UNDP yahimiza ubunifu wa vyanzo vya mapato ili kuvutia wawekezaji

UNDP yahimiza ubunifu wa vyanzo vya mapato ili kuvutia wawekezaji
Mkutano wa 4 wa Ufadhili wa Maendeleo (FFD4) ukiendelea huko Sevilla Hispania, juhudi za kuhakikisha nchi zinajitegemea kifedha kupitia vyanzo jumuishi na vya ubunifu zimezidi kupewa kipaumbele. Katika hafla ya kufungua mafunzo ya Muongozo wa Upatikanaji wa Fedha kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, au Intergrated Local Financing Framework (ILFF) yaliyofanyika katika Manispaa ya Morogoro kaskazini-mashariki mwa Tanzania hivi majuzi , Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la Mpango wa Maendeleo nchini humo, UNDP umetoa mafunzo ya namna halmashauri zinaweza kuandaa mikakati madhubuti ya kuhimiza maendeleo ya ndani kupitia ushirikiano kati ya sekta binafsi, mashirika ya kiraia, benki na jamii.
Lengo ni kuendelea kuunga mkono serikali na wadau mbalimbali barani Afrika katika kutafuta mbinu mbadala za kufadhili maendeleo.
Mafunzo ya Muongozo wa Upatikanaji wa Fedha kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa yaliratibiwa na Chuo cha Mipango, (IRDP) kwa ufadhili wa UNDP. Mratibu Mkuu wa Malengo ya Maendeleo Endelevu – Fedha na Uwekezaji kutoka UNDP, Emmanuel Nnko anazitaka halmashauri zote nchini Tanzania zibuni vyanzo vipya vya mapato ambavyo si tu shirikishi bali pia vinavyovutia uwekezaji endelevu na lengo ni kuondokana na utegemezi wa bajeti kuu ya serikali.
“Kwanza, zinatambua vyanzo vyao vya sasa vya mapato, na pia kuchambua vyanzo hivyo kwa undani zaidi. Wanapaswa kutathmini ni vyanzo gani vinaweza kuongezewa thamani au kuboreshwa kwa njia ya ubunifu ili kuweza kuongeza kiwango cha mapato yanayokusanywa zaidi ya kile kinachopatikana sasa. Aidha, zinatakiwa kuanza kuzingatia vyanzo vingine mbadala vya fedha, vinavyojulikana kama alternative financing. Baada ya tathmini hiyo, tutashirikiana nazo kuandaa mpango mkakati wa utafutaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi waliyojiwekea kwa mwaka ujao wa fedha wa 2025-2026-2027”

Katika mpango huu, UNDP inahimiza ushirikishwaji wa pande zote, akisema, "Mpango huo utakuwa wa kijumuishi, ambapo hautatekelezwa na serikali ya halmashauri husika pekee, bali utawahusisha pia wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi, asasi za kiraia, pamoja na wabia wa maendeleo wenye miradi katika halmashauri husika. Vilevile, wananchi kwa ujumla watashirikishwa ili kuhakikisha kuwa yale yanayopangwa na kutekelezwa si mali ya halmashauri pekee, bali ni maamuzi yanayotokana na mashauriano ya pamoja katika ngazi zote husika."
Suala la miradi k utekelezwa kwa wakati likasisitizwa na Johnson L. K Nyingi, Mkurugenzi Msaidizi – Uratibu wa Shughuli za Serikali kutoka Idara ya Tawala, Tanzania. Anasema “Mradi unapaswa kuhusisha watu katika hatua zote za utekelezaji. Kuna vyanzo mbadala vya fedha vinavyopatikana. Hii inatupa fursa ya kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa mipango ili kuleta ufanisi. Tunaona ushirikiano huu kama mfano bora wa mashirikiano ya kimaendeleo, na tuna matarajio makubwa kwamba huu ni mwanzo mzuri wa hatua endelevu. Ni mfano halisi wa jinsi miradi inaweza kujiendesha kwa ufanisi endapo wadau wote watashirikishwa ipasavyo.”
Bonamax Mbasa, Mratibu wa MAfunzo kutoka Chuo ya Mipango akamulika hoja ya kuhakikisha miradi inafikia wananchi akisisitiza kuwa “Hii ni miongoni mwa majukumu yetu kama Chuo cha Mipango—kutoa huduma za ushauri kwa wadau wa maendeleo. Halmashauri ni miongoni mwa wadau wetu muhimu, ambapo tunawapa mafunzo ya kitaalamu kutokana na tafiti tulizofanya. Utafiti wetu umebaini kuwa kuna changamoto kubwa ya gharama katika utekelezaji wa miradi katika ngazi ya halmashauri. Miradi mingi hushindwa kutekelezwa kwa wakati, na mingine hufutwa kabisa kutokana na ukosefu wa fedha. Hivyo basi, tunawawezesha kuandaa mwongozo utakaowasaidia kupata rasilimali fedha za kugharamia miradi hiyo, sambamba na kuongeza mapato ya ndani. Mwongozo huo ni sehemu ya mpango mkakati wa miaka 5, uliobuniwa kwa lengo la kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati kama ilivyopangwa.”