Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jitihada za TEN/MET katika kuboresha elimu – Tanzania

Nasra Kibukila kutoka shirika la TEN/MeT nchini Tanzania.
UN News/Anold Kayanda Nasra Kibukila kutoka shirika la TEN/MeT nchini Tanzania.

Jitihada za TEN/MET katika kuboresha elimu – Tanzania

Na Sharon Jebichii - New York, Marekani
Utamaduni na Elimu

Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) umeendelea kuonesha dhamira thabiti ya kuhakikisha watoto wote wa kitanzania wanapata elimu bora, jumuishi na yenye usawa, kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali wa elimu ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na Sharon Jebichii wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani,  Mkurugenzi wa TEN/MET Nasra Kibukila ameeleza kuwa mtandao huo unaounganisha mashirika zaidi ya 245 yanayojishughulisha na masuala ya elimu nchini Tanzania, wanaendelea na azma yao kuhakikisha haki ya msingi ya elimu kwa kila mtoto.

Katika mahojiano hayo, ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kufanyika kwa mkutano wa CSW68, TEN/MET imefanikiwa kushiriki kikamilifu katika kusukuma ajenda ya kuwepo kwa bajeti ya elimu yenye mrengo wa kijinsia.

"Lengo letu ni kuona kwamba bajeti ya elimu sio tu inaongeza ugharamiaji wa elimu, bali pia inazingatia mahitaji ya kijinsia, hususan mazingira ya mtoto wa kike shuleni," alisema.

Changamoto katika usawa wa kijinsia shuleni

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa licha ya hatua zilizopigwa na serikali katika kugharamia elimu, bado Tanzania haijafikia kiwango cha asilimia 20 ya bajeti ya elimu kinachopendekezwa kimataifa.

Amesema pia kuwa upungufu wa walimu wa kike katika maeneo ya vijijini unachangia changamoto kwa watoto wa kike, hasa pale wanapohitaji msaada wa kijamii au wa kihisia kutoka kwa mtu wa jinsia yao.

"Tukimwangalia mwalimu kama mzazi wa pili, mtoto wa kike anakosa mtu wa kuzungumza naye iwapo hakuna mwalimu wa kike shuleni," amefafanua.

Mpango wa kurudisha wasichana waliokatiza masomo shuleni

Katika hatua nyingine, TEN/MET kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali wamefanikiwa kuandaa mpango wa kitaifa wa utekelezaji wa sera ya kuruhusu wanafunzi wa kike waliokatisha masomo ikiwemo kwa sababu ya ujauzito kurejea shuleni.

Mpango huo unaofahamika kama National Re-entry Implementation Plan, unaeleza kwa kina jinsi ya kuweka mazingira wezeshi ili binti au kijana anaporejea shuleni aweze kubaki na kumaliza mzunguko wa elimu.

"Sisi kama wadau hatutaki mtoto wa kike adondoke tena. Ndiyo maana mpango huu unalenga kuondoa vikwazo vyote vinavyomzuia kuendelea na masomo yake," amesema.

Wito wa mshikamano

TEN/MET imesisitiza kuwa pamoja na hatua hizi muhimu, bado kuna kazi kubwa ya kuelimisha jamii, kuimarisha miundombinu ya shule, na kuhakikisha ugharamiaji wa elimu unakuwa wa kutosha na wa kijinsia.

"Hatujafika pale tunapopataka, lakini tunaelekea huko. Tunahitaji ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi, na jamii ili kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma," amehitimisha.

Tenmet inaamini kuwa kwa mikakati madhubuti na ushirikiano wa karibu na Serikali, Tanzania inaweza kufikia elimu bora na jumuishi kwa wote.