Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN atoa wito kwa BRICS kuongoza kukabili mabadiliko ya tabianchi, afya na mageuzi ya ufadhili

Viongozi wa dunia wakipiga picha ya pamoja katika Mkutano wa 17 wa BRICS huko Rio de Janeiro, Brazil, mwaka wa 2025.
United Nations/Ana Carolina Fernandes Viongozi wa kimataifa wanaonesha mshikamano wao katika mkutano wa BRICS nchini Brazil.

Katibu Mkuu wa UN atoa wito kwa BRICS kuongoza kukabili mabadiliko ya tabianchi, afya na mageuzi ya ufadhili

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito mzito kwa viongozi wa dunia katika Mkutano  wa BRICS unaofanyika nchini Brazil, akihimiza kuchukuliwa kwa hatua za haraka na za pamoja katika kukabiliana na mizozo inayohusiana ya mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira, na afya ya umma.

BRICS ni kifupi cha kiingereza cha wanachama waasisi wa kundi hilo ambazo ni  Brazil, Urusi, China na Afrika Kusini, ambapo sasa wamefikia 11 wakiwemo wanachama wapya Saudi Arabia, Misri, Ethiopia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Iran na Indonesia, huku washirika wapya ni Belarus, Bolivia, Kazakhstan, Thailand, Cuba, Malaysia, Nigeria, Vietnam, Uganda na Uzbekistan.

Akizungumza katika kikao kilichojadili “Mazingira, COP30 na Afya ya Kimataifa,” Guterres amesema dunia kwa sasa “inashambuliwa kutoka pande zote,” akitaja kuongezeka kwa uchafuzi wa mazingira, kupotea kwa bayonuai kwa kasi ya kutisha, na athari zinazoendelea za mabadiliko ya tabianchi.

“Joto kali linaua. Uchafuzi wa maji nao unaua,” ameonya, akieleza kuwa watu maskini na walio hatarini ndio wanaoathirika zaidi. Amesisitiza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi kwa afya ya binadamu ni mbaya sana na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti katika eneo la makutano kati ya mazingira na afya.

Amesifu nafasi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) na kueleza umuhimu wa kulisaidia zaidi, hasa kwa nchi zinazoendelea zinazokumbwa na changamoto za kiafya zinazochochewa na uharibifu wa mazingira.

Katibu Mkuu UN António Guterres akizungumza katika meza ya mkutano akiwa na bendera UMOJA WA MATAIFA na Shirika la Biashara Duniani, wakati wa Mkutano wa 17 wa BRICS huko Rio de Janeiro.
United Nations Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia katika Mkutano wa 17 wa wakuu wa nchi za BRICS mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Uharaka wa kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi na kuwekeza kwenye nishati safi

Kwa kuwa uzalishaji wa hewa ukaa unaendelea kuongezeka, Guterres amesema lengo la kuzuia joto kuongezeka zaidi ya nyuzi joto 1.5°C lipo “katika hali ya hatari,” na kusisitiza hitaji la “kupunguza kwa kiwango kikubwa uzalishaji kuanzia sasa.”

Amekumbusha kuhusu dhana ya “wajibu wa pamoja lakini tofauti” katika kukabili mabadiliko ya tabianchi, lakini akasisitiza kuwa kila nchi lazima ifanye juhudi za ziada.

“Nishati jadidifu tayari imekuwa chanzo cha bei nafuu na cha haraka zaidi cha umeme katika maeneo mengi duniani,” amesema. Pia ameeleza kuwa nishati safi inaweza kuboresha upatikanaji wa umeme kwa watu milioni 700 ambao bado hawajafikiwa na huduma hiyo, na kusaidia kupunguza vifo vinavyotokana na uchafuzi wa hewa ambao unaua watu milioni saba kila mwaka.

Amehimiza nchi za BRICS kuongoza katika kuimarisha miundombinu ya nishati safi, kupambana na ukosefu wa haki katika minyororo ya thamani ya madini muhimu, na kuhakikisha kuwa mataifa yanayoendelea yanapata manufaa ya rasilimali zao.

Maandalizi ya COP30 na hatua zaidi

Kuhusu Mkutano wa COP30 unaotarajiwa kufanyika nchini Brazil mwaka 2025, Guterres ametoa wito wa kupatikana kwa mkataba wa kisheria wa kukomesha uchafuzi unaotokana na plastiki mwaka huu, pamoja na mfumo wa kifedha madhubuti kwa ajili ya kulinda bayonuai, na mpango mpya wa kitaifa wa kupunguza hewa chafuzi (NDCs) kufikia Septemba.

“NDC hizo lazima zijumuishe uzalishaji wote wa hewa chafuzi, sekta zote za uchumi, ziendane na lengo la 1.5°C, na zihakikishe utekelezaji wa mabadiliko ya nishati yaliyoafikiwa katika COP28,” ameeleza.

Mvulana mdogo anakimbia kuelekea kwenye mwamba mkubwa wenye kidimbwi kidogo cha maji katika eneo kavu na tasa katika wilaya ya Ban Phai, mkoa wa Khon Kaen, Thailand.
© UNICEF/Roengrit Kongmuang Mvulana anacheza katika mandhari iliyoathiriwa na ukame kaskazini mashariki mwa Thailand.

Ufadhili na Haki ya Tabianchi

Katibu Mkuu amekosoa vikali hali ya sasa ya fedha za mabadiliko ya tabianchi, akitoa mfano unaogusa hisia kuonesha uzito mdogo unaowekwa kwenye mfuko wa fidia kwa hasara na uharibifu: “Mchango uliotolewa wakati wa uzinduzi wa mfuko huu ulilingana na mshahara wa mchezaji bora wa mpira wa kikapu nchini Marekani,” amesema na kuongeza, “lazima tuwe makini na makini zaidi kuhusu mfuko wa hasara na uharibifu.”

Ametoa wito kwa nchi zilizoendelea kutimiza ahadi zao, ikiwemo kutoa dola bilioni 40 kila mwaka kwa ajili ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi ifikapo mwaka 2025, kuhakikisha dola bilioni 300 kwa mwaka zinatolewa kwa nchi zinazoendelea ifikapo mwaka 2035, na kuchangisha dola trilioni 1.3 kila mwaka kupitia vyanzo vipya vya fedha na bei halisi ya hewa ukaa.

Mageuzi ya Mfumo wa Kifedha wa Dunia

Zaidi ya fedha za tabianchi, Guterres amesisitiza umuhimu wa mageuzi makubwa ya mfumo wa fedha wa kimataifa, likiwemo suala la msamaha wa madeni, ushirikiano wa Kusini kwa Kusini, na kuongezwa kwa mara tatu uwezo wa benki za maendeleo kwa manufaa ya nchi zinazoendelea.

Amehitimisha akisema, “huu ni wakati wa hatari kubwa lakini pia fursa kubwa. Naziomba nchi za BRICS kuwa nguzo ya mshikamano wa dunia kwa ajili ya watu, sayari na ustawi wa wote.”