Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini: Mapigano yasababisha WFP kudondoshea wahitaji misaada kutoka angani

Mifuko ya mtama ikishushwa kutoka kwa ndege katika Jimbo la Jonglei, Sudan Kusini.
© WFP/Samantha Reinders
Mifuko ya mtama ikishushwa kutoka kwa ndege katika Jimbo la Jonglei, Sudan Kusini.

Sudan Kusini: Mapigano yasababisha WFP kudondoshea wahitaji misaada kutoka angani

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani,  (WFP) limeanza kudondosha misaada ya dharura ya chakula kwa njia ya anga kwa maelfu ya familia katika Jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini, ambako mzozo unaozidi kuongezeka tangu mwezi Machi mwaka huu umelazimu watu kuhama makazi yao na kukaribia kutumbukiza baadhi ya jamii kwenye njaa ya kupindukia.

Taarifaya WFP iliyotolewa leo Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini inasema mgao huu ni wa kwanza kutoka WFP katika kipindi cha zaidi ya miezi minne, na unalenga kuokoa maisha kwa zaidi ya watu 40,000 wanaokabiliwa na njaa kali katika maeneo ya mbali ya kaunti za Nasir na Ulang, maeneo ambayo yanaweza kufikishiwa misaada kwa kudondoshewa kutokea angani pekee.

Mary-Ellen McGroarty, Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Kusini amesema “kwa masikitiko makubwa uhusiano kati ya mzozo na njaa ni dhahiri Sudan Kusini, na tumeshuhudia hili katika miezi iliyopita huko Upper Nile. Bila kuongeza msaada huu kwa kiwango kikubwa, kaunti za Nasir na Ulang ziko katika hatari ya kuingia kwenye baa kamili ya njaa. Tunahitaji kufikishia familia hizi chakula kwa haraka, na tunafanya kila juhudi kuwafikia wale wenye uhitaji zaidi kabla hali haijazidi kuwa mbaya.”

WFP yashusha msaada wa dharura wa chakula kupitia ndege angani kwa maelfu ya watu katika Jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini.
©WFP/Peter Louis
WFP yashusha msaada wa dharura wa chakula kupitia ndege angani kwa maelfu ya watu katika Jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini.

Watu milioni 1 Upper Nile wana njaa kali

WFP inasema zaidi ya watu milioni moja jimboni Upper Nile wanakabiliwa na njaa kali, wakiwemo zaidi ya watu 32,000 wanaopitia viwango vya juu kabisa vya njaa au (IPC5) ambacho kiwango cha juu zaidi cha uhaba wa chakula.

Idadi hii imeongezeka mara tatu tangu kuzuka kwa mapigano mwezi Machi, ambayo yamesababisha watu wengi kukimbia makazi yao, wakiwemo waliovuka mpaka kwenda Ethiopia ambako WFP inatoa msaada wa chakula kwa watu takribani 50,000 waliokimbia kutoka Upper Nile wakitafuta chakula na usalama.

WFP inalenga kuwafikia watu 470,000 jimboni Upper Nile na Jonglei Kaskazini wakati wa msimu wa mwambo, ambao ni kipindi kigumu zaidi cha mwaka kwa upatikanaji wa chakula, kinachoendelea hadi mwezi Agosti.

Hata hivyo mapigano yanayoendelea pamoja na changamoto za kiufundi vimekuwa vikwazo kwa upatikanaji na mwitikio kamili. Hadi sasa mwaka huu, WFP imeweza kuwafikia watu 300,000 tu jimboni Upper Nile.

Watu wakibeba magunia ya nafaka baada ya ndege kushuka nje ya Pieri katika Jimbo la Jonglei nchini Sudan Kusini.
© WFP/Samantha Reinders
Watu wakibeba magunia ya nafaka baada ya ndege kushuka nje ya Pieri katika Jimbo la Jonglei nchini Sudan Kusini.

Njia za usafirishaji kupitia mito zifunguliwe

WFP inasema ili iweze kufanikisha kazi zake, njia kuu za mto zinazoingia katika jimbo hilo zinapaswa kufunguliwa kwa haraka ili kuwafikishia familia zenye njaa msaada endelevu wa kibinadamu.

Njia hizo ndizo zenye gharama nafuu zaidi kufikisha msaada mkubwa kwa maeneo ya Upper Nile na Jonglei Kaskazini, lakini zimekuwa zimefungwa kutokana na mapigano tangu katikati ya Aprili.

Tayari WFP ina tani 1,500 za chakula tayari kwa kusafirishwa pindi njia za mto zitakapoanza kutumika tena.