Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

‘Fikra za umoja’: Jinsi ushirika unavyoimarisha amani Sudan Kusini

Kuhusisha vijana wa Sudan Kusini katika shughuli za kilimo kunaweza kuwazuia kujitumbukiza kwenye vitendo vya uhalifu.
UN Photo/Gregorio Cunha
Kuhusisha vijana wa Sudan Kusini katika shughuli za kilimo kunaweza kuwazuia kujitumbukiza kwenye vitendo vya uhalifu.

‘Fikra za umoja’: Jinsi ushirika unavyoimarisha amani Sudan Kusini

Ukuaji wa Kiuchumi

Ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, ushirika wa wakulima wa mahindi na mtama wenye wanachama 20 katika Jimbo la Equatoria ya Kati, nchini Sudan Kusini, ulikua hadi kufikia wanachama zaidi ya 150, na hivyo kuwawezesha wanachama wengi kuongeza kipato chao na kuweza kuwahudumia familia zao kwa mara ya kwanza.

“Ushirika ni mfumo unaowawezesha raia wa Sudan Kusini kuboresha maisha yao, lakini pia unachangia katika Uchumi. Hii ndio njia pekee ya Sudan Kusini kuondokana na umasikini,” amesema Louis Bagare, Meneja wa Miradi ya Ushirika katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) nchini Sudan Kusini.

Alikuwa akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuelekea Siku ya Kimataifa ya Ushirika, inayoadhimishwa kila tarehe 5 Julai, ambayo huangazia namna vyama vya ushirika vinavyowawezesha watu kukidhi mahitaji yao ya msingi hasa katika mazingira ambayo mtu binafsi hawezi kufanikisha kwa peke yake.

Njia ya kuelekea amani

Mkulima Sudan Kusini akilima shambani mwake.
© FAO/Daniel Chaplin
Mkulima Sudan Kusini akilima shambani mwake.

Nchini Sudan Kusini, uwezo wa vyama vya ushirika unazidi kuonekana kuwa zaidi ya kuwainua kiuchumi. “Ushirika ni mojawapo ya njia zinazoweza kuleta amani na utulivu nchini Sudan Kusini,” amesema Bw. Bagare.

Kwa zaidi ya muongo mmoja, Sudan Kusini imekumbwa na changamoto mbalimbali zinazochangamana. Baada ya kupata uhuru wake mwaka 2011, vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka na kuhitimishwa mwaka 2018 kwa makubaliano ya amani. Hata hivyo, amani hiyo bado ni dhaifu sana.

Wizi wa kutumia nguvu na mapigano baina ya jamii, hasa yanayochochewa na vijana, bado ni changamoto kubwa kwa jamii nyingi ambazo tayari zinakumbwa na uhaba mkubwa wa chakula na mishtuko ya mara kwa mara ya hali ya hewa.

Katika hali hii, vyama vya ushirika vinatoa mwanga wa matumaini. “Ushirika ulibadilisha mtazamo wa watu wetu na kuleta utulivu nchini,” amesema Deng William Achiek, Mkurugenzi wa Wazalishaji vijijini katika Wizara ya Kilimo na Usalama wa Chakula ya Sudan Kusini.

Lakini ni nini hasa kinachofanya vyama vya ushirika kuwa njia ya kuleta amani ya kudumu?

Kikundi cha hiari na kidemokrasia

Ushirika ni shirika la kiuchumi la hiari ambalo wanachama hushiriki kwa pamoja katika hatari, kazi na mapato.

“Ushirika ni chama cha kijamii na kidemokrasia cha watu ambao, kila mmoja akiwa peke yake, hawezi kuboresha hali yake ya maisha na hadhi ya kijamii... lakini wanapoungana katika ushirika, wanaweza kuinua viwango vyao vya maisha,” amesema Oneil Yosia Damia, Mkurugenzi Mkuu wa Maendeleo ya Ushirika Sudan Kusini.

FAO nchini Sudan Kusini imepatia wana ushirika wa wakulima wanawake mafunzo ya uzalishaji wa mbegu.
© FAO/Daniel Chaplin
FAO nchini Sudan Kusini imepatia wana ushirika wa wakulima wanawake mafunzo ya uzalishaji wa mbegu.

Bwana Bagare kutoka FAO anaamini kwamba aina hii ya uongozi wa kidemokrasia katika ngazi za chini inaweza kuenea hadi ngazi ya kitaifa na kuchochea ushirikiano mpana zaidi katika mfumo wa kidemokrasia kote Sudan Kusini.

Mapato badala ya bunduki

Mbali na kutoa mfano wa uongozi wa kidemokrasia, vyama vya ushirika pia vinawezesha ukuaji wa uchumi na maendeleo, na kutoa njia mbadala endelevu kwa jamii — hasa kwa vijana — badala ya kujihusisha na uporaji.

“Wakati hasa vijana wanapojihusisha na shughuli za uzalishaji zinazowapatia mapato, hawatakuwa na hamu ya kuchukua bunduki ili kwenda kupigana au kupora,” amesema Bw. Bagare.

Nchini Sudan Kusini, jamii zinazounda vyama vya ushirika mara nyingi hazina rasilimali za kutosha za mtu binafsi kuweza kuendesha maisha yao kwa njia endelevu, jambo ambalo linawasukuma vijana kujiingiza katika uporaji wa kutumia nguvu ili kuishi.

“Wakati wanajamii wanapofanya kazi pamoja, wakileta mawazo pamoja, wakileta rasilimali pamoja, huwa rahisi zaidi kwao kushinda changamoto za maisha,” amesema Bwana Bagare.

Halikadhalika amesema kuwa benki huwa tayari zaidi kuwekeza kwa vikundi, na mashirika kama FAO yana uwezekano mkubwa wa kutoa msaada kwa vyama vya ushirika. Lakini hatimaye, lengo ni kwamba msaada huo usiwe wa kudumu.

“Lengo ni kujenga uwezo wao ili waweze kuunda maisha,” amesisitiza Bwana Bagare.

Muundo wa kihistoria katika nchi changa zaidi duniani

Nchini Sudan Kusini, kuna vyama vya ushirika vya aina tofauti na ukubwa mbalimbali. Kwa kiasi kikubwa, vyama hivi vinahusiana na kilimo, lakini vingine vinazalisha sabuni, mkate na nguo. Historia ya Sudan Kusini imejaa mifano ya kazi za aina hii.

“Ushirika si kitu kipya. Umekuwa sehemu ya utamaduni wa Sudan Kusini,” amefafanua Bwana Bagare.

Kwa Bwana Daima amekumbusha “kipindi cha dhahabu” cha vyama vya ushirika ambacho kilikuwepo kabla ya vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2011.

Amesema ofisi yake katika Wizara ya Kilimo na Usalama wa Chakula inafanya kazi kwa bidii kurudisha kipindi hicho.

“Nataka vyama vyetu vya ushirika viwe na harakati  'kama nyuki. Huu ndio moyo wa umoja,” amesema Bwana Daima.

Ingawa hivyo Bwana Bagare ana matumaini ya siku zijazo ambapo vyama vya ushirika vitakuwa sehemu ya kila sekta ya uchumi nchini Sudan Kusini — si kilimo tu.

Ametamatisha akisema, “Iwapo tutaweza kufanya kazi pamoja, tunaweza kuwa watu bora kesho. Lakini tukiendelea kupigana sisi kwa sisi, tutaendelea kujiharibu wenyewe.”