Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Sevilla wafikia tamati kwa kuhuisha matumaini na umoja licha ya maendeleo endelevu kutishiwa

Mkutano wa 4 wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo unanafunga pazia tarehe leo 3 Julai.
UN Photo/Mariscal
Mkutano wa 4 wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo unanafunga pazia tarehe leo 3 Julai.

Mkutano wa Sevilla wafikia tamati kwa kuhuisha matumaini na umoja licha ya maendeleo endelevu kutishiwa

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano muhimu wa Ufadhili kwa Maendeleo uliofanyika Sevilla, FFD4 umekamilika kwa hali mpya ya azma na msisitizo wa kuchukua hatua zinazoweza kubadilisha maisha duniani kote, kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed.

“Matokeo ya kibinadamu ya ongezeko la madeni, mvutano wa kibiashara unaoongezeka, na kupunguzwa kwa msaada rasmi wa maendeleo yamewekwa wazi kabisa wiki hii,” amesema katika kikao cha kufunga mkutano huo muhimu, katikati ya joto kali kusini mwa Hispania.

FFD4-nyuma ya pazia.
UN Photo/Julio Muñoz
FFD4-nyuma ya pazia.

Ushirikiano wa Kimataifa Unafanya Kazi

Hata hivyo, licha ya changamoto hizo, mkutano huu umetoa jibu madhubuti ; waraka wa pamoja unaolenga suluhisho, ukisisitiza tena ahadi zilizowekwa Addis Ababa miaka kumi iliyopita, kwa lengo la “kuhuisha matumaini” kupitia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), na kuonesha kuwa ushirikiano wa kimataifa bado ni muhimu na una ufanisi, amesema Bi. Mohammed.

Amepongeza ahadi ya taifa mwenyeji, Hispania, ya kusaidia kuzindua Jukwaa Jipya la Umoja wa Mataifa la Sevilla kuhusu madeni, Jukwaa la wakopaji akilitaja kuwa ni hatua muhimu kusaidia nchi kusimamia na kuratibu mchakato wa kurekebisha madeni yao.

“Sevilla itakumbukwa si kama mahali pa kutua, bali kama kizindua-hatua cha kuboresha maisha kote duniani,” amesema Carlos Cuerpo, Waziri Mkuu wa Fedha wa Hispania, katika mkutano wa mwisho na waandishi wa habari.

“Aidha, kwa pamoja tumepeleka ujumbe thabiti wa kujitolea na kuamini katika ushirikiano wa kimataifa ambao unaweza kuleta matokeo halisi ya kuweka maendeleo endelevu tena katika mkondo sahihi.”

Li Junhua, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii na Katibu Mkuu wa Mkutano huo, amesema wiki hii imethibitisha kuwa Umoja wa Mataifa ni “zaidi ya jukwaa la majadiliano; ni jukwaa lenye nguvu la suluhisho linalobadilisha maisha.”

“Kule Sevilla, tumeonesha nia ya pamoja kukabiliana na changamoto ngumu na za dharura zaidi za kifedha za wakati wetu,” amesisitiza mkuu huyo wa DESA katika hafla ya kufunga.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed akizungumza kwenye Mkutano wa 4 wa Ufadhili wa maendeleo huko Seville, Hispania.
UN Photo/Juanjo Martín
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed akizungumza kwenye Mkutano wa 4 wa Ufadhili wa maendeleo huko Seville, Hispania.

Mpango Madhubuti wa Hatua

Bi. Mohammed amewaambia wanahabari katika kikao cha kufunga kuwa wajumbe wamefanya “jaribio la dhati na lililochelewa kwa muda mrefu la kukabiliana na mgogoro wa deni,” huku wakilenga kufunga pengo kubwa la fedha kwa ajili ya kufanikisha SDGs za mwaka 2030.

Amesisitiza maeneo matatu makuu ya hatua katika Ahadi ya Sevilla:

  • Kusukuma kwa nguvu uwekezaji ili kufunga pengo la ufadhili wa SDGs
  • Hatua madhubuti za kushughulikia mizigo ya madeni isiyoweza kudumishwa
  • Kuongeza sauti ya nchi zinazoendelea katika maamuzi ya kifedha ya kimataifa

Pamoja na makubaliano hayo, zaidi ya miradi mipya 100 imezinduliwa kupitia Jukwaa la Sevilla la Hatua. Hii inajumuisha kituo cha kimataifa cha kubadilisha deni, muungano wa “kusitisha deni” kwa muda, na ushuru wa mshikamano kwa ndege binafsi na safari za daraja la kwanza kufadhili malengo ya maendeleo na hali ya hewa.

“Jukwaa hili limechochea ushirikiano mpya, suluhisho bunifu ambalo litaleta mabadiliko ya kweli katika maisha ya watu,” amesema Bi. Mohammed. “Hizi si mbadala wa ahadi kubwa za ufadhili, bali ni ishara kwamba fikra bunifu sasa zinaanza kushika kasi.”

Akikiri ukosoaji kutoka kwa mashirika ya kiraia kuhusu ukosefu wa fursa ya kushiriki kwenye mijadala rasmi, ameahidi kusukuma juhudi za kujumuisha zaidi. “Tunawasikia,” ametangaza, na kuongeza kuwa “imani hii inapaswa kujengwa.”

Waandamanaji wakiandamana katika mkutano wa Ufadhili wa Maendeleo huko Sevilla.
UN News/Matthew Wells
Waandamanaji wakiandamana katika mkutano wa Ufadhili wa Maendeleo huko Sevilla.

Muhtasari wa Ahadi Kuu za Sevilla

Kukabili Mizigo ya Madeni:
  • Hispania na Benki ya Dunia kuongoza Kituo cha Mabadilishano ya Deni kwa Maendeleo
  • Italia kubadilisha euro milioni 230 za deni la Afrika kuwa uwekezaji wa maendeleo
  • Muungano wa Kusitisha Deni utawezesha nchi kuahirisha malipo ya deni wakati wa migogoro
  • Jukwaa la Sevilla kuhusu Deni kusaidia nchi kuratibu usimamizi na urekebishaji wa madeni
Kuchochea Uwekezaji:
  • Muungano wa Ushuru wa Mshikamano Duniani kutoza kodi ndege binafsi na safari za daraja la juu ili kufadhili malengo ya hali ya hewa na SDGs
  • Jukwaa la SCALED kupanua fedha mchanganyiko kwa kushirikisha sekta binafsi na ya umma
  • FX EDGE na Delta kusaidia kuongeza mikopo kwa sarafu za ndani kupitia zana za kudhibiti hatari.
  • Brazil na Hispania kuongoza juhudi za kodi ya haki kwa matajiri
  • Vituo vipya vya msaada wa kiufundi kusaidia maandalizi na utekelezaji wa miradi
Kuimarisha Mifumo ya Kifedha:
  • Majukwaa ya kifedha yanayoongozwa na nchi kusaidia mipango ya kitaifa
  • Muungano wa UK-Bridgetown kupanua fedha za kukabiliana na majanga