Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utafiti wa FAO wabaini mazito kuhusu hali ya vijana katika mifumo ya chakula na kilimo

Kama wakulima wa viazi, familia ya Salma ilijiunga na Ushirika wa "Mkulima wa Birahim", ambao ulipata usaidizi muhimu katika kupanua upatikanaji wao wa fedha, masoko, teknolojia na habari.
© FAO/Saikat Mojumder
Kama wakulima wa viazi, familia ya Salma ilijiunga na Ushirika wa "Mkulima wa Birahim", ambao ulipata usaidizi muhimu katika kupanua upatikanaji wao wa fedha, masoko, teknolojia na habari.

Utafiti wa FAO wabaini mazito kuhusu hali ya vijana katika mifumo ya chakula na kilimo

Ukuaji wa Kiuchumi

Kukiwa na vijana wapatao bilioni 1.3 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 duniani kote, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) limezindua ripoti kamili iitwayo The Status of Youth in Agrifood Systems (Hali ya Vijana katika Mifumo ya Chakula na Kilimo), ambayo inachunguza na kusisitiza umuhimu mkubwa wa vijana katika kubadilisha mifumo ya chakula na kilimo ili kuboresha uhakika wa chakula, lishe, na fursa za kiuchumi.

Ripoti hiyo ya FAO iliyowekwa wazi leo Julai 3 inaeleza kuwa karibu asilimia 85 ya vijana duniani wanaishi katika nchi za kipato cha chini na cha kati, ambapo mifumo ya chakula na kilimo ni muhimu kwa ajira na maisha yao. Kuwajumuisha vyema vijana katika mifumo hiyo kunaweza kuleta mchango wa hadi trilioni moja ya dola kwa uchumi wa dunia.

Ripoti inachambua hatua za kiufundi na sera zinazolenga kuunda ajira bora, kuboresha uhakika wa chakula na lishe, na kuongeza uwezo wa vijana kukabiliana na mishtuko. Vijana wanaelezwa kama mawakala muhimu wa mabadiliko katika sekta ya kilimo, wakiwa kizazi kijacho cha wazalishaji, wachakataji, watoa huduma, na watumiaji wa chakula. Wanakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo kuongeza uzalishaji wa chakula kwa ajili ya idadi ya watu inayoongezeka, kuchukua nafasi ya wafanyakazi wanaozeeka, na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa maji, na uhamiaji wa watu mijini.

FAO inaeleza kwamba duniani kote, asilimia 44 ya vijana wanaofanya kazi wanategemea mifumo ya chakula na kilimo, ikilinganishwa na asilimia 38 ya watu wazima. Hata hivyo, viwango hivyo hutofautiana kwa kiasi kikubwa: kuanzia asilimia 82 katika maeneo yenye migogoro ya muda mrefu hadi asilimia 23 tu katika mifumo ya viwanda. Cha kusikitisha ni kwamba ukosefu wa chakula kwa vijana umeongezeka kutoka asilimia 16.7 hadi 24.4 kati ya miaka 2014-2016 na 2021-2023, hasa barani Afrika.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu, Akieleza kuhusu ripoti hiyo anasema: "Ripoti hii inatoa tathmini ya wakati muafaka na yenye ushahidi kuhusu jinsi ajira bora na uhakika wa chakula kwa vijana vinaweza kupatikana kupitia mageuzi ya mifumo ya chakula na kilimo, na jinsi vijana waliowezeshwa wanaweza kuwa kichocheo cha mabadiliko makubwa zaidi."

Kuwawezesha Vijana

Ripoti inaonesha kuwa zaidi ya asilimia 20 ya vijana hawapo katika ajira, elimu au mafunzo (NEET), huku wasichana wakiwa na uwezekano mara mbili zaidi kuingia katika kundi hili. Kutatua tatizo hili na kutoa ajira kwa vijana wenye umri wa miaka 20 hadi 24 wanaokosa fursa hizi kunaweza kuongeza pato la dunia (GDP) kwa asilimia 1.4, sawa na dola trilioni 1.5, ambapo asilimia 45 ya ongezeko hilo linatokana na mifumo ya chakula na kilimo.

Ili kuwawezesha vijana, ripoti inapendekeza hatua zifuatazo:

  • Kuongeza ushiriki wao na uwezo wa kufanya uamuzi;
  • Kuboresha upatikanaji wa mafunzo na rasilimali;
  • Kuwezesha tija ndani na nje ya mashamba;
  • Kupanua programu za ulinzi wa kijamii kutokana na changamoto za upatikanaji wa mikopo ya jadi.

Ripoti pia inaonesha takwimu muhimu kuhusu idadi ya vijana:

  • Asilimia 54 wanaishi mijini, wengi wakiwa Asia Mashariki;
  • Vijana wa vijijini ni asilimia 5 tu ya watu katika mifumo ya chakula na kilimo ya viwanda;
  • Hali hii inaashiria upungufu wa wafanyakazi iwapo kazi za kilimo hazitafanywa kuwa za kuvutia;
  • Vijana wengi wa vijijini wanaishi maeneo yenye uwezekano mkubwa wa uzalishaji wa kilimo, hivyo kuna fursa kubwa za uwekezaji katika miundombinu na masoko.

Matukio ya hali mbaya ya hewa na mishtuko mingine ya tabianchi ni tishio kubwa. Inakadiriwa kuwa vijana milioni 395 wa vijijini wanaishi katika maeneo ambayo uzalishaji wa kilimo unatarajiwa kushuka, hasa Afrika katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.

Takwimu muhimu kwenye ripoti:

  • Idadi ya vijana barani Afrika katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 65 ifikapo mwaka 2050;
  • Asilimia ya vijana wanaofanya kazi katika mifumo ya chakula na kilimo imeshuka kutoka asilimia 54 mwaka 2005 hadi asilimia 44 mwaka 2021;
  • Vijana wenye umri wa miaka 15–24 ni asilimia 16.2 ya wahamiaji wa kimataifa kutoka Afrika katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, na asilimia 15.2 kutoka Amerika ya Kusini na Karibea.

Mikakati mitatu mikuu ya kukabiliana na changamoto:

  1. Kuongeza maarifa: Kupunguza pengo la taarifa na ushahidi kuhusu ushiriki wa vijana katika mifumo ya chakula na kilimo;
  2. Kuwajumuisha zaidi: Kuweka sauti za vijana katika sera na uamuzi;
  3. Kuwekeza aidi: Kuwekeza kwa lengo maalum la kupanua fursa za kiuchumi kwa vijana na kuwawezesha.

Hatua muhimu zinazohitajika:

  • Kupanua Fursa za Kiuchumi: Kuandaa vijana kwa ujuzi na rasilimali zinazohitajika kwenye mifumo ya chakula;
  • Kuwekeza Kisasa: Kuwekeza kwenye miundombinu ili kufanya ajira za kilimo kuwa za kuvutia;
  • Kuwezesha Upatikanaji wa Rasilimali: Kuanzisha mipango ya ardhi na mikopo kwa vijana;
  • Kuhamasisha Uhamiaji Salama: Kuunda njia salama za uhamiaji kwa vijana ili kukabiliana na uhaba wa wafanyakazi;
  • Kuboresha Upatikanaji wa Teknolojia ya Kidigitali: Kuwawezesha vijana wakulima kutumia teknolojia ya kisasa na kufikia masoko kwa urahisi.