Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kibinadamu Gaza yazidi kuzorota, Guterres azungumza

Mvulana akiwa amesimama eneo la Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza kichwa chake kikiwa kimefungwa bandeji kutokana na mashambulizi yanayoendelea.
© UNICEF/Eyad El Baba
Mvulana akiwa amesimama eneo la Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza kichwa chake kikiwa kimefungwa bandeji kutokana na mashambulizi yanayoendelea.

Hali ya kibinadamu Gaza yazidi kuzorota, Guterres azungumza

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameshtushwa na kuzidi kuzorota kwa hali ya kibinadamu huko Ukanda wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric kupitia taarifa aliyotoa Alhamisi mchana, New York, Marekani amemnukuu Guterres akisema kuwa mashambulizi mengi katika siku za hivi karibuni yameharibu makazi ya wakimbizi wa ndani na vile vile maeneo ya mgao wa vyakula.
 
Mashambulizi pia yamesababisha vifo vya raia na wengine wengi wamejeruhiwa ambapo Guterres, “amelaani vikali vifo vya raia.”
 
“Katika siku moja tu wiki hii, maagizo ya kuhama yamewalazimu takriban watu 30,000 kukimbia tena, bila kuwa na mahali salama pa kwenda na bila mahitaji ya msingi kama malazi, chakula, dawa au maji,” amesema Guterres.

Sheria ya kimataifa ya kibinadamu iko wazi kabisa

Katibu Mkuu amesema raia lazima waheshimiwe na walindwe, na mahitaji ya watu lazima yatimizwe.
“Kwa kuwa hakuna mafuta yaliyoingia Gaza kwa zaidi ya wiki 17, nina wasiwasi mkubwa kwamba mbinu za mwisho za kuokoa maisha zinayoyoma,” amesema Katibu Mkuu.
 
Amesema bila kufikishwa kwa mafuta ya dharura mashine za kusaidia watoto wachanga kupumua zitazimika, magari ya wagonjwa hayatakuwa na uwezo wa kuwafikia majeruhi na wagonjwa, na maji hayatakuwa na uwezo wa kusafishwa. Halikadhalika, hatua za Umoja wa Mataifa na wadau wake za kuwasilisha misaada ya kibinadamu na kuokoa maisha zitakwama kabisa.

Misaada ifikishwe bila mkwamo

Guterres ametoa wito tena wa upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa ukamilifu, kwa usalama na kwa uendelevu ili misaada iweze kuwafikia watu waliokosa mahitaji ya msingi ya maisha kwa muda mrefu mno.
 
Amekumbusha kuwa, Umoja wa Mataifa una mpango wa wazi na uliothibitishwa, unaozingatia misingi ya kibinadamu, wa kufikisha misaada muhimu kwa raia – kwa usalama na kwa kiwango kikubwa, popote walipo.
 
Katibu Mkuu anasisitiza tena kwamba pande zote lazima zitimize wajibu wao chini ya sheria za kimataifa huku akirejea tena wito wake wa kutaka kusitishwa kwa mapigano mara moja na kwa kudumu, pamoja na kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote.