliano, na ingawa huenda nisiweze kuzungumza katika vikao vya ngazi ya juu kabisa, bado ni fursa ya kujifunza mbinu bora.”

Mkutano huu unaomalizika Julai 11, umeandaliwa kwa pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Mpango wa Maendeleo (UNDP)  na Maendeleo na Biashara (UNCTAD) huku wenyeji wenza ni shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano, ITU na shirikisho la Uswisi.