Jukwaa la wakopaji laanzishwa kupaza sauti dhidi ya wakopeshaji

Jukwaa la wakopaji laanzishwa kupaza sauti dhidi ya wakopeshaji
Mfumo mpya unaotoa njia kwa nchi zinazokabiliwa na matatizo ya madeni kuratibu hatua na kukuza sauti yao katika mfumo wa kifedha wa kimataifa, umezinduliwa kwenye mkutano muhimu wa Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo endelevu huko Sevilla nchini Hispania.
Ukipatiwa jina Jukwaa la Wakopaji linatambuliwa kuwa hatua muhimu katika juhudi za mageuzi ya mfumo wa kimataifa wa madeni, likiwa limeungwa mkono na Umoja wa Mataifa na likionekana kuwa sehemu kuu ya hati ya matokeo ya Makubaliano ya Sevilla.
"Hii si maneno tu – huu ni utekelezaji," amesema Waziri wa Mipango na Maendeleo ya Kiuchumi wa Misri, Dkt. Rania Al-Mashat. “Jukwaa la Wakopaji ni mpango halisi, unaoendeshwa na nchi, wa kuunda sauti na mkakati wa pamoja katika kukabiliana na changamoto za madeni.”
Rebeca Grynspan, Katibu Mkuu wa UNCTAD ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo, amesema kuwa mara nyingi nchi zinazoendelea hukabili wakopeshaji walioungana huku zenyewe zikijadili zikiwa peke yao.
"Sauti si tu uwezo wa kuzungumza — ni nguvu ya kuathiri kwa uchanya matokeo. Leo, watu bilioni 3.4 wanaishi katika nchi zinazotumia akiba zaidi kwenye ulipaji wa madeni kuliko afya au elimu,” amesema Bi. Grynspan.
Umuhimu wa jukwaa
Jukwaa hilo — moja ya mapendekezo 11 ya Kundi la Wataalamu la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Madeni — litaruhusu nchi kushiriki uzoefu, kupata ushauri wa kiufundi na kisheria, kukuza viwango vya uwajibikaji katika ukopaji na ukopeshaji, na kujenga nguvu ya pamoja ya majadiliano.
Uzinduzi huu unajibu mwito wa muda mrefu kutoka nchi zinazoendelea kwa uamuzi jumuishi zaidi katika mfumo wa madeni unaotawaliwa na maslahi ya wakopeshaji.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia, Mulambo Haimbe, amewaambia waandishi wa habari kuwa juhudi hiyo itakuza "ushirikiano wa muda mrefu, heshima ya pande zote na uwajibikaji wa pamoja", na akaonesha utayari wa nchi yake kuandaa mkutano wa awali.
Waziri wa Fedha wa Hispania, Carlos Cuerpo, ameelezea janga la sasa la madeni kuwa "kimya lakini la dharura," na ameliita Jukwaa hilo kuwa "Wakati wa Sevilla" unaoweza kufanana na Klabu ya Paris ya wakopeshaji, iliyoanzishwa karibu miaka 70 iliyopita.

Mjumbe Maalum wa UN kuhusu Ufadhili wa Ajenda ya 2030, Mahmoud Mohieldin, amesema jukwaa hilo ni jibu la moja kwa moja kwa mfumo uliowaweka nchi zinazodaiwa katika hali ya upweke kwa muda mrefu.
"Hili ni kuhusu sauti, kuhusu haki – na kuhusu kuzuia mgogoro mwingine wa madeni kabla haujaanza,” amesema.
Uzinduzi huu unakuja wakati ambapo matatizo ya madeni yanaongezeka kote katika ulimwengu wa maendeleo.
Makubaliano hayo ya Sevilla, yanayojulikana kwa Kihispania kama Compromiso de Sevilla – yaliyopitishwa kwa muafaka katika mkutano huo, yanajumuisha mkusanyiko wa ahadi kuhusu mageuzi ya madeni ya kitaifa.
Pamoja na kuunga mkono juhudi zinazoongozwa na wakopaji, makubaliano hayo yanataka:
- Uwazi zaidi wa madeni,
- Uratibu ulioboreshwa kati ya wakopeshaji,
- Uchunguzi wa mfumo wa kisheria wa kimataifa kuhusu urejeleaji wa madeni.
Pia yanapendekeza mikakati ya kudumu ya nchi kuhusu uendelevu wa madeni, masharti ya kusimamisha malipo kwa nchi zilizo hatarini kwa mabadiliko ya tabianchi, pamoja na msaada zaidi kwa mpango wa kubadilisha madeni kwa ajili ya mazingira na hali ya hewa — lakini kwa uangalizi mkali zaidi na ushahidi wa athari.
Kauli za mashirika ya raia : Kutokuwepo kwa mageuzi ya kweli ya mfumo wa madeni
Mashirika ya kiraia siku ya Jumatano yalikosoa vikali matokeo ya mkutano wa Sevilla, yakiyaita fursa iliyopotea kuleta mageuzi halisi ya mfumo wa kimataifa wa madeni unaoikandamiza nchi nyingi zinazoendelea.
Katika mkutano na waandishi wa habari ndani ya mkutano huo, Jason Braganza kutoka AFRODAD ambalo ni jukwaa na Mtandao wa Afrika kuhusu Madeni na Maendeleo, amesema kuwa hati ya mwisho iliyopitishwa – Makubaliano ya Sevilla – haikufikia kile kilichohitajika.
"Hati hii haikuanza na matarajio makubwa, lakini bado imepunguzwa zaidi," amesema
"Takribani nusu ya nchi za Afrika zinakabiliwa na mzozo wa madeni. Badala ya kuwekeza kwenye afya, elimu na maji safi, wanawalipa wakopeshaji."
Braganza amesifu uongozi wa Kundi la Afrika na Muungano wa Nchi Ndogo za Visiwa, waliopigania Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu madeni ya kitaifa. Ingawa azma hiyo haikutimia kikamilifu, amekaribisha mafanikio madogo kupitia mchakato mpya wa serikali kwa serikali unaoweza kuandaa msingi wa mageuzi ya baadaye.
Viongozi wa mashirika ya kiraia pia wameonya kuhusu hatari za kile kinachoitwa "ubadilishanaji wa madeni kwa tabianchi", huku Braganza akivitaja kama "majawabu bandia" ambayo hayatoi nafasi halisi ya kifedha kwa nchi zinazoendelea.
Tove Ryding kutoka Eurodad au (Mtandao wa Ulaya kuhusu Madeni na Maendeleo) ameunga mkono wasiwasi huo, akisema:
"Tunaambiwa hakuna pesa za kupambana na umasikini au mabadiliko ya tabianchi — lakini pesa zipo. Tatizo ni ukosefu wa haki wa kiuchumi. Na matokeo ya mkutano huu yanadhihirisha hali ile ile ya kawaida ya mambo."
amesisitiza mafanikio yaliyopatikana kuhusu Mkataba mpya wa Kodi wa UN kama ushahidi kwamba nchi zenye dhamira zinaweza kuleta mabadiliko ya kweli, na kuongeza:
"Laiti tungekuwa na dola ya kodi kwa kila wakati tuliambiwa siku hii haitakuja kamwe."

Makubaliano ya Sevilla yaanza kuzaa matunda kwa afya ya umma
Kusaidia kuziba pengo katika huduma na sera za umma, na kukabiliana na upunguzaji wa huduma za afya ambao unaweza kugharimu maisha ya maelfu, Hispania siku ya Jumatano imezindua Mpango wa Hatua wa Afya ya Ulimwengu, uliolenga kufufua mfumo mzima wa afya wa kimataifa.
Mpango huu utapeleka dola milioni 371 kwenye mfumo wa afya duniani kati ya 2025 na 2027, na unaungwa mkono na mashirika makubwa ya kimataifa ya afya na zaidi ya nchi 10.