Ni wakati wa kufadhili mustakabali wetu na kubadilisha mwelekeo, Guterres awaambia viongozi wa dunia huko Sevilla

Ni wakati wa kufadhili mustakabali wetu na kubadilisha mwelekeo, Guterres awaambia viongozi wa dunia huko Sevilla
“Tupo hapa Sevilla kubadilisha mwelekeo,” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewaambia viongozi wa dunia Jumatatu, akiwaalika watumie fursa hii ya kipekee inayotokea mara moja kwa muongo mzima kuziba pengo la ufadhili la dola trilioni 4 linalozikabili nchi zinazoendelea ili kutimiza malengo ya maendeleo endelevu na kujenga dunia bora kwa wote.
António Guterres ametoa wito huu akibainisha kuwa “maendeleo endelevu yanayochochewa na ushirikiano wa kimataifa sasa yanakumbana na vikwazo vikubwa.”
Akihutubia kikao cha ufunguzi cha Mkutano wa 4 wa Ufadhili wa Maendeleo (FFD4) katika joto kali la Sevilla Hispania likiwa limevunja rekodi za joto kwa mwezi Juni Katibu Mkuu amesema ushirikiano wa kimataifa nao pia unakumbana na changamoto, huku imani miongoni mwa mataifa na taasisi ikidhoofika.
Dunia inawaka moto, ikitikiswa na ukosefu wa usawa, machafuko ya mabadiliko ta tabianchi na migogoro inayoongezeka, “Ufadhili ndio injini ya maendeleo na kwa sasa, injini hii inayumba,” amewaambia wajumbe wa mkutano, ambao ni zaidi ya viongozi 50 wa dunia, kutoka nchi 150 na wajumbe wapatao 15,000.
“Tunapokutana, Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu ambayo ni ahadi yetu ya kimataifa ya kubadilisha dunia yetu kwa mustakabali bora na wa haki zaidi ipo hatarini.”
Takriban theluthi mbili ya malengo makuu ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yaliyoafikiwa mwaka 2015 yako nyuma kwa kiasi kikubwa na hivyo kuhitaji uwekezaji mkubwa wa dola trilioni 4 ili kurekebisha hali hii.
“Tupo hapa Sevilla kubadilisha mwelekeo. Kurekebisha na kuongeza kasi ya injini ya maendeleo ili kuchochea uwekezaji kwa kiwango na kasi inayohitajika,” amesema Bwana Guterres.
Ameelezea azimio linalojulikana kama Ahadi ya Sevilla iliyopitishwa Jumatatu bila Marekani ambayo ilijiondoa mapema mwezi huu kama “ahadi ya kimataifa kwa mataifa yenye kipato cha chini ili kuyapandisha juu katika ngazi ya maendeleo”.

Katibu Mkuu amebainisha maeneo matatu muhimu ya hatua:
• Kwanza, kuhakikisha rasilimali zinatiririka haraka ndani ya nchi ili kuchochea ukuaji endelevu, na kwa nchi tajiri kutimiza ahadi yao ya kuongeza mara mbili misaada kwa nchi maskini ili kuongeza maendeleo. Hii inajumuisha kuongeza mara tatu uwezo wa mikopo wa Benki za Maendeleo za Kimataifa na suluhu bunifu za kufungua mitaji binafsi.
• Pili, kurekebisha mfumo wa madeni wa dunia ambao “hauwezi kuhimilika, hauko sawa na hauna unafuu.” Kwa sasa, nchi maskini zinatumia takriban dola trilioni 1.4 kulipia riba za madeni yao makubwa. Miongoni mwa suluhu mpya ni jukwaa jipya la wakopaji litakalohakikisha utatuzi wa haki wa madeni na hatua stahiki.
• Tatu, kufanya mageuzi katika mfumo wa kifedha wa dunia, kwa wanahisa wakuu kuchukua jukumu lao, ili uweze kuwawezesha wote. “Tunahitaji mfumo wa ushuru wa kimataifa ulio wa haki na unaoundwa na wote, si wachache pekee.”
Mgogoro wa sasa wa gharama na maendeleo yaliyokwama ni “mgogoro wa watu,” ameendelea, unaoziacha familia zikiwa na njaa, watoto bila chanjo na wasichana wakiachwa nje ya elimu.
“Mkutano huu hauhusu hisani. Unahusu kurejesha haki na kuwezesha kila mtu kuishi kwa heshima,” amesema Bwana Guterres.
“Mkutano huu hauhusu fedha unahusu uwekezaji katika mustakabali tunaotaka kuujenga pamoja.”

Ramani ya njia dhahiri na inayotekelezeka
Mfalme Felipe wa Hispania alizungumza muda mfupi kabla ya ufunguzi rasmi, akiwaambia wajumbe kuwa jiji lenye tamaduni nyingi la Sevilla linaikaribisha dunia “kwa mikono miwili.”
Alisema ramani mpya ya njia itatokana na kile ambacho ni “cha dhahiri, cha kutekelezeka na kinachoweza kuchukuliwa hatua.”
Mkutano lazima uwe wa mafanikio, kwani ushirikiano ni nguzo kuu ya mfumo wa kimataifa wa pande nyingi na “mfano wa mwisho wa maadili yanayouendeleza hasa katika kipindi hiki cha kihistoria ambapo uhakika mwingi unayeyuka na hofu na wasiwasi vinachukua nafasi.”
Wakati wetu ni sasa
Rais wa Hispania Pedro Sánchez amewaambia wajumbe, “wakati wetu ni sasa na mahali petu ni hapa.” Maisha ya mamilioni ya watu yatategemea maamuzi yatakayofanywa Sevilla na siku za usoni.
Lazima tuchague “uthubutu badala ya kufa moyo, mshikamano badala ya kutojali na ujasiri badala ya urahisi,” ameendelea, akiongeza kuwa “macho ya dunia yako kwenye ukumbi huu, kuona kile tunachoweza kufanya pamoja na mbele ya changamoto hii ya kihistoria lazima tudhihirishe thamani yetu.”
Sevilla ilikuwa “New York ya karne ya 16” kwa maneno ya kidiplomasia, amewaambia wajumbe na ni kitovu cha kimataifa sote tunapaswa kulipa jiji hili urithi huo leo.

Sevilla sio mwisho
Katibu Mkuu wa mkutano, Li Junhua anayesimamia Idara ya Masuala ya Uchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa (DESA) amesema wiki hii Sevilla ni wakati muhimu wa kuhamasisha rasilimali zinazohitajika kujenga mustakabali wa haki, jumuishi na endelevu.
Juhudi za Umoja wa Mataifa za kufadhili maendeleo zimejikita kwenye ushirikiano wa kimataifa na mshikamano lakini leo, mfumo mzima uko chini ya “shinikizo kubwa.”
Amesema maendeleo endelevu hayajawahi kujaribiwa hivi, lakini mkataba uliopitishwa Sevilla unawarudisha watu katikati ya suala hilo muhimu.
“Sevilla sio mwisho, bali ni jukwaa la kuzindua enzi mpya ya utekelezaji, uwajibikaji na mshikamano.” UNDESA iko tayari kusaidia mataifa yote kutafsiri ahadi hii kuwa hatua za kimataifa, amesisitiza.
Rais wa Baraza Kuu la UN Philémon Yang amewaambia wajumbe juu ya yote, “tunahitaji uongozi wa kuiongoza dunia kuelekea mustakabali wenye mwangaza na ustawi kwa kila mtu, kila mahali.”
Amesema mfumo wa Sevilla utahuisha ushirikiano wa kimataifa kwa muongo unaokuja na kutoa mkazo kwa mzigo wa madeni unaokandamiza dunia inayoendelea.
Rais wa Baraza la Uchumi na Kijamii la Umoja wa mataifa Bob Rae amesema imani miongoni mwa nchi lazima iimarishwe, kwani ukosefu wake “unaleta vurugu.”
“Zaidi ya yote, ninapongeza nchi kwa kuonesha uthubutu na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za kifedha.” Wiki hii inawakilisha ahadi ya kweli ya kuchukua hatua, amesema.
Ajay Banga, Rais wa Benki ya Dunia, amewaambia wajumbe kuwa kumaliza umaskini bado ni jukumu lake kuu na ongezeko la idadi ya watu katika nchi zinazoendelea linahitaji rasilimali kwa kiwango na kasi ambavyo havijawahi kushuhudiwa.”
Amesema kila mtu anajua kuwa serikali, mashirika ya hisani na taasisi haziwezi kutimiza kila makadirio au ahadi ndio maana sekta binafsi ni muhimu kwa Mkataba wa Sevilla ili mitaji iweze kutiririka.
Bwana Banga ameongeza kuwa mageuzi ya benki katika miaka ya karibuni yanahusu kuwa mshirika bora kwa sekta binafsi na wateja wa serikali.
Kuboresha muda wa hatua, kuongeza mitaji na mifumo ya ukuaji ni muhimu lakini zaidi inahitajika ili kutimiza malengo kwa vizazi vijavyo.

Kusamehe mataifa duni ushuru wa adhabu: WTO
Ngozi Okonjo-Iweala, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) amesema mkutano unafanyika wakati wa ugumu wa kipekee.
Baada ya miongo ya mafanikio, mfumo wa biashara wa kimataifa sasa umekumbwa na zahma sana na kufanya mauzo ya nje kukwama kutokana na ushuru wa upande mmoja na ukosefu wa uhakika wa sera kiasi kwamba WTO imeshusha makadirio ya ukuaji.
Vikwazo zaidi vya ushuru kufikia tarehe 9 Julai muda uliowekwa na serikali ya Marekani vitafanya mdororo wa biashara duniani kuwa mbaya zaidi.
Amekumbusha kuwa WTO imependekeza nchi maskini na Afrika kwa jumla zisamehewe ushuru huo, “ili tuzibidishe vizuri zaidi katika mfumo wa biashara wa dunia na si kuzitenga zaidi.”
Amesema Mkataba wa Sevilla unatambua kwa usahihi biashara ya kimataifa kama injini ya maendeleo.
“Hivyo tunapaswa kuimarisha uthabiti na uhakika katika biashara ya kimataifa,” kupitia hatua katika viwango vingi ambavyo vinaweza kukuza rasilimali za kitaifa kupitia mauzo ya nje, amewaambia wajumbe.
IMF yaomba msingi mpana wa ushuru
Nigel Clarke, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ametoa wito wa kupanua msingi wa ushuru, kujenga mifumo thabiti ya usimamizi wa kifedha, kuratibu msaada na kushughulikia madeni kwa njia endelevu zaidi.
“Nchi nyingi bado zinapambana na gharama kubwa za riba,” amesema, akiitaka jumuiya ya kimataifa kuboresha mchakato wa kurekebisha madeni.
Ameongeza kuwa kupitia maendeleo ya uwezo, Shirika linawezesha wanachama wake kuchora ramani zao wenyewe na pia linatoa msaada wa kifedha wakati wanapouhitaji zaidi.