Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa haki na chaguo katika afya ya uzazi unadhoofisha kizazi cha vijana DRC

Ombeni Mburano, ambaye ana ujauzito wa miezi saba na mtoto wake wa sita, amesimama mbele ya magofu ya makazi ya muda iliyolipuliwa na bomu katika eneo lisilo rasmi la watu waliokimbia makazi yao magharibi mwa Goma, DR Congo.
© UNFPA/Jonas Yunus
Ombeni Mburano, ambaye ana ujauzito wa miezi saba na mtoto wake wa sita, amesimama mbele ya magofu ya makazi ya muda iliyolipuliwa na bomu katika eneo lisilo rasmi la watu waliokimbia makazi yao magharibi mwa Goma, DR Congo.

Ukosefu wa haki na chaguo katika afya ya uzazi unadhoofisha kizazi cha vijana DRC

Wahamiaji na Wakimbizi

Ndoto ya Ombeni Mburano, mwenye umri wa miaka 31, ya kuwa na watoto watatu imevunjika “Nilitaka kuwa na watoto watatu. Tayari nina 5, na wa sita anakuja hivi karibuni. Sijawahi kuwa na uhuru wa kuchagua.” ameambia Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi UNFPA.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya UNFPA ya Hali ya Idadi ya Watu Duniani, asilimia 44 ya wanawake na wasichana duniani hawana mamlaka ya kufanya maamuzi kuhusu uhusiano wa kimapenzi, matumizi ya vifaa vya mpango wa uzazi au huduma za afya ya uzazi. Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hali hii ni mbaya zaidi –ikiifikia asilimia 69.

“Nchini kwetu, si kila wakati wewe huamua kama unataka mtoto au la. Wakati mwingine ni familia yako, mume wako... au tu hali ya maisha” Ombeni anaeleza.

Utafiti uliofanywa kwa ajili ya ripoti hiyo pia ulibaini kuwa takriban mtu 1 kati ya 3 amewahi kupata ujauzito usiopangwa. Takwimu hizi ni za kusikitisha hasa nchini DRC, nchi iliyo na kiwango cha juu cha uzazi duniani. Umaskini, ukatili wa kingono, ndoa za utotoni, vita na ukosefu wa huduma za afya ya uzazi huondoa uwezo wa wanawake kupanga kwa uhuru kama na lini watapata watoto.

Ombeni, mume wake, na watoto wao wakiwa nje ya makazi yao ya muda katika eneo la watu waliohama magharibi mwa Goma baada ya kukimbia ghasia.
© UNFPA/Jonas Yunus
Ombeni, mume wake, na watoto wao wakiwa nje ya makazi yao ya muda katika eneo la watu waliohama magharibi mwa Goma baada ya kukimbia ghasia.

Huko Goma, mkunga Espérance ameeleza kuwa wanawake wengi vijana wanataka kuchelewa kupata mtoto, lakini hawana njia za kujilinda wala uwezo wa kusema hapana. Upatikanaji mdogo wa taarifa na huduma za uzazi wa mpango unawazuia kupanga familia zao. Takwimu za 2023-2024 zinaonesha kuwa mwanamke 1 kati ya 5  nchini DRC anataka kuchelewesha au kuepuka ujauzito lakini hawawezi kupata vifaa vya kupanga uzazi. Hali hii imesababisha kiwango cha juu cha watoto kuzaliwa kwa wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 19.

Maisha yaliyoingiliwa na kuvurugika, familia zinahangaika

Esther, msichana mdogo aliyehamishwa kutoka Rutshuru, Kivu Kaskazini, ana umri wa miaka 18 tu – na ni mjamzito wa miezi 7. Yeye wala mpenzi wake Samuel, mwenye umri wa miaka 25, hawakuwa na maarifa kuhusu afya ya uzazi au mpango wa uzazi. Esther alipata ujauzito muda mfupi baada ya kuanza uhusiano na Samuel.

Bila msaada wowote wa kifedha, Esther alilazimika kuhamia kwa mama wa Samuel, Thérèse. Lakini huyu si mjukuu wake wa kwanza.

Miaka iliyopita, mpenzi wa kwanza wa Samuel alipata mimba, lakini Samuel aliogopa na kuamua kukimbia – hakuwahi kusikia tena kutoka kwa msichana huyo. Dada yake pia alipata mtoto  na baba wa mtoto huyo pia aliacha familia hiyo.

Thérèse, mwenye umri wa miaka 62, anajitahidi kulea watoto wake na wajukuu kupitia biashara ndogo ya mboga. Na sasa, mjukuu mwingine anakuja.

Samuel hufanya  kazi za hapa na pale, akitafuta njia ya kujipatia riziki. Hali yake si ya kipekee. zaidi ya asilimia 60 ya vijana chini ya miaka 30 nchini humo hawana ajira rasmi. Wengi hufanya kazi katika sekta isiyo rasmi, bila mikataba, bila ulinzi wa kijamii, na bila matumaini ya kupata maendeleo – hali inayotia wasiwasi kwa wazazi wachanga.

Samuel anasema “Esther alipopata ujauzito, sikuwa na nyumba, kazi wala mipango. Mama yangu alilazimika kumpokea, kama alivyofanya kwa dada yangu. Ninajihisi nimekwama, ninalazimika kubeba jukumu bila kuwa tayari.”

Kuwawezesha vijana kuchagua na kuwa na familia wanazotamani

Thérèse amembeba mjukuu wake kwenye ua la nyumba ya familia huko Goma. Kwa kutarajia mjukuu mwingine hivi karibuni, Thérèse ana wasiwasi jinsi atakavyosimamia kutunza familia.
© UNFPA
Thérèse amembeba mjukuu wake kwenye ua la nyumba ya familia huko Goma. Kwa kutarajia mjukuu mwingine hivi karibuni, Thérèse ana wasiwasi jinsi atakavyosimamia kutunza familia.

Uwekezaji kwa vijana, ustawi wao na uwezo wa kufanya maamuzi ni muhimu ili kuwawezesha kupanga familia kwa hiari.

“Kupata mtoto ni uamuzi wa pamoja na wa kufahamu, si jambo la kufanyiwa bila hiari,” anasema Dkt. Solange N. Ngane, mratibu wa mpango wa afya ya uzazi wa UNFPA huko Goma.

Mashariki mwa nchi, ambapo mizozo inaendelea na kusababisha uharibifu mkubwa wa vituo vya afya na watu kuhama makazi, UNFPA inaimarisha upatikanaji wa vifaa va kupanga uzazi na huduma za afya ya uzazi. Timu za wahudumu wa afya ya jamii na washauri rika wa vijana wanaofadhiliwa na UNFPA wanafikia watu waliopoteza makazi kwa kuwapatia vifaa vya kupanga uzazi, kampeni za uelimishaji kuhusu afya ya uzazi, na kuwapeleka kwenye vituo vya afya vinavyotoa huduma hizo. UNFPA pia inasambaza vifaa vya afya ya uzazi kwenye vituo vya afya na imetuma wakunga 148 kuhakikisha kuwa huduma za afya ya uzazi zinapatikana kwa wanawake waliokimbia makazi yao, waliorejea, na jamii zinazowapokea.

Kituo kimoja ni cha afya cha Buhimba, ambako Esther na Samuel walihudhuria kliniki ya wajawazito. Wakiwa na wanandoa wengine, walipata elimu kutoka kwa mkunga na msaidizi wa kisaikolojia. Huduma hizi ni bure kwa wanawake waliopoteza makazi kama Esther.

Katika kituo cha afya cha Buhimba, Samuel anaambatana na Esther, 18, kwa mashauriano yake ya tatu ya ujauzito, ambapo pia walipata taarifa za afya ya uzazi kutoka kwa mkunga wa UNFPA.
© UNFPA/Jonas Yunus
Katika kituo cha afya cha Buhimba, Samuel anaambatana na Esther, 18, kwa mashauriano yake ya tatu ya ujauzito, ambapo pia walipata taarifa za afya ya uzazi kutoka kwa mkunga wa UNFPA.

“Tulijifunza jinsi ya kutambua dalili hatarishi kwa wanawake wajawazito, na pia kuhusu njia za kupanga uzazi tutakazoweza kutumia baada ya kujifungua. Sikujua kama tungepokelewa vizuri hivi, hata bila pesa. Sasa najihisi salama, na Samuel pia anaelewa kuwa tunaweza kuamua pamoja,” anasema Esther.

Msaada unahitajika ili vijana wachague mustakabali wao

Programu kama ile ya kituo cha Buhimba hufadhiliwa na Umoja wa Ulaya, Japani, Norway, Uswidi na Uingereza.

Lakini mahitaji makubwa yanazidi rasilimali zilizopo: katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, ni asilimia 7 tu ya watu waliolengwa kupata huduma za afya ya uzazi kupitia mpango wa mahitaji ya kibinadamu na majibu walioweza kufikiwa. Hali hii imekuwa mbaya zaidi baada ya Marekani kujiondoa katika kutoa msaada, hatua iliyopunguza zaidi ya nusu ya ufadhili wa afya ya uzazi nchini.

Takwimu za UNFPA zinaonesha kuwa hali hiyo imesababisha ongezeko la ujauzito usiokusudiwa, utoaji mimba usio salama, maambukizi ya magonjwa ya zinaa, na vifo vya akina mama na watoto – jambo linaloonesha kuwa waathirika wakuu kila mara ni wale walioko katika mazingira magumu zaidi.

“Msichana anapopata ujauzito bila kutarajia, maisha yake hubadilika kabisa,” amesema Dkt. Ngane. “Kuwekeza kwa vijana kunamaanisha kuwapa uwezo wa kuamua kwa uhuru kama wanataka kuwa wazazi, lini, na katika hali gani. Hiyo ndiyo haki ya kweli ya uzazi.”