Hispania na Brazil zasukuma hatua za kimataifa kutoza kodi kwa matajiri wakubwa ili kupunguza ukosefu wa usawa
Hispania na Brazil zasukuma hatua za kimataifa kutoza kodi kwa matajiri wakubwa ili kupunguza ukosefu wa usawa
Hispania na Brazil wamezindua mpango wa pamoja wa kimataifa wa kuongeza ukusanyaji wa kodi kutoka kwa matajiri wakubwa duniani, kwa lengo la kukabiliana na ongezeko la ukosefu wa usawa ili kuhakikisha kuwa wale walio na mali nyingi wanachangia ipasavyo.
Mpango huo uliowasilishwa wakati wa Mkutano wa 4 wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo ulioingia siku ya pili mjini Sevilla, nchini Hispania, na unasisitiza tatizo linalozidi kukua: watu matajiri zaidi mara nyingi huchangia kidogo katika fedha za umma ukilinganisha na walipa kodi wa kawaida, kutokana na viwango vya chini vya kodi na mianya ya kisheria.
“Nchi zetu zinahitaji mapato zaidi ya umma ili kukidhi mahitaji yake. Ukosefu wa usawa ni tatizo kila mahali, na matajiri hulipa kodi kidogo kuliko watu wa tabaka la kati – hata kidogo kuliko walipa kodi wa kipato cha chini,” amesema Waziri wa Masuala ya Fedha wa Hispania, Jesús Gascón, wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika eneo la mkutano, ambako joto limepanda hadi kufikia viwango vya juu vya kihistoria katika siku za hivi karibuni.
Serikali hizo mbili zinatoa wito kwa nchi nyingine kujiunga katika juhudi za kuanzisha mfumo wa kodi wa kimataifa ulio wa haki na wa maendeleo. Wanasisitiza ukweli mchungu: asilimia moja ya watu matajiri zaidi duniani wanamiliki zaidi ya asilimia 95 ya mali yote ya binadamu.
Kushirikiana maarifa, kuziba mianya
Katika dunia ya sasa iliyounganishwa, upatikanaji wa takwimu ya kuaminika ni muhimu. Mpango huu unapendelea ushirikishwaji wa taarifa – kati ya serikali na mamlaka za kodi – kusaidia kufichua mapungufu katika mifumo ya kodi, kufunga mianya, na kupambana na ukwepaji na uepukaji wa kodi.
Kuboresha ubora wa takwimu na kujenga uwezo wa kitaifa wa uchambuzi wa takwimu kutasaidia mamlaka za kodi kubaini mali ilipojilimbikizia, kiasi gani kinacholipwa kwa sasa, na ni mabadiliko gani yanahitajika.
Ingawa hatua fulani tayari zimepigwa, nchi hizo zinasema bado kuna kazi kubwa ya kufanya na nchi nyingi zaidi zinapaswa kujiunga.
“Kuna haja halisi ya kujua nani hasa ni wamiliki halisi wa kampuni na miundo ya kisheria inayotumika kuficha utajiri,” amesema Bwana Gascón. Mpango huu pia unapendekeza ushirikiano wa kiufundi, mafunzo ya uchambuzi wa data, na mifumo ya mapitio ya nchi kwa nchi ili kuimarisha mifumo ya kitaifa ya kodi.
Jedwali la kimataifa la mali?
Hispania na Brazil pia wanazingatia hatua za kuelekea kwenye kuanzisha jedwali la kimataifa la utajiri – wakitambua kuwa hili litahitaji muda, utashi wa kisiasa, na juhudi kubwa za kitaifa.
Lakini lengo ni wazi: uwazi zaidi, uwajibikaji zaidi, na mchango wa haki kutoka kwa matajiri wakubwa.
“Hatupaswi kuvumilia ukali wa ukosefu wa usawa, ambao umekuwa ukiongezeka katika miaka ya hivi karibuni,” amesema Mshauri Mkuu wa Brazil katika Umoja wa Mataifa, José Gilberto Scandiucci, akikanusha kuwa hili ni ajenda ya mrengo wa kushoto.
“Huu ni mpango wa wastani wa kukabiliana na hali halisi iliyo kali sana.”
Pendekezo hili ni sehemu ya Jukwaa la Hatua la Sevilla, ambalo linahamasisha hatua za hiari kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) – ambayo kwa sasa yako nyuma kwa ajili ya kufikiwa ifikapo mwaka 2030.
G20 yasema ‘matajiri wa hali ya juu’ ni kipengele muhimu
Mpango huu pia unakuja kufuatia makubaliano ya mwaka 2024 ya nchi 20 zenye viwanda zaidi duniani, (G20) waliokutana Rio, Brazil – ambayo ndiyo makubaliano ya kwanza ya kimataifa ya kushughulikia kodi ya watu matajiri sana.
Mpango wa kazi wa miezi mitatu sasa unaandaliwa, huku mikutano ya mara kwa mara ikipangwa kufuatilia maendeleo. Lengo: kuzihusisha nchi zaidi, mashirika ya kimataifa na jamii ya kiraia ili kusukuma mbele mageuzi ya kodi yanayowalenga matajiri wakubwa zaidi.
“Iwapo tunataka kutoza kodi kwa ufanisi kwa matajiri wa kupindukia, kupambana na ukosefu wa usawa na kufanya mifumo yetu ya kodi iwe ya haki na yenye maendeleo zaidi, tunahitaji utashi wa kisiasa – na tunahitaji kuchukua hatua kwa kutumia rasilimali tulizonazo,” ameongeza Bwana Gascón.