Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana wakumbatia kilimo bunifu kupambana na mabadiliko ya tabianchi Kajiado Kenya

Norah Makena, Mtaalamu wa kilimo wa Edmund Rice Dairies huko huko Embulbul, Kajiado Kenya anatoa  mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa jamii inayomzunguka.
UN News
Norah Makena, Mtaalamu wa kilimo wa Edmund Rice Dairies huko huko Embulbul, Kajiado Kenya anatoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa jamii inayomzunguka.

Vijana wakumbatia kilimo bunifu kupambana na mabadiliko ya tabianchi Kajiado Kenya

Tabianchi na mazingira

Kwa mujibu wa wataalamu wa kilimo, teknolojia imefungua njia mpya ya kuinua maisha ya wakulima wadogo, hasa kwa kutumia ukulima wa kisasa unaotumia maarifa na Teknolojia. Sharon Jebichii anatupeleka kaunti ya Kajiado, Kenya, katika eneo la EMbulbul, kukutana na vijana wanaotumia maarifa ya kilimo cha kisasa kubadilisha maisha yao na ya jamii.

Ni Abel Ongidi ni kijana mpenda mazingira na mwanzilishi  wa kikundi cha kijamii cha Mpenda Mazingira Initiative. Anawahamasisha  wakazi wa maeneo ya mijini na vijijini kutunza mazingira na kuendeleza kilimo kwa njia bunifu.

“Tutaangazia ukulima mdogo unaofanyika nyumbani, unaojulikana kama Kitchen Gardening. Kama hautaki kununua mboga sokoni, anza kupanda mboga nyumbani, iwe kwenye kibaraza au mahali popote penye nafasi kidogo. Hiyo nafasi ndogo inaweza kuongeza uzalishaji wa kilimo chako. Hakikisha kuwa shamba lako lina mboga , mahindi na  matunda. Kwa kufanya hivi, utaweza kupunguza matumizi ya pesa na pia utalinda mazingira yako.”

Abel Ongidi huyu, kijana mpenda mazingira na mwanzilishi  wa kikundi cha kijamii cha Mpenda Mazingira Initiative kutoka Kajiado Kenya.
UN News
Abel Ongidi huyu, kijana mpenda mazingira na mwanzilishi wa kikundi cha kijamii cha Mpenda Mazingira Initiative kutoka Kajiado Kenya.

Kwa Abel, kilimo si tu chanzo cha chakula bali ni fursa kwa vijana. Anasema, vijana wakihamasishwa kuhusu uzuri wa kilimo, watabadilisha mtazamo na kuona kuwa kilimo kinaweza kuwa chanzo cha kipato.

Pale nyumbani, waoneshe vijana uzuri wa kufanya ukulima. Hii itahamasisha vizazi vijavyo kuendelea kuhifadhi mazingira yetu na kuyafanya kuwa safi na kijani kibichi. Kutoka hapa nyumbani hadi maeneo mengine, tutaona mazingira yanavyobadilika kuwa ya kijani kabisa. Kilimo inaweza kuleta fursa nyingi. Fanya vijana wajue kuwa ukulima ni chanzo cha kipato.”

kwa upande wake Norah Makena, mtaalamu wa kilimo wa Edmund Rice Dairies huko huko Embulbul, Kajiado anatoa  mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa jamii inayomzunguka. Anaeleza kuhusu umuhimu wa kutumia teknolojia na njia bunifu kuongeza tija kwa wakulima wadogo.

Nora anasema kilimo cha kisasa haijalishi kama shamba lako ni kubwa au ndogo, bali ni mbinu na malengo yako. Shirika letu lina  malengo mawili, elimu na maendeleo. Tunataka jamii ijifunze kujiendeleza wenyewe  bila kutegemea wengine.  Hata hivyo, unahitaji mtaji ili kuboresha mbinu zako za kilimo. Pia, ujuzi maalum unahitajika kufanya kazi kwa ufanisi. Sisi tunatumia vifaa vilivyorejelewa kama plastiki na magunia, ili kutumia nafasi ndogo vyema na kupata mazao mengi kwa juhudi kidogo. Bustani hizi ni rahisi kutunza. Tunapolima, tunataka pia majirani waige mfano huu ili wajitegemee na waache kununua mboga.

Soundcloud

Kwa Makena, kutoa maarifa ni msingi wa kuimarisha maisha ya wakulima, hivyo anasema “Wakulima wanapaswa kupata mafunzo kutoka kwa wataalamu ili waelewe kilimo kisichotumia kemikali badala ya kutegemea mbolea za kemikali. Pia, wanahitaji ujuzi wa masoko ili wauze mazao yao kwa faida.Mkulima anaweza kufanikiwa na ukulima lakini anakosa uelewa wa masoko.  Mafunzo kuhusu misimu ya kupanda mimea ni muhimu. Pia tunasisitiza wakulima wajifunze mabadiliko ya hali ya hewa na mimea inayofaa kulimwa katika maeneo yao. Katika Edmund Rice Dairies, tunatoa mafunzo bure kwa wakulima ili kuwasaidia kutumia mbinu bora za kilimo na kuongeza uzalishaji wao kwa hatua.”