Mkutano wa UN wamulika ‘tamu na chungu’ za Akili Mnemba
Mkutano wa UN wamulika ‘tamu na chungu’ za Akili Mnemba
Jukwaa kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu akili mnemba, (AI) limefunguliwa mjini Geneva siku ya Jumanne, likijikita katika mazungumzo ya ngazi ya juu kwa siku nne, maonesho ya teknolojia ya hali ya juu, na miito ya dharura ya kuweka mifumo jumuishi ya usimamizi wa AI.
Tukio hili linakuja wakati ambapo mifumo ya kiotomatiki na ile inayozalisha maudhui inakua kwa kasi kuliko kanuni na sheria zinavyoweza kuendana nayo.
Ukibeba maudhui, “AI kwa maslahi bora” mkutano unawakutanisha serikali, viongozi wa teknolojia, wasomi, mashirika ya kiraia na vijana ili kuchunguza jinsi AI inaweza kuelekezwa katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) – na kuondokana na hatari zinazoendelea kama vile ongezeko la ukosefu wa usawa, upotoshaji wa taarifa, na madhara kwa mazingira.
"Sisi ni kizazi cha AI," amesema katika hotuba ya ufunguzi, Doreen Bogdan-Martin, Katibu Mkuu wa shirika la Umoja wa Kimataifa la Mawasiliano (ITU) – shirika mahsusi la UN kuhusu teknolojia ya habari na mawasiliano .
Lakini kuwa sehemu ya kizazi hiki haimaanishi tu kutumia teknolojia hizi, akisema, "inamaanisha kuchangia jitihada za kuinua ujuzi kwa jamii nzima, kuanzia shule za awali hadi kujifunza kwa maisha yote.”.
Onyo kuhusu hatari za AI
Bi. Bogdan-Martin ameonya juu ya hatari zinazoongezeka za kutumia AI bila uelewa wa kutosha wa umma au usimamizi wa kisera.
"Hatari kubwa tunayokabiliana nayo si AI kufuta binadamu duniani. Ni mbio za kuingiza AI kila mahali bila kuelewa vya kutosha maana yake kwa watu na sayari yetu," amesema.
Kauli yake inaakisi hali ya dharura inayozidi kuongezeka miongoni mwa watunga sera na wataalamu wa teknolojia, hasa wakati mifumo mipya ya AI yenye uwezo wa kufanya maamuzi na kuchukua hatua kwa uhuru inapoendelea kuibuka kwa kasi isiyowahi kushuhudiwa.
Wakati baadhi ya wataalamu wakitabiri kufikiwa kwa AI yenye uwezo sawa na binadamu ndani ya miaka mitatu ijayo, hofu kuhusu usalama, upendeleo, matumizi ya nishati, na uwezo wa udhibiti imeongezeka.
Maonesho ya teknolojia na mvutano ulioko
Ajenda ya mkutano inaonesha mvutano huu.
Zaidi ya mita za mraba 20,000 katika ukumbi wa Palexpo mjini Geneva zinatumika kwa zaidi ya maonesho 200, yakiwemo gari linaloruka, kifaa cha kuchunguza ubora wa maji chenye muundo wa samaki, miingiliano ya ubongo na kompyuta, na zana za kukabiliana na majanga, vyote vikiendeshwa kwa AI.
Warsha zitakazofanyika wiki nzima zitashughulikia mada kama AI katika afya na elimu, maadili, ujumuishaji wa kijinsia, na utawala wa kimataifa.
Mojawapo ya mambo muhimu ni Siku ya Usimamizi wa AI siku ya Alhamisi, ambapo wasimamizi wa kitaifa na mashirika ya kimataifa watajadili pengo lililopo katika usimamizi wa kimataifa.
Utafiti wa ITU umeonesha kuwa asilimia 85 ya nchi hazina sera au mkakati mahsusi kuhusu AI, jambo linalozua hofu kuhusu maendeleo yasiyo sawa na pengo linalozidi kuongezeka la kidijitali.
Kipaumbele kwa afya
Afya ni mada kuu mwaka huu ambapo siku ya Jumatano, Shirika la Afya Duniani (WHO) litaongoza kikao kinachoitwa “Kuwezesha AI kwa Ubunifu na Upatikanaji wa Huduma za Afya”, kikileta pamoja wataalamu wa teknolojia, wasimamizi, madaktari na viongozi wa kibinadamu ili kujadili jinsi AI inavyoweza kuboresha utoaji wa huduma za afya – hasa katika maeneo yenye rasilimali chache.
Matumizi halisi ya AI – kuanzia uchunguzi wa haraka katika huduma za dharura hadi zana za uchunguzi kwa kliniki za vijijini – yataangaziwa, pamoja na kuonesha muhtasari wa Mwongozo wa WHO kuhusu AI katika Tiba Asilia, unaotarajiwa kuzinduliwa rasmi jukwaani.
Wataalamu pia watachunguza changamoto za muingiliano wa mifumo, usawazishaji wa udhibiti wa kimataifa, na haki miliki katika makutano ya AI na afya ya kimataifa.
Mkutano pia utatoa Tuzo za AI kwa Maslahi Bora, kutambua miradi bunifu inayotumia AI kwa manufaa ya umma, zikiwa katika vipengele vya watu, sayari na ustawi.
Jukwaa la kuchochea hatua
Mwelekeo wa afya unaakisi lengo kuu la mkutano: kuhakikisha AI inahudumia manufaa ya jamii, hasa katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.
Vikundi vya roboti vinavyoongozwa na vijana kutoka jamii zilizo pembezoni vitawasilisha suluhisho za kurejesha hali baada ya majanga na usimamizi wa taka, huku kampuni changa zikishindana katika Kiwanda cha Ubunifu kuonesha zana za AI kwa elimu na ustahimilivu wa hali ya hewa.
Teknolojia za roboti kulima shambani
Maonesho ya moja kwa moja ni pamoja na roboti ya shambani inayofanya kazi peke yake, choo cha kujisafisha chenyewe, na mfumo wa ndge isiyo na rubani ya kuchambua vijinasaba au drone-eDNA kwa ufuatiliaji wa viumbe hai na wadudu kwa kiwango kikubwa.
Akihitimisha hotuba yake, Bi. Bogdan-Martin amewakumbusha washiriki kuwa mustakabali wa AI ni jukumu la pamoja.
"Tusiache kamwe kuiweka AI iwe kwa ajili ya watu wote na sayari yetu," amesema.