Namba ya simu ya huduma yasaidia wakulima vijijini Rwanda kujikomboa

Chantal anatumia simu yake ya mkononi kupiga namba 845 ili apate huduma za kilimo.
Namba ya simu ya huduma yasaidia wakulima vijijini Rwanda kujikomboa
Ukuaji wa Kiuchumi
Wakati Chantal alipoona kwamba wadudu walikuwa wameanza kuharibu mazao yake ya thamani ya mahindi, alijua ni wapi pa kuomba msaada. Alichukua simu yake ya kiganjani na kupiga namba 845.
Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD kupitia wavuti wake umechapisha makala hii kuadhimisha siku ya maendeleo vijijini inayoadhimishwa tarehe 6 mwezi Julai kila mwaka.
“Kwa kupitia namba hii 845 ya kupiga bila gharama yoyote, tunapata mafunzo bila kuacha kazi zetu,” anasema Chantal, akiongeza kuwa, “Unapewa maelekezo ya kubonyeza namba tofauti kulingana na mafunzo unayotaka kufuata.”
Kwa kufikia mojawapo ya mafunzo manane yanayopatikana kwenye huduma ya simu ya kujibu kiotomatiki, Chantal amejifunza namna ya kutambua wadudu waliokuwa wakiharibu mazao yake, pamoja na viuatilifu sahihi vya kuwaua na jinsi ya kuvitumia kwa usalama.
Chantal si pekee aliyenufaika na huduma hii ya simu. Akiwa sehemu ya kikundi cha ushirika cha Imirasire kilichoko mashariki mwa Rwanda, ameona wanachama wengine 30 wakipata ushauri wanaohitaji ili kuongeza mavuno yao. Na kama Katibu wa ushirika huo, ameona jinsi hali ya kifedha ya wanachama ilivyoimarika kwa njia isiyokuwa ya kawaida.
Suluhisho kwa vipindi vya ukame
Ushirika wa Imirasire ulianzishwa mwaka 2018 na hukodisha ardhi kutoka serikalini ili kulima mahindi, maharagwe aina ya soya, pamoja na mboga. Katika eneo lao lililo kwenye miteremko na ukijani kibichi , wakulima wameweza kuvuna mara tatu kwa mwaka.
Lakini kutokana na kuongezeka kwa ukame, Chantal amepata shida kumwagilia mazao yake maji ya kutosha, akitumia mabeseni na sufuria kumwagilia.

Mwanamke anachambua mbegu za mahindi kwa ajili ya kuzihifadhi kaskazini mashariki mwa Rwanda.
Ingawa ushirika umepatiwa wanachama chakula kwa bei nafuu wakati wa shida, hali ngumu ilizidi kuwa ya kawaida na ikatishia mustakabali wa wakulima.
Miaka miwili iliyopita, wanachama wa ushirika walijulishwa kuhusu STARLIT, mpango wa dola 483,470 unaofadhiliwa na Mfuko wa China kupitia IFAD ambao ni Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo. Mpango huo IFAD - SSTC, wenye lengo la kuongeza ustahimilivu wa wakulima wadogo nchini Kenya na Rwanda uligeuka kuwa msaada uliokuja kwa wakati mwafaka.
Kupitia STARLIT, Chantal na wakulima wenzake wameweza kubadilisha maisha yao. Wanaweza kupata huduma za ugani wa kilimo kwa lugha yao wakati wowote bila kutoka kazini, kwa kupiga tu namba 845 na kuunganishwa na mfumo wa kujibu kiotomatiki ulioandaliwa na jukwaa la kidijitali, VIAMO na kuidhinishwa na Bodi ya Kilimo ya Rwanda.
STARLIT pia uliunganisha ushirika na taasisi za kifedha, kuwawezesha kupata mikopo midogo kwa ajili ya vifaa vya umwagiliaji vinavyoendeshwa kwa nishati ya jua, hivyo mashamba yao yanapata maji hata wakati wa kiangazi.
Kupata upeo mpya
Kupitia ongezeko la kipato chake kutoka kwenye kilimo, Chantal ameweza kutimiza ndoto yake ya kuwa na biashara ya pili. Baada ya kulipia ada za shule na bima ya afya kwa watoto wake watatu na kununua shamba jipya ambako analima migomba, Chantal amenunua kifaa alichosubiri kwa miaka 20: Cherehani ya kushonea nguo. Sasa, anapata kipato cha ziada kwa kushonea wanawake wa eneo hilo nguo.
Wakati huo huo, Claude, mwenyekiti wa ushirika wa Imirasire, ameweza kusafiri hadi Kenya kwa ziara ya kujifunza kupitia STARLIT. Amerejea na mawazo mapya na mbinu kama vile kuwaalika wasambazaji kuweka zabuni, kushirikiana vyema na wauzaji wa pembejeo za kilimo kama mbolea kwa bei nafuu, na kuhifadhi mazao kwa usalama baada ya mavuno ili kuyauza kwa bei nzuri msimu unapopita.

Chantal ameketi kwenye cherehani yake.
Matokeo chanya
Kama Chantal, Claude sasa ana uwezo wa kuwekeza katika elimu na afya ya watoto wake, na bado hubaki na fedha za kununua mifugo.
Wanachama wa ushirika huu ni miongoni mwa wakulima wadogo 3,400 waliotumia huduma ya 845 kwa mafunzo ya kilimo. Habari kuhusu huduma hii zilisambaa kwa kasi: karibu nusu ya wakulima waliopokea mafunzo hawakulengwa moja kwa moja na mradi, bali walijulishwa na wenzao.
Wakiwa na maarifa mapya, vifaa na pembejeo za kilimo, wakulima wadogo kama Claude na Chantal wameona mazao yao yakistawi. Ambapo zamani walivuna tani 1.5 za mahindi kwa ekari, sasa wanapata hadi tani 6.
Wakulima hawa wanawekeza si tu kwenye mashamba yao, bali pia katika maisha yao binafsi. Chantal tayari ana mipango ya kuboresha biashara yake ya ushonaji – hivi karibuni, anatumaini kununua mashine ya kushonea ya umeme na kuona maono yake ya ubunifu yakitimia.