Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nidhamu chanya huchagiza makuzi bora kwa mtoto - UNICEF Tanzania

Mafunzo ya malezi bora ya watoto nchini Tanzania.
UNICEF TANZANIA
Mafunzo ya malezi bora ya watoto nchini Tanzania.

Nidhamu chanya huchagiza makuzi bora kwa mtoto - UNICEF Tanzania

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limekuwa likihimiza umuhimu wa malezi na makuzi chanya kwa watoto kama njia mojawapo ya kulinda haki kuu nne za msingi za mtoto ambazo ni kuishi, kuendelezwa, kushirikishwa na kulindwa.

Nchini Tanzania, Alinune Nsemwa, Mtaalamu wa masuala ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto katika Ofisi ya UNICEF Tanzania anataja vigezo vitatu muhimu vya malezi bora kwa watoto wa kitanzania.

“Dokezo namba moja. Tenga muda wa kukaa na kumsikiliza pamoja na kuzungumza na mtoto wako. Muulize siku yako inaendaje. Muulize changamoto alizozipata katika siku yake, lakini mambo gani pia amefurahia. Mazungumzo ya namna hii yanamsaidia mtoto kuweza kujiamini, kuwaamini watu wengine. Lakini pia kuelewa kuwa anapendwa anajaliwa na kuwa rahisi kwake kujua kwamba yupo salama.”

Vipi kuhusu kidokezo namba mbili?

“Tumia nidhamu chanya. Kama mtoto akikosea, mweleze kosa lake na namna gani ya kuweza kufanya kwa usahihi. Mtoto hujifunza vizuri zaidi anapokelewa kwa upendo, furaha, lakini pia kwa subira na siyo kwa kujengewa hofu.”

Na kisha akataja kidokezo namba tatu akisema..

“Mpe mtoto fursa ya kucheza michezo na umuhimu mkubwa kwa mtoto katika ukuaji na ustawi wake. Iwasaidie watoto kupata fursa ya kucheza. Tunawawezesha watoto waweze kujifunza lakini waweze kujiamini waweze kuwa wabunifu. Bila kusahau malezi bora yanahusisha afya bora, lishe ya kutosha, ulinzi na usalama kwa mtoto. Ujifunzaji wa awali pamoja na malezi yenye mwitikio.”