Miaka 15 mambo 15: Changamoto na suluhisho kwa usawa wa kijinsia
Miaka 15 mambo 15: Changamoto na suluhisho kwa usawa wa kijinsia
Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masuala ya wanawake, UN Women linapotimiza miaka 15 mwaka huu wa 2025, dunia imepiga hatua muhimu katika usawa wa kijinsia ambazo zimebadilisha maisha ya wanawake na wasichana kote duniani. Hii ni sababu ya kusherehekea, lakini harakati za kusukuma mbele usawa wa kijinsia zinapoteza mwelekeo.
Utafiti wa Machi 2025 unaonesha ongezeko la asilimia 60 ya wasiwasi kuhusu ukosefu wa maendeleo katika usawa wa kijinsia. Takwimu za UN Women kutoka zaidi ya ripoti 150 za serikali zinathibitisha hali hiyo: karibu nchi 1 kati ya 4 imeathirika. Ukatili wa kijinsia unaongezeka. Pengo la kijinsia katika matumizi ya teknolojia linapanuka. Zaidi ya wanawake na wasichana milioni 600 sasa wanaishi karibu na maeneo ya migogoro.
Katika hali hii ya kihistoria lakini hatarishi, mafanikio yaliyopatikana yanatishiwa kurudi nyuma. Ni wakati wa uongozi thabiti na kujitolea kwa dhati kutimiza ahadi zilizowekwa katika Ajenda ya 2030, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama, na Azimio la Beijing.
Kwa kusukuma mbele usawa wa kijinsia, UN Women inatoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua 15 zifuatazo:
1. Kushughulikia msukosuko dhidi ya haki za wanawake:
Mnamo 2024, karibu nchi 1 kati ya 4 ziliripoti kurudi nyuma kwa haki za wanawake, mdororo mkubwa katika juhudi za usawa wa kijinsia.
Suluhisho: Nia ya kisiasa lazima ifufuliwe ili kulinda mafanikio yaliyopatikana na kuhakikisha mifumo ya kisheria, kisiasa na kifedha inaendeleza usawa wa kijinsia.
2. Kumaliza migogoro
Mnamo mwaka 2023, takriban wanawake na wasichana milioni 612 waliishi ndani ya kilomita 50 kutoka eneo lenye migogoro- zaidi ya asilimia 50 kuliko miaka 10 iliyopita.
Suluhisho: Kuongeza uwekezaji katika kuzuia migogoro, upatanishi na ujenzi wa amani.
3. Kukuza ushiriki wa wanawake katika mchakato wa amani
Amani hudumu zaidi wanawake wanaposhiriki. Lakini kati ya mwaka 2020–2023, mazungumzo 8 kati ya 10 ya amani hayakuwahusisha wanawake.
Suluhisho: Wajumbe wa migogoro na wadau wahakikishe ushiriki kamili, sawa na wa maana wa wanawake katika michakato ya amani.
4. Kutokomeza umaskini
Mwanamke au msichana 1 kati ya 10 anaishi katika umaskini wa kupindukia (chini ya dola 2.15 kwa siku). Kwa kasi ya sasa, itaichukua miaka 137 kumaliza hali hii.
Suluhisho: Serikali zitekeleze sera za ulinzi wa kijamii kama msaada wa kifedha, likizo ya uzazi ya kulipwa, na pensheni salama.
5. Kumaliza uhaba wa chakula
Wakulima wadogo, wengi wao wakiwa wanawake, huzalisha 1/3 ya chakula cha dunia, lakini wanawake milioni 47.8 zaidi ya wanaume wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Suluhisho: Sheria na sera zifungue fursa sawa kwa wanawake katika kilimo na malipo.
6. Kukomesha ukatili dhidi ya wanawake
Mwanamke au msichana mmoja huuawa kila dakika 10 na mwenza au jamaa. Jumla ya wanawake na wasichana 85,000 waliuawa kimakusudi mwaka 2023.
Suluhisho: Sheria zibadilishwe, takwimu ziboreshewe, na mashirika yanayowasaidia manusura yapate ufadhili.
7. Kukuza ushiriki wa wanawake katika ukuaji wa uchumi
Wanawake hufanya kazi ya kulea bila malipo mara 2.5 zaidi ya wanaume, ikijumuisha jumla ya saa milioni 250 kwa siku zinazotumika kuteka maji - mara tatu zaidi ya wanaume na wavulana, na hivyo kuwazuia kupata kazi rasmi.
Suluhisho: Uwekezaji katika mifumo ya huduma na ajira bora unaweza kuunda ajira milioni 300 ifikapo 2035 hivyo kuboresha maisha na Uchumi
8. Kuondoa pengo la malipo ya kijinsia
Ulimwenguni, wanawake bado wanapata asilimia 20 chini ya wanaume kwa kazi ya thamani sawa. Pengo la mishahara linasalia kuwa ukweli kwa wanawake, likichochewa na kutofautiana kwa kimuundo kama vile mgawanyo wa kazi, adhabu za ulezi, na ubaguzi unaoendelea.
Suluhisho: Malipo sawa kwa kazi sawa, uwazi wa mishahara, fursa zaidi kwa wanawake, na likizo ya uzazi ya haki kwa wote na kuimarisha sheria dhidi ya ubaguzi mahali pa kazi
9. Kulinda Sayari
Mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuwatumbukiza wanawake na wasichana milioni 158 zaidi katika umaskini wa kupindukia ifikapo 2050. Ni asilimia 28 tu ya mawaziri wa mazingira ni wanawake-licha ya ushahidi wa wazi kwamba uongozi wa wanawake unaongoza kwa sera bora zaidi za hali ya hewa.
Suluhisho: Wanawake washirikishwe kwa usawa katika uongozi wa kimazingira na kufadhili suluhisho zinazotokana na wanawake.
10. Kuongeza uongozi wa wanawake katika siasa
Takriban asilimia 75 ya wabunge ni wanaume, na nchi 103 hazijawahi kuwa na kiongozi mwanamke.
Suluhisho: kupambana na kanuni za kijamii na unyanyapaa unaowarudisha nyuma wanawake na kukomesha unyanyasaji unaowalenga wanapoingia madarakani.
11. Kuondoa mifumo ya kisheria ya kibaguzi
Wanawake wana haki asilimia 64 tu ya haki za kisheria ambazo wanaume wanazifaidi. Katika asilimia 51 ya nchi, kuna angalau kizuizi kimoja kinachozuia wanawake kufanya kazi sawa na wanaume.
Suluhisho: Sheria zote za ubaguzi zibadilishwe ili kuendeleza haki za wanawake.
12. Kufunga pengo la kidijitali la kijinsia
Mnamo mwaka 2024, wanaume milioni 277 zaidi ya wanawake walitumia mtandao wa intaneti. Iwapo pengo la jinsia ya kidijitali litaendelea nchi za kipato cha chini na cha kati zitapoteza dola bilioni 500 ya mapato katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Suluhisho: Kuondoa vikwazo vya kijinsia katika teknolojia na kukomesha ukatili wa kidijitali dhidi ya wanawake. Vikwazo vya ushiriki sawa na uongozi wa wanawake na wasichana katika sayansi, teknolojia na uvumbuzi lazima viondolewe.
13. Kuhakikisha usawa wa kijinsia katika elimu
Wasichana milioni 119 bado hawapo shuleni. Asilimia 39 ya wanawake vijana hawamalizi shule ya sekondari.
Suluhisho: Kupunguza gharama za elimu, kutoa misaada ya kifedha, na kuhakikisha mazingira salama ya kujifunzia.
14. Komesha vifo vya wajawazito
Takriban wanawake 800 hufariki dunia kila siku kutokana na sababu zinazozuilika za ujauzito-asilimia 61 ya vifo hivi hutokea katika nchi 35 tu zilizoathiriwa na migogoro.
Suluhisho: Kuwekeza katika huduma za afya ya uzazi zilizo salama na nafuu, na kuimarisha mifumo dhaifu ya afya.
15. Kuongeza ufadhili kwa usawa wa kijinsia
Ni asilimia 4 tu ya misaada rasmi ya maendeleo iliyoelekezwa moja kwa moja kwenye usawa wa kijinsia mwaka 2021–2022.
Suluhisho: Mashirika ya umma na binafsi lazima yaongeze uwekezaji katika usawa wa kijinsia kama msingi wa maendeleo endelevu.