Marekebisho ya ushirikiano wa kimataifa ni muhimu- Guterres
Marekebisho ya ushirikiano wa kimataifa ni muhimu- Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametumia hotuba yake kwenye mkutano wa viongozi wa nchi zinazounda BRICS huko Rio de Janeiro, Brazil, kutoa wito wa kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa na kuboresha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa.
BRICS ni kifupi cha kiingereza cha wanachama waasisi wa kundi hilo ambazo ni Brazil, Urusi, China na Afrika Kusini, ambapo sasa wamefikia 11 wakiwemo wanachama wapya Saudi Arabia, Misri, Ethiopia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Iran na Indonesia, huku washirika wapya ni Belarus, Bolivia, Kazakhstan, Thailand, Cuba, Malaysia, Nigeria, Vietnam, Uganda na Uzbekistan.
“Wakati huu ambapo ushirikiano wa kimataifa unadhoofishwa, tukumbushe dunia kuwa ushirikiano ni uvumbuzi mkubwa zaidi wa mwanadamu. Ushirikiano unaanza na uaminifu, na uaminifu huanzia kwa kuheshimu sheria za kimataifa na mataifa yote, bila ubaguzi wowote,” amesema Katibu Mkuu katika hotuba yake kwenye mkutano huo wa 17 unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, masuala ya kiuchumi na kijamii, pamoja na akili bandia.
“Tuchukue hatua inayostahili: tuboreshe na tufanye mageuzi ya mfumo wa ushirikiano wa kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa na taasisi zote, ili ziwahudumie watu wote, kila mahali,” amesema Guterres.
Kuweka mwelekeo chanya kwenye akili mnemba, AI.
Akitambua kuwa akili mnemba (AI) inabadilisha uchumi na jamii, Katibu Mkuu amesema ni muhimu kupunguza hatari na kuongeza manufaa chanya ya AI.
Amesema anahofia sana matumizi ya AI kama silaha, katika dunia ambayo sasa inahitaji amani kuliko wakati mwingine wowote.
Kwa mujibu wake, akili mnemba “inahitajika kujibiwa kwa njia ya pamoja ya kimataifa, inayozingatia usawa na haki za binadamu.”
amekumbusha kuwa Mkataba wa Zama Zijazo ulioidhinishwa na nchi wanachama wa UN, unatoa wito wa kuwekwa kwa mfumo mpya wa uaminifu na ushirikiano, ikianzia na kuanzishwa kwa Jopo la Kimataifa la Kisayansi Huru kuhusu Akili Mnemba, litakalotoa mwongozo usioegemea upande wowote, unaotegemea ushahidi, na litakalopatikana kwa nchi zote wanachama.
“AI haiwezi kuwa ya wachache tu, bali lazima inufaishe wote, hasa nchi zinazoendelea, ambazo zinapaswa kuwa na sauti halisi katika usimamizi wa kimataifa wa AI,” amesema Bwana Guterres, na kuongeza kuwa atawasilisha ripoti hivi karibuni itakayopendekeza njia bunifu za hiari za kufadhili ujenzi wa uwezo wa AI katika nchi zinazoendelea.
Kupambana na sintofahamu kuhusu mifumo ya dunia
Hata hivyo, kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa UN, haiwezekani kusimamia AI kwa ufanisi – na kwa haki – bila kushughulikia mizani ya kina ya kimuundo iliyo ndani ya mfumo wa dunia.
“Tunaishi katika enzi ya ulimwengu wa nguvu nyingi. Mizani ya nguvu inabadilika. Dunia ya aina hii inahitaji utawala wa pamoja wa kimataifa, kupitia taasisi zinazolingana na nyakati hizi, ikiwa ni pamoja na Baraza la Usalama na mfumo wa kifedha wa kimataifa,” amesisitiza.
Amekumbusha kuwa taasisi hizi “zilibuniwa kwa ajili ya enzi iliyopita, dunia iliyopita, yenye mfumo wa zamani wa mahusiano ya nguvu.” Kwa mujibu wake, mageuzi ya Baraza la Usalama “ni jambo muhimu mno.”
Ameeleza kuwa ujumbe kutoka kwa Mkutano wa Ufadhili kwa Maendeleo uliofanyika wiki iliyopita huko Seville nchini Hispania ulikuwa wazi: kuhakikisha ushiriki mkubwa wa nchi zinazoendelea katika uongozi wa kiuchumi duniani na taasisi zake; kuweka mfumo bora wa kurekebisha madeni; na kutripu uwezo wa kukopesha wa mabenki ya maendeleo ya kimataifa, ikijumuisha mikopo nafuu na ya ndani ya sarafu ya taifa.
“Haya yote ni muhimu kwa nchi – hasa zile za kusini mwa dunia – kuweza kuvuka pengo la kidijitali na kutumia kikamilifu uwezo wa akili bandia, na kuifanya kuwa chombo chenye nguvu cha ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu,” amesisitiza.