IOM yataka uwekezaji wa kibunifu katika uhamiaji

IOM yataka uwekezaji wa kibunifu katika uhamiaji
Katika Mkutano wa nne wa kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo (FFD4) unaoendelea jijini Seville, Hispania, Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limetoa wito wa kuimarisha uwekezaji wa kibunifu katika uhamiaji wa watu ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kusaidia kuziba pengo la kila mwaka la dola trilioni 4 za ufadhili wa maendeleo.
Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope amenukuliwa akisema, “wahamiaji wanachangia katika kila ngazi ya jamii, wanaimarisha uchumi, kuunganisha jamii, na kuongeza uimara wakati wa misukosuko. Hata hivyo, uhamiaji bado hautiliwi mkazo katika mipango na ufadhili wa maendeleo.” Hivyo anashauri akisema,“tunapowekeza katika uhamiaji salama, wenye mpangilio na wa kawaida, tunaleta jamii imara na zilizounganishwa zaidi.”

IOM imetaka uhamiaji kutambuliwa kama kichocheo cha fursa za kiuchumi na mshikamano wa kijamii, ikiwa utaungwa mkono kwa heshima na maono ya muda mrefu. Imeziomba serikali na benki ya maendeleo kuakisi hilo katika upangaji na ufadhili wa miradi yao ya maendeleo.
Hili linahusisha:
- Kujenga mifumo ya kifedha inayofanya uhamiaji kuwa salama na wa kutabirika,
- Kuingiza uhamishaji wa watu kwenye mipango ya maendeleo ya kitaifa,
- Kupunguza gharama za kutuma fedha kutoka ughaibuni,
- Kupanua upatikanaji wa huduma za kidijitali,
- Kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji wa wanadiaspora.
Pia kunahitajika matumizi ya takwimu bora kubaini ni nani aliyelazimika kuhama, mahitaji yao ni nini, na suluhisho gani lina matokeo makubwa zaidi.
Mfumo mmoja uliotajwa ni Mfuko wa Ushirikiano wa Wadau Wengi wa Uhamiaji, chombo cha kifedha cha pamoja kinachounga mkono usimamizi wa uhamiaji jumuishi na wa kuheshimu haki katika nchi za asili, za kupita na za mwisho. Tangu kuzinduliwa, Mfuko huo umefadhili miradi 27 ya pamoja. IOM inahimiza washirika kuongeza mchango ili kufikia lengo la dola milioni 150 ifikapo mwaka 2026.
Matokeo muhimu ya mkutano huo ni Compromiso de Sevilla – azimio la kisiasa la kubadilisha mfumo wa ufadhili wa maendeleo kwa kuzingatia ushirikishwaji, uendelevu na matokeo ya maana. Azimio hilo linaweka mkakati wa pamoja wa kimataifa wa kuziba pengo la kila mwaka la ufadhili la takribani dola trilioni 4 zinazohitajika ili kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Kama mshirika wa Kikosi Kazi cha Mashirika ya Umoja wa Mataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo, IOM inatoa utaalamu kuhusu jinsi uhamiaji, fedha za wahamiaji, uwekezaji wa wanadiaspora, na ufadhili wa wakimbizi vinavyoweza kusaidia kuziba pengo la maendeleo na kuhakikisha msaada unawafikia wahitaji zaidi.