Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mji mkuu wa Haiti wazidi kusambaratika, wananchi waunda makundi ya kujilinda

Magenge ya uhalifu yanadhibiti eneo kubwa la mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince.
© UNOCHA/Giles Clarke
Magenge ya uhalifu yanadhibiti eneo kubwa la mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince.

Mji mkuu wa Haiti wazidi kusambaratika, wananchi waunda makundi ya kujilinda

Amani na Usalama

Zaidi ya watu milioni 1.3 wamepoteza makazi yao nchini Haiti kutokana na kuongezeka kwa vurugu zinazoongozwa na magenge ya uhalifu, kutokuwepo kwa utawala wa sheria, na ukosefu wa uwajibikaji—hali inayowaweka watu katika hatari kubwa, hasa wanawake na wasichana, ya kukabiliwa na unyanyasaji na ukatili wa kingono.

Tangu Januari mwaka huu, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala nchini Haiti (BINUH), imeripoti zaidi ya watu 4,000 kuuawa kwa makusudi— ikiwa ni ongezeko la asilimia 24 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024.

Tweet URL

Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano, Miroslav Jenča,  Mkuu wa Masuala ya Amerika katika Idara ya Masuala ya Kisiasa ya Umoja wa Mataifa (DPPA), amesema “mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince umekwama kabisa kimsingi kwa sababu ya magenge ya uhalifu na kutengwa kutokana na kusitishwa kwa safari za kimataifa za kibiashara katika uwanja wa ndege wa kimataifa.”

Baada ya kufanya ziara nchini humo hivi karibuni, ameonya kuwa kuwa magenge  ya uhalifu“yameimarisha makazi yao,” na sasa yanaathiri kila eneo la jiji la Port-au-Prince na maeneo ya karibu, “na kusukuma hali halisi kukaribia kufikia ukingoni.”

Ameitaka  jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti na za haraka, akisema “kusambaratika kabisa kwa uwepo wa dola katika mji mkuu kunaweza kuwa hali halisi kabisa.”

Magenye ya uhalifu yapanua maeneo yao

Ghada Fathi Waly, Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), amesisitiza suala hilo.

Akihutubia wajumbe wa Baraza, kutoka Vienna, Uswisi kwa njia ya video, amesema, “kadri magenge ya uhalifu yanavyozidi kudhibiti maeneo, uwezo wa serikali kuendesha shughuli zake unazidi kupungua kwa kasi, hali inayokuja na madhara ya kijamii, kiuchumi na kiusalama.”

“Kudhoofika huku kwa uhalali wa dola kuna madhara makubwa,” amesea, akiongeza kuwa, huku biashara halali ikikwama kutokana na magenge kudhibiti njia kuu za biashara—hali inayozidisha kiwango kikubwa tayari cha uhaba wa chakula na mahitaji ya kibinadamu.

Makundi yaibuka ya watu kujilinda

Kufuatia hasira kubwa ya umma dhidi ya uwezo mdogo wa serikali kutoa ulinzi, makundi ya “wanamgambo” au ya kujilinda yameanza kupata uungwaji mkono kutoka kwa wananchi.

Ingawa baadhi yao wanasukumwa na haja ya kulinda jamii zao, mengi yao yanatekeleza shughuli nje ya mfumo wa sheria, na katika baadhi ya matukio wanahusiana moja kwa moja na magenge au kufanya mauaji ya kiholela.

Kuongezeka kwa makundi haya kumesababisha ongezeko la mahitaji ya silaha na silaha za kijeshi, “hali inayochochea masoko haramu ya silaha na kuongeza hatari ya silaha halali kuangukia mikononi mwa wahalifu,” amesema Bi. Waly.

Biashara haramu ya binadamu

Wakati huo huo, kuzorota kwa usalama na hali ya kiuchumi katika mji mkuu na maeneo mengine ya nchi kunaendelea kuongeza ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Licha ya kutotolewa taarifa nyingi za ukatili wa kingono kutokana na hofu ya kulipiziwa kisasi, unyanyapaa wa kijamii, na ukosefu wa imani kwa taasisi, BINUH imeripoti ongezeko la matukio ya ukatili wa kingono unaofanywa na magenge ya uhalifu katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Polisi wavamia eneo linalodaiwa kuuza viungo vya binadamu

Mwezi Mei mwaka huu, polisi wa Haiti walivamia kituo cha afya katika eneo la Pétion-Ville kilichoshukiwa kuhusika katika biashara haramu ya viungo vya binadamu, huku madai ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya uchukuaji wa viungo yakianza kuibuka.

Kwa kuwa hali nchini Haiti inazidi kuwa mbaya, “hakuna muda wa kupoteza,” amesisitiza Bwana Jenča.