Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa UNFPA wa michezo na elimu warejesha tabasamu la matumaini kwa vijana wakimbizi wa DRC nchini Burundi

Mradi wa UNFPA wa michezo na elimu warejesha tabasamu la matumaini kwa vijana wakimbizi wa DRC nchini Burundi.
© UNFPA
Mradi wa UNFPA wa michezo na elimu warejesha tabasamu la matumaini kwa vijana wakimbizi wa DRC nchini Burundi.

Mradi wa UNFPA wa michezo na elimu warejesha tabasamu la matumaini kwa vijana wakimbizi wa DRC nchini Burundi

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), kwa kushirikiana na serikali ya Burundi, limekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia vijana wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), walioko kwenye kambi ya Musenyi, mkoani Rutana huko Burundi. Kupitia michezo, tamaduni, na shughuli za elimu ya afya ya uzazi, vijana hawa wamepata matumaini mapya na fursa ya kujenga maisha yao upya. 

Mradi huu unaangazia umuhimu wa kuwekeza kwa vijana walioko katika mazingira magumu ili kuwasaidia kufikia ndoto zao.

Video inaanza kwa mandhari ya kambi ya Musenyi, iliyoko mkoani Rutana, kusini mashariki mwa Burundi kisha inaonesha watototo wakishiriki michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa kabumbu. Pembeni mwa uwanja, vijana wengine wameketi wakisikiliza kwa makini mafunzo kutoka kwa wawakilishi wa UNFPA na wakufunzi wa kijamii.  

Katika uwanja wa mpira wa miguu, michezo si burudani tu, bali ni darasa la maisha. Vijana wanajifunza kuhusu afya ya uzazi, kujitambua, kujikinga dhidi ya mimba za mapema, na ukatili wa kijinsia. Georges Gahungu – Afisa wa vijana anayehusika na miradi ya UNFPA Burundi ya  kupambana na  Virusi Vya Ukimwi, VVU anasema,

"Mara ya kwanza tulipokutana na wakimbizi hawa kutoka DRC ilikuwa huko Cibitoke  (tamka Chibitoke)– hali yao ilikuwa ya kusikitisha. Lakini sasa, katika kambi ya Musenyi, hali imebadilika kabisa. Unaweza kuona kwenye nyuso zao kwamba wameanza kufurahia maisha. Shughuli tunazofanya zinawalenga vijana wa umri wa miaka 10 hadi 19, wavulana na wasichana, tukitumia michezo, tamaduni na elimu ya afya kuibua uelewa."

Kwa Sheilla mwenye umri wa miaka 15, mpira wa miguu umekuwa tiba ya kiakili. Anasema "UNFPA imenisaidia sana. Ndoto yangu ilianza kufufuka tena. Mpira ulileta furaha moyoni mwangu na kunisaidia kusahau machungu niliyopitia."

Naye Angeligue mkimbizi mwenye umri wa miaka 17 anasema "Kupitia UNFPA, nilisikia furaha sana mimi na wenzangu tulipokuwa tunacheza. Michezo ni ya kufurahisha na yenye mafunzo. Ningependa kuendelea kucheza kabumbu na kucheza na watoto kwa sababu ni ya maana sana."

Mradi wa UNFPA wa michezo na elimu warejesha tabasamu la matumaini kwa vijana wakimbizi wa DRC nchini Burundi.
© UNFPA
Mradi wa UNFPA wa michezo na elimu warejesha tabasamu la matumaini kwa vijana wakimbizi wa DRC nchini Burundi.

Kutoka katika mafunzo haya Rosette mwenye umri wa miaka 14 amepata kujua namna ya kujilinda, kuepuka vishawishi ili kuondokana  na mimba za utotoni . 

UNFPA walitupa elimu bora, wakatufundisha sisi wasichana mambo mengi ya kutujenga.  Tunashukuru sana UNFPA  kwa kutuletea michezo na taulo za kike.

Pia, kwa vijana wa kiume kama Glorie, mafunzo haya ni dira.

"kipindi hiki kilinisaidia kuelewa zaidi kuhusu mwili wangu wakati wa balehe .Wakati huu kuna mabadiliko ya sauti, misuli, mwili. Haya yote yalinifundisha jinsi ya kujilinda na kuishi na wasichana ili kuepuka mimba."

Georges Gahungu anasisitiza kuwa mahitaji bado ni makubwa. Anatoa wito kwa wahisani waweze kuingilia kati na kutoa msaada kwa wakimbizi hao akisema "Katika afya ya uzazi na kuzuia ukatili wa kijinsia, mahitaji ni makubwa sana, hasa kwa vijana. Tunatoa wito kwa watu binafsi na mashirika kusaidia. Tunahitaji rasilimali nyingi kukidhi mahitaji ya hawa vijana, pamoja na wanawake wajawazito walioko kambini."